MKURUGENZI Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania
(TGNP), Usu Mallya amefungua mafunzo ya Ukatili wa Kijinsia na Haki za
Binadamu kwa kundi la washiriki kutoka mikoa na taasisi anuai za umma na
binafsi ili kuwajengea uwezo juu ya mapambano ya masuala upiganiaji
haki kwa jamii.
Akizungumza na washiriki wa semina hiyo, Bi. Mallya aliwataka
washiriki kutumia nafasi waliopata ipasavyo kwa kuhakikisha wanafuatilia
mafunzo vizuri ili kila mmoja atoke kama malozi wa chachu ya mapambano
juu ya vitendo vyote vya kikatili kwa jamii na masuala ya haki za
binadamu.
Aliwaeleza washiriki kila mmoja kwa nafasi aliyonayo sasa anaweza
kuwa chachu ya mabadiliko endapo atatimiza wajibu wake kwenye eneo
alipo. Alisema suala la ukatili wa kijinsia ni suala mtambuka nchini
kwani limeenea karibuni kila eneo la nchi, hivyo kuna kila sababu ya
kuzidisha mapambano dhidi yake.
“…Kwa kweli suala la ukatili wa kijinsia ni suala mtambuka kwenye
maeneo yote ya nchi yetu, twakwimu za kitaifa zinatuambia takribani
asilimia 40 ya wanawake wote wamekwisha fanyiwa ukatili wa namna moja
ama nyingine, kwa kila wanawake wawili mmoja ameshafanyiwa ukatili wa
kijinsia…wengine tumepigwa, wengine tumefanyiwa ukatili wa kiuchumi,
kisaikolojia…,” alisema Mallya.
Aidha Mallya aliongeza kuwa ukatili wa kijinsia kwa sasa katika mfumo
wa utandawazi lipo kila upande bila kujali ni kwa wanawake au wanaume,
kwani kila mmoja anaathirika na suala hilo. Alisema lengo la mafunzo
kama hayo ni kuona mabadiliko katika mfumo juu ya kujali na kuheshimu
haki za makundi yote, yaani haki za watoto, haki za kijamii, haki za
watu wenye ulemavu, haki za wanawake haki za vijana n.k.
Alisema kuwa nchi nyingi za Bara la Afrika zinapambana na mifumo
miwili mikubwa, ambayo ni mfumo wa kitabaka unaoongeza nafasi kati ya
matajiri na masikini (walio nacho na wasionacho) na mfumo dume ambao nao
umekuwa ukiwakandamiza wanawake katika jamii.
Mafunzo hayo yanaendeshwa na Chuo cha Mafunzo ya Jinsia (GTI) ambacho
kilianzishwa na TGNP ili kuratibu mafunzo anuai ya jinsia chini ya
mwamvuli wa TGNP. Miongoni mwa washiriki katika semina hiyo ni
wawakilishi kutoka madawati ya jinsia ya Jeshi la Polisi, mahakama,
idara ya ustawi wa jamii, washiriki kutoka asasi za watu wenye ulemavu
na wasio na ulemavu na baadhi ya wajumbe kutoka mikoa kadhaa ya
Tanzania.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)