Msimamizi
wa Mradi wa Bara bara tatu za Vijijini za Unguja kutoka Wizara ya
Miundo Mbinu na Mawasiliano Mhandisi Suleiman Abdulla Ali akimpatia
maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
aliyetembelea mradi huo katika Bara bara ya Cheju – Jendele – Kaebeona.Kati
kati yao aliyevaa kofia ya Kiua ni Waziri wa Wizara hiyo Rasdhid Seif
na pembeni ya Mhandisi Suleiman ni Mshauri Muelekezi waMradi huo Kutoka
Kampuni ya Newtech Consulting Group ya Nchini Sudan El- Tayeb Rabah
Mohammed
Mshauri
Muelekezi wa Mradi huo Kutoka Kampuni ya Newtech Consulting Group ya
Nchini Sudan El- Tayeb Rabah Mohammed akimuhakikishia Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif ujenzi wa bara bara zenye
kiwango katika mradi wa bara bara tatu za Vijiji za Unguja huko Cheju
Wilaya ya Kati, Mkoa Kusini Unguja.Picha na Hassan Issa-Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar
--
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewaagiza wataalamu
wanaopata fursa za Ujenzi wa Bara Bara Nchini kuhakikisha kwamba bara
bara wanazozijenga zinakuwa katika kiwango kinachokubakila Kimataifa ili
ziwe na uwezo wa kudumu kwa kipindi kirefu.
Agizo
hilo amelitoa wakati wa ziara fupi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa
Bara bara ya Jendele-Cheju hadi Kaibona yenye urefu wa Kilo mita 11.741
ambayo ni miongoni mwa bara bara iliyomo ndani ya mradi wa ujenzi wa
bara bara tatu za vijijini katika Kisiwa cha Unguja.
Balozi
Seif alisema wapo baadhi ya wahandisi wa ujenzi wa Bara bara wasio
waaminifu ambao baadhi ya wakati hudiriki kuondoa njiani miradi ya
ujenzi wa bara bara wanayopewa bila ya kuzingatia masharti na mikataba
waliyoiridhia.
Alisema
hali hiyo huleta kero kwa wafadhi wa miradi hiyo na mara nyingi kuyatia
hasara Mataifa yenye miradi hiyo ambayo mengine yanashindwa kuihudumia
Miradi husika kutokana na ufinyu wa uchumi wao.
“Baadhi ya Makandarasi
wamekuwa na tabia ya kuondosha njiani kazi wanazopewa za ujenzi tabia
ambayo huwakera wafadhili wa miradi hiyo na kwa upande mwengine
kuyaongezea mzigo Mataifa yenye kusaidiwa ufadhili wa miradi hiyo “. Alisisitiza Balozi Seif.
Akizungumzia
suala la fidia ya vipando, mali pamoja na majengo ya wananchi
wanaoathirika na miradi hiyo Balozi Seif aliiagiza Wizara ya Miundo
Mbinu na Mawasiliano Zanzibar kuwa makini ya baadhi ya watu wajanja
wenye tabia ya kujipandikiza katika madai ya fidia hizo.
Alisema
tabia hiyo ambayo hujichomoza mara kwa mara wakati wa uanzishwaji wa
miradi tofauti katika maeneo mbali mbali Nchini imekuwa ikiitia hasara
kubwa Serikali kwa vile haimo ndani ya jabeti iliyokubalika kwa pande
zote mbili.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliipongeza Kampuni ya ujenzi wa Bara bara
hiyo ya D.P Shapriya +Co. Ltd ya Dara es salaam kwa hatua iliyofikia ya
ujenzi wa mradi huo licha ya kuchelewa kidogo kutokana na msimu wa mvua
za masika.
Mapema
Msimamizi wa Mradi huo wa Bara bara tatu za Vijijini Unguja kutoka
Wizara ya Miundo Mbinu na Mawasiliano Zanzibar Mhandisi Suleiman Abdulla
Ali alisema Serikali kupitia Wizara husika tayari imeshawalipa fidia
wananchi wote waliohusika na ile bara bara ya Jendele- Cheju- hadi
Kaebona.
Mhandisi
Suleiman alimueleza Balozi Seif kwamba tathmini ya fidia imeshafanywa
pia kwa bara bara ya Koani – Jumbi yenye urefu wa Kilo Mita 6.3 kwa
kushirikiana na masheha wa shehia zinazopita bara bara hiyo na Wizara
husika italipa fidia mara tuu fedha zitakapopatikana.
Alifahamisha
kwamba ufinyu wa bajeti ya kazi za ujenzi wa Bara bara hizo za Vijijini
Unguja umepelekea kutolewa kwenye mradi huo kwa Bara bara ya Kizimbani –
Kiboje yenye kilo mita 7.
Msimamizi
huyo wa mradi wa ujenzi wa bara bara hizo alieleza kuwa ujenzi wa kazi
hiyo ulioanza mapema mwezi Januari mwaka huu wa 2013 umegharamiwa na
Benki ya Maendeleo ya Kiislamu { Badea } kwa kushirikiana na SMZ kwa
kiasi cha Shilingi za Kitanzania Bilioni 14,834,615,889.06/-.
Akitoa
maelezo Mshauri muelekezi wa Mradi huo kutoka kampuni ya Newtech
Consulting Group ya Nchini Sudan El-Tayeb Rabah Mohammed alisema kuwa
mradi huo umepangwa kuchukuwa takriban miezi 17 hadi kukamilika kwake mwezi Mei mwaka ujao.
El
– Tayeb alimuhakikishia Makamau wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
kwamba ana matumaini makubwa ya kupatikana kwa kiwango kizuri cha
ujenzi kitakachokidhi mahitaji yaliyokusidiwa kwa pande zote mbili.
Alieleza
kuwa Wataalamu hao wa ujenzi wameshasafisha eneo la wastani wa Kilo
mita 10 na kufanya kazi za kutengeneza Tabaka la Chini kwa wastani wa
Kilo mita mbili kwa Bara bara ya Cheju –Jendele – Kaebona.
Wizara
ya Miundo Mbinu na Mawasiliano Zanzibar ilitilianasaini Mkataba na
Kampuni ya DP Shapriya + Co Ltd ya Dar es salaam kwa kazi za utekelezaji
wa ujenzi wa Bara bara tatu za Vijijini Unguja mnamo tarehe 11 Septemba
mwaka 2012.
Kukamilika kwa bara bara hizo na
hasa ile ya Cheju-Jendele- Kaebona kwa kiasi kikubwa itawaondoshea
usumbufu wakulima wa zao la mpunga ambao walikuwa wakipata usumbufu kwa
miaka kadhaa sasa
Na
Othman Khamis Ame,
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)