Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dk. Emmanuel Nchimbi katika Kikao na
Wawakilishi wa Nchi za Umoja wa Ulaya waliotembelea Wizarani jana.
Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mbarak
Abdulwakil. (Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi).
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Serikali
ya Tanzania imesema itahakikisha inaendelea kuimarisha hali ya ulinzi
na usalama kwa watanzania na raia wa kigeni waliopo na wanaoendelea
kutembelea hapa nchini kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali
za binafsi na kimaendeleo ili watu wote waweze kutekeleza majukumu yao
na kuishi kwa amani na usalama hapa nchini.
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dk. Emmanuel Nchimbi amesema hayo leo wakati
akizungumza katika kikao baina yake na Ujumbe wa Wawakilishi wa nchi za
Umoja wa Ulaya na mabalozi wa nchi hizo hapa nchini kilichofanyika
katika Ukumbi wa Mikutano wa wizara hiyo.
Mabalozi
hao ni Dk. Ad Koekkoek wa Uholanzi, Marcel Escure wa Ufaransa, Diana
Melrose wa Uingereza, Koenaad Adam wa Belgium na Luis Cuesta wa Spain.
Kikao
hicho kilichowakutanisha Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Dk.
Emmanuel Nchimbi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,
Mbarak Abdulwakil, Mkuu wa Jeshi la Polisi(IGP) Said Mwema , Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Kinondoni Charles Kenyela , Kamanda wa Polisi Kanda
Maalum Dar es Salaam Suleiman Kova na Ujumbe wa Wawakilishi wa Jumuia
ya Ulaya ikiongozwa na Balozi Filberto Cerani Sebregondi kimejadili
hali ya usalama katika Jiji la Dar es Salaam.
Waziri
Nchimbi amesema kwa sasa serikali kupitia Jeshi la Polisi imejiwekea
mikakati mbalimbali ya kukabiliana na vitendo vya uhalifu katika Jiji la
Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla ikiwemo kufanya kila jitihada
kuhakikisha kuwa hali ya ulinzi na usalama inaimarishwa na kwamba
takwimu zinaonyesha kupungua kwa vitendo vya uhalifu.
“
Jeshi la Polisi tayari limeanzisha Dawati Maalumu litakalowahudumia
raia wa kigeni ili kuwawezesha kufungua kesi zao kwa urahisi, kuwepo kwa
wepesi wa majadiliano na ziweze kushughulikiwa kwa haraka na hatimaye
kupatiwa ufumbuzi”. Amefafanua Waziri Nchimbi.
Waziri
Nchimbi amesema pia katika kusimamia suala la Ulinzi na Usalama wa raia
na mali zao kwa sasa wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi itafanya ukaguzi
wa Kampuni Binafsi ya Ulinzi ili kuangalia na kujiridhisha kama
yanakidhi viwango vya ubora vinavyotakiwa.
Kwa
upande wake Kiongozi wa Ujumbe wa Wawakilishi wa nchi za Umoja wa Ulaya
hapa nchini Balozi Filberto Cerani Sebregondi amesema Umoja huo
utaendelea kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambapo pia
ameishukuru Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa jitihada inayoendelea
kuchukua kuhakikisha ulinzi na usalama kwa wageni na raia wa nchini
Tanzania.
Kwa
upande wao Mabalozi waliohudhuria kikao hicho wameitaka Serikali na
Watanzania kuhakikisha usalama unadumishwa ili kutoathiri taswira ya
Tanzania Kimataifa na hivyo kuhatarisha uwezekaji na utalii.
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI,
28 Mei, 2013
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)