Mkuu Msaidizi wa Sekondari ya Nduweni, Venance Mramba
Mkuu wa Sekondari ya Tanya, Victus Kiwango
Na Thehabari.com, Rombo
CHAMA cha Walimu
Tanzania (CWT), Wilaya ya Rombo kimesema shule nyingi za Sekondari za
Kata wilaya hiyo na maeneo mengine nchini zinajiendesha kwa kutegemea
fedha za mifukoni kwa walimu wakuu wanaoziongoza shule hizo.
Kauli hiyo imetolewa jana na Katibu wa CWT Wilaya ya
Rombo, Erasmo Mwingira alipokuwa akifanya mahojiano na mwandishi wa
habari hizi. Hata hivyo uchunguzi uliofanywa na gazeti hili hivi
karibuni kwa kutembelea shule kadhaa za sekondari wilayani hapa umebaini
kuwepo na mazingira magumu ya uendeshaji wa shule hizo kutokana na ugao
wa fedha za uendeshaji shule hizo kutokuwa wa uhakika huku hata kiasi
kinachozifikia hakitoshelezi gharama za uendeshaji.
Akifafanua Mwingira alisema fedha zinazotolewa
kuziendesha shule hizo 'capitation' licha ya kuwa hazitoshi huwa
hazifiki kabisa shuleni hali ambayo huwafanya walimu wakuu kubuni mbinu
mbalimbali za uendeshaji wa shule zao ikiwemo kuweka utitiri wa michango
kwa wazazi ili kuhakikisha mambo yanakwenda shuleni.
"Sasa hivi shule za msingi na sekondari (za
serikali) zinaendeshwa na mifuko ya walimu wakuu...capitation haifiki
kabisa shuleni, fedha inayowafikia ni kidogo sana na haiwezi kuendesha
zile shule, walimu wanatumia mbinu zao kuziendesha shule ndio maana
unaona michango inakuwa mingi shuleni," alisema Mwingira.
Alisema licha ya serikali kusema ada ya sekondari ni
shilingi 20,000 kwa sasa michango katika shule hizo ni mingi kiasi cha
kufikia 120,000 jambo ambalo limewafanya baadhi ya wazazi kuelemewa na
mzigo wa michango na wengine kushindwa kabisa kuimudu.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi
katika shule za Sekondari za Tanya, Nduweni, Urauri, Holili na Ngaleku
na nyinginezo zote za wilayani Rombo umebaini uwepo wa utitiri wa
michango jambo ambalo limelalamikiwa na baadhi ya wazazi na wadau wa
elimu wilayani hapa. Mfano shule ya Sekondari Tanya jumla ya michango
yake imefikia sh. 115,000; mgawanyiko wake ukiwa kama ifuatavyo:- Ada sh
20,000, Madawati sh 15,000, Chakula sh 60,000, Tahadhari sh 5,000,
Ulinzi 5,000, Taaluma sh 5,000 na Kitambulisho sh 5,000.
Aidha uchunguzi zaidi umebaini shule nyingi za
sekondari za kata hazina walimu wa masomo ya sayansi jambo ambalo
huwalazimisha walimu wakuu kutafuta walimu wa kukodi hasa wanafunzi
waliomaliza kidato cha sita kuja kuwafundisha wanafunzi masomo ya
sanyansi kama Hisabati, Fizikia, Kemia, Baiolojia na mengineyo huku
wakitumia mbinu anuai kukusanya michango kuwalipa walimu hao wa kukodi.
"Nashauri Serikali iongeze fungu la uendeshaji wa
fedha shuleni maana fedha za michango zinazotolewa na wazazi hazitoshi
kuendesha shule...huwa tunakodi walimu (wanafunzi waliomaliza kidato cha
sita) kuja kutufundishia masomo ya sayansi kwa muda unakuta gharama
zinakuwa kubwa za uendeshaji shule," alisema Mkuu wa Sekondari ya Tanya,
Victus Kiwango.
"Sisi tumelazimika kuajiri kwa muda wanafunzi sita
waliomaliza kidato cha sita kufundisha masomo ya sayansi kwa fedha za
shule...tunajibanabana kwa michango pamoja na wazazi na kuhakikisha
tunapata chochote kuwalipa walimu hawa wa muda bila hivyo mambo
hayaendi," alisema Mkuu Msaidizi wa Sekondari ya Nduweni, Venance Mramba
akizungumza na mwandishi wa habari hizi.
Kwa upande wake Mwingira alisema vijana wa kidato
cha sita ambao hutumiwa na shule nyingi kuokoa jahazi ya masomo ya
sayansi wamekuwa wakiwakaririsha wanafunzi kujibu mitihani na sio
kuwafundisha jambo ambalo alisema ni hatari kwa elimu ya Tanzania.
"Kujua kusoma na kuandika si kigezo cha kumfundisha mtu...vijana hawa wa
kidato cha sita hawana mbinu za ufundishaji wanachokifanya ni
kuwakaririsha wanafunzi. Pamoja na hayo aliishauri serikali kutojitoa
katika jukumu la kuendesha shule za kata na kuwaachia wazazi kwani shule
hizo ziko katika hali mbaya na zinahitaji kuongezewa fedha za
uendeshaji.
Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa
Wilaya ya Rombo, Judethadeus Mboya alikiri kuwepo na tatizo la upungufu
wa walimu wa sayansi katika shule nyingi za wilaya yake, hivyo walimu
kulazimika kuajiri kwa muda vijana wa kidato cha sita kusaidia wanafunzi
huku jitihada zikiendelea kufanya kukabiliana na tatizo hilo.
"Walimu wa sayansi ni tatizo Rombo hawatoshi...mwaka
huu tumejitahidi na kuajiri takribani walimu 134 wakiwemo wachache wa
masomo ya sayansi lakini tatizo bado lipo," alisema Mboya kikilitolea
ufafanuzi suala hilo ofisini kwake wilayani Rombo hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)