mji wa mtwara waghubikwa na ukimya leo, shughuli zimesimama kwa hofu ya vurugu, polisi waimarisha ulinzi - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

mji wa mtwara waghubikwa na ukimya leo, shughuli zimesimama kwa hofu ya vurugu, polisi waimarisha ulinzi


Soko Kuu, kituo kuu cha mabasi na maduka yamefungwa tangu asubuhi.
Ulinzi umeimarishwa kila kona
Mji wa Mtwara ni sehemu ya pilika pilika ya watu lakini leo hali si hivyo na katika kituo kikuu cha mabasi cha Mtwara hakuna basi lililoingia au kutoka kutwa nzima leo.

Na Abdulaziz Video,
Hali ya usalama ndani ya Manispaa ya Mtwara-Mikindani ni tete. Soko
Kuu, kituo kuu cha mabasi na maduka yamefungwa tangu asubuhi.

Usafiri wa Pikipiki unapatikana katika baadhi ya maeneo machache ya
mji, huku maneo makuu ya biashara yakiwa wazi bila ya pilikapilika za
watu kama ilivyo kawaida.  Polisi wakiwa kwenye magari wameonekana katika maeneo mbalimbali ya mji, na wengine kuweka makambi madogo katika maeneo yanayoaminika kuwa na msongamano wa watu katika siku za kawaida. Mwandishi huyu ameshuhudia magari ya polisi yakiwa na askari katika maeneo ya Bima, Soko kuu ambako pia kulikuwa na gari la kumwaga maji yakuwasha, Magomeni, Skoya na Majengo.

 Hata hivyo hadi kufikia saa 7 mchana hakukuwa na hali yeyote ya
uvunjifu wa amani, makundi ya vijana walionekana wakijadiliana mambo
katika maeneo mengi ya mji.

Hali hiyo imejitokeza kufuatia kusambazwa kwa vipeperushi na ujumbe wa
simu za mkononi na watu wasiojulikana ukiwataka wafanyabishara
kusimamisha shughuli za biashara kwa siku ya (leo) jana ili kutoa
fursa kwa wananchi hao kusikiliza bajeti ya Nishati na Madini
iliyotarajiwa kuwasilishwa leo Bungeni mjini Dodoma. Hata hivyo bajeti
hiyo itawaslishwa Bungeni Mei, 22, mwaka huu. 

 Sehemu ya kipeperushi hicho kilichopambwa na picha ya mtoto
aliyeshikia kombora kinasomeka “Wote kwa pamoja siku ya
tarehe17.05.2013 (Ijumaa saa 3 asubuhi) tusikilize bajeti ya Wizara ya
Nishati na Madini (Bungeni) ili kujua mustakabali mzima wa gesi yetu
na ili kuonyesha kilio, msimamo wetu kwa serikali wa kutaka maendeleo
kwa mikoa ya kusini, siku hiyo huduma zote za jamii zisimamishwe” 
 Licha ya polisi mkoani hapa kuwasihi wananchi kuendelea na shughuli
zao kama kawaida kwa kuwa jeshi hilo litaimarisha ulinzi bado wananchi
wameonesha kutokubaliana na wito huo. 

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa ameliambia amesema kuwa hali ni shwari na kwamba jeshi lake limeimarisha
ulinzi.

 “Hali ni shwari, wapo madereva Bodaboda wanaendelea na kazi zao,
wananchi wanatembea kama kawaida, ispokuwa baada ya maduka yamefungwa” alisema Sinzumwa

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages