Na Benedict Liwenga-Maelezo, Dodoma.
SERIKALI
imetenga shilingi Bilioni 326.0 katika mwaka wa masomo 2012/2013 kwa
ajili ya kuwakopesha wanafunzi 95,902 wakiwemo wanafunzi wa mwaka wa
kwanza, ikilinganishwa na kiasi cha Shilingi Bilioni 56.1 kilichokuwa
kimetengwa mwaka wa masomo 2005/2006 kilichomudu kukopesha wanafunzi
42,729.
Kauli
hiyo imetolewa leo Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Ufundi, Mhe. Philipo Mulugo wakati akijibu swali la Mhe.
Rashid Ali Abdallah Mbunge Jimbo la Tumbe alilotaka kujua kwanini
Serikali imeshindwa kuwapatia mikopo baadhi ya Wanafunzi wenye sifa za
kuendelea na masomo na Serikali ina mpango gani wa makusudi kuhakikisha
kuwa Wanafunzi hao wanapata elimu.
Alisema
kuwa ongezeko hilo la fedha ni ishara tosha kuwa Serikali ina nia ya
kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wenye sifa za kusoma Vyuo vya Elimu ya
Juu wanapata mikopo itakayowawezesha kupata elimu yao katika mazingira
mazuri.
“Serikali
ina nia njema ya kuhakikisha kuwa kila Mtanzania mwenye uwezo wa kusoma
Chuo cha Elimu ya Juu anapata fursa hiyo”. Naibu Waziri Mulugo alisema. Aliongeza
kuwa kwa mwaka wa masomo 2012/2013, wanafunzi wa mwaka wa kwanza
waliowasilisha maombi ya kupata mkopo walikuwa 37,315, baada ya
uchambuzi kufanyika wanafunzi waliobainika kuwa na sifa ya kukopeshwa
walikuwa 34,140 lakini kati ya hao ni wanafunzi 30,319 sawa na asilimia
88.9 walipata mikopo.
“Kwa
mantiki hii wanafunzi waliokosa mikopo ni 3,821 sawa na asilimia 11.1 ya
wanafunzi wote walioomba mkopo, wanafunzi hawa wachache walikosa mikopo
hiyo kutokana na ukomo wa kibajeti pamoja na vipaumbele vilivyowekwa na
Serikali”. Mhe. Mulugo alisema.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)