Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph
Warioba akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo (Jumatatu,
Aprili 29, 2013). Kulia ni Katibu wa Tume, Bw. Assaa Rashid.
Mwenyekiti wa kamati ya uwasilishaji wa mapendekezo ya
muundo wa mabaraza ya Katiba kwa jamii ya watu wenye ulemavu, Bw. David Nyendo
(kushoto) akiwasilisha maoni yake ya kamati hiyo kwa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba katika mkutano baina yao uliofanyika
ofisi za Tume Jijini Dar es Salaam tarehe 13 Feb mwaka huu (2013). Kulia
ni Mjumbe wa Tume, Dkt. Salim Ahmed Salim. Picha na Tume ya
Katiba
Na Mwandishi Wetu
Tume ya Mabadiliko ya Katiba imesema imejipanga
kuandaa rasimu ya katiba itakayoweka mbele maslahi ya taifa na kuwaomba
wananchi waijadili na kutoa maoni yao katika mabaraza ya katiba yatakayokutana
kuanzia mwezi Juni mwaka huu (2013).
Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Jospeh Warioba amesema
leo (Jumatatu, Aprili 29, 2013) jijini Dar es Salaam kuwa katika kuandaa rasimu
hiyo, Tume yake haitapokea shinikizo kutoka taasisi, asasi, makundi au vyama
vya siasa.
“Tume haitengenezi katiba ya vikundi au vyama,
tunaandaa katiba ya nchi,” amesema Jaji Warioba katika mkutano wake na
waandishi wa habari katika ofisi za Tume na kufafanua kuwa Tume inazingatia
uzito wa hoja zilizotolewa na wananchi
na sio idadi ya watu waliotoa maoni.
Jaji Warioba amewataka wananchi kutokubali kutumiwa
na makundi, asasi, taasisi na vyama wakati wa kujadili na kutoa maoni katika
mabaraza ya katiba ya wilaya.
MABARA YA WANANCHI WENYE ULEMAVU
Akizungumza kuhusu ushiriki wa walemavu katika
mabaraza ya katiba, Jaji Warioba amesema Tume yake inatarajia kuunda mabaraza
ya Katiba ya watu wenye ulemavu ili kuwapa fursa walemavu kutoka Tanzania Bara
na Zanzibar kutoa maoni yao kuhusu rasimu ya Katiba itakayotolewa na Tume.
Hatua hii inafuatia ombi la Shirikisho la Vyama vya
Watu wenye ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) na Umoja wa Watu wenye ulemavu
Zanzibar (UWAZA) waliloliwasilisha kwa Tume.
Jaji Warioba amesema Baraza moja litaundwa Tanzania
Bara na jingine Zanzibar na kwamba yatashirikisha wananchi kutoka ngazi ya
chini ya wilaya hadi Taifa.
“Tunaelewa kuwa watu wenye ulemavu ni karibu
asilimia 10 ya watanzania wote na mchakato huu hauwezi kuwatenga katika ngazi
yoyote,” amesema Jaji Warioba na kuongeza kuwa taarifa ambazo Tume yake inazo
zinaonyesha baadhi ya watu wenye ulemavu wamependekezwa na mitaa, vijiji,
vitongoji na shehia kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya.
CHAGUZI ZA WAJUMBE MABARAZA YA KATIBA YA WILAYA.
Aidha, Jaji Warioba amezungumzia mafanikio na
changamoto zilizojitokeza katika chaguzi zilizofanyika nchini kote hivi
karibuni za kuchagua Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba kuanzia ngazi ya mitaa,
vijiji, vitongoji na shehia.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, tathmini ya Tume
inaonyesha kuwa kwa kiwango kikubwa viongozi na watendaji katika ngazi za
vijiji, mitaa, shehia na kata walizingatia mwongozo uliotolewa na Tume na kuwa
maeneo mengi wananchi walichaguana kwa amani na utulivu.
“Kwa mfano jumla ya shehia 323 sawa na asilimia
96.4 kati ya shehia 335 kwa upande wa Zanzibar zimekamilisha vizuri mchakato
huu, hali kadhalika jumla ya Kata 3,331 sawa na asilimia 99.8 kati ya Kata 3,339
kwa Tanzania Bara nazo zimekamilisha mchakato wa kuwapata wajumbe wa Mabaraza
ya Katiba ya Wilaya kwa kuzingatia utaratibu uliotolewa kwa mujibu wa Mwongozo,”
amesema Jaji Warioba.
Kuhusu hatua inayofuata baada ya chaguzi hizo, Jaji
Warioba alisema Tume inaendela kupokea majina kutoka kwa Mamlaka za Serikali za
Mitaa na ya wananchi wote waliopendekezwa kutoka katika Kata na Shehia na kazi
hiyo inatarajia kukamilika ifikapo tarehe 30 Aprili mwaka huu (2013).
Changamoto Akizungumzia kuhusu changamoto zilizojitokeza
katika chaguzi hizo, Jaji Warioba amesema kuwa pamoja na mafanikio
yaliyopatikana pia kulijitokeza changamoto kadhaa ambazo zilisabishwa na
misimamo ya kisiasa na kidini
“Katika baadhi ya maeneo mikutano ya uchaguzi ngazi
za vijiji, mitaa na shehia ilishindwa kufanyika kutokana na mivutano ya kisiasa
na kidini zilizosababishwa na baadhi ya wananchi kufangamanisha chaguzi za
Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya na masuala ya kisiasa na kidini,”
amesema Jaji Warioba.
Jaji Warioba ametaja changamoto nyingine kuwa ni
pamoja na baadhi ya wananchi kujiingiza katika vitendo vya rushwa katika
chaguzi hizo ili wapendekezwe kuwa wajumbe wa mabaraza hayo ya katiba.
“Tumepokea pia malalamiko ya vitendo vya rushwa,”
alisema Mwenyekiti huyo na kusema vitendo hivyo ni kinyume cha sheria na
kuongeza kuwa taasisi zenye mamlaka ya kupambana na vitendo hivyo zinapaswa
kushughulikia malalamiko hayo.
AINA NA MAJUKUMU YA MABARAZA YA KATIBA:-
Katika mkutano huo uliofanyika katika katika Ofisi
za Tume zilizopo mtaa wa Ohio jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti huyo pia
alizungumza kuhusu aina na majukumu ya Mabaraza ya Katiba.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba, Sura ya 83 imetoa fursa ya kuundwa kwa mabaraza ya aina mbili ambayo ni
Mabaraza yatakayoundwa, kusimamiwa na kuendeshwa na Tume katika muda na tarehe
itakayopangwa na Tume.
Aina ya pili, kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, ni
Mabaraza ya Katiba ya Asasi, Taasisi na Makundi mbalimbali yenye malengo
yanayofanana. Mabaraza haya yatajiunda, yatajisimamia na kujiendesha yenyewe na
kisha kuwasilisha maoni yao kuhusu rasimu ya Katiba ndani ya muda utakaopangwa
na Tume.
“Kazi kubwa ya Mabaraza ya Katiba ya aina zote
mbili ni kuipitia, kuijadili na kuitolea maoni rasimu ya Katiba itakayokuwa
imeandaliwa na Tume kutokana na maoni yaliyokusanywa kutoka kwa wananchi,”
alisema Jaji Warioba na kuziomba taasisi, makundi, asasi na vyama mbalimbali
kutumia fursa hiyo ya kisheria kuunda mabaraza na kutoa maoni yao kuhusu rasimu
ya Katiba itakayotolewa.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)