Mabinti wakiwa wamevaa Vimini
Imeandikwa na Basil Msongo - Mwananchi Communication
KUPUNGUA sanjari na kukiukwa kwa maadili katika jamii nchini na
kwingineko si jambo geni, yanayofanywa na watu wa rika tofauti yanaweza
kukuudhi, kukukera, au kukustaajabisha lakini naamini kwa wengi
yamezoeleka na huenda sasa yanatafsiriwa kuwa ni mambo ya kawaida na ni
sehemu ya maisha ya kila siku.
Januari 24 mwaka huu simshangai Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Rehema
Nchimbi anapowataka wazee wasimamie maadili kwa vijana, kwa kuwa
wanapotoka. Ingawa hakuusema upotovu huo kwa undani huo ndiyo ukweli,
baadhi ya matendo ya kundi hilo yanatia kinyaa.
Dk Nchimbi anatoa mfano kuwa, vijana wengi wakiwemo wasomi waliopo
vyuoni Dodoma wanapenda starehe hali inayotia mashaka hata maendeleo
yao, na kwamba, wateja wakubwa wa sehemu za starehe ni wanafunzi wa vyuo
vikuu.
Huhitaji elimu ya chuo kikuu au kufanya utafiti kuthibitisha
anayosema kiongozi huyu wa Serikali, ukiwa Dodoma mjini nenda kwenye
kumbi kubwa za starehe usiku, mfano Club 84, Club Maisha, Club La Aziz
na kwingineko, utakutana na wanafunzi wengi wa vyuo vilivyopo mkoani
humo kikiwemo Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Chuo Cha Mipango, Chuo Kikuu
Cha Mtakatifu John, Chuo Cha Elimu ya Biashara (CBE) na kuna tetesi
kuwa baadhi yao wanajiuza!
“Hivi hizi ni starehe gani zinazoharibu watoto wetu, na Mamlaka ya
Mapato wamekuwa wakikusanya kodi kwenye klabu za usiku, ambazo
zinaendelea kuharibu akili za wanafunzi na huko klabu wanapokwenda
ukiona walivyovaa, utatamani ardhi ipasuke uingie, halafu tunalalamika
mvua hazinyeshi,” anasema Dk Nchimbi.
Machi 7 mwaka huu, Dk Nchimbi anarudia kutoa kauli inayofanana na
hiyo kwa kuwataka wazazi na walezi wenye watoto wanaosoma katika vyuo
vikuu wawe makini kufuatilia mienendo ya watoto wao kwa kuwa wengi
wamekuwa wakiendekeza starehe kwa kukesha kwenye klabu za usiku na
wanapofanya vibaya katika masomo lawama zinaelekezwa kwenye vyuo husika.
Anasema, kila mzazi au mlezi anatakiwa kusimama katika nafasi yake ya
kusimamia maadili ya watoto ambao wamekuwa wakipotoka huku wengine
wakiwa na mavazi yasiyo na heshima na anahoji inakuwaje mama anaweka
mikono kichwani na kusema mtoto wake amemshinda.
“Dodoma kuna vyuo vikuu vingi lakini nini maadili ya wanafunzi katika
vyuo hivyo, kwani wengine hawazingatii kilichowapeleka chuoni, wamekuwa
wakivaa mavazi yasiyo na heshima na hata kutumia vilevi na wamekuwa
hawafanyi vizuri katika masomo yao,” anasema Nchimbi wakati wa kongamano
kuhusu sera ya kuondoa umasikini na jinsia iliyofanyika katika ukumbi
wa Mwalimu Nyerere, Chuo cha Mipango Mjini Dodoma.
Maadili hayakiukwi mitaani tu, Askofu Mkuu wa Kanisa la Tanzania
Assemblies of God (TAG), Barnabas Mtokambali, anakemea vitendo vya
baadhi ya wanaume wanaovaa suruali chini ya makalio, huko mitaani uvaaji
huo ni maarufu kwa jina la ‘kata K’.
Askofu huyo anasema, wanaovaa hivyo ni sawa na mashoga kwa kuwa,
mwanamume kuvaa suruali chini ya makalio ni sawa na kujitangazia
biashara ya ushoga ya kufanya mapenzi ya jinsia moja na kwamba, wanavaa
hivyo kujitambulisha.
Mtokambali anatoa kauli hiyo hivi karibuni wakati akizindua Chuo cha
Ualimu cha Mount Sinai kilichopo Bunju, nje kidogo ya Jiji la Dar es
Salaam na kusisitiza kwamba, machangudoa wanavaa nusu uchi kuonesha kuwa
wapo katika biashara, mashoga nao wanavaa ili kujitambulisha.
Tatizo halipo TAG tu, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania
(KKKT), Dayosisi ya Morogoro linasema, halitawafungisha ndoa watarajiwa
watakaoingia kwenye ibada wakiwa wamevalia mavazi yanayodhalilisha hasa
kwa wanawake wanaoacha matiti nje na migongo wazi.
Makamu wa Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT)
Dayosisi ya Morogoro, Mchungaji George Pindua, anatoa agizo hilo kwa
niaba ya uongozi wa Kanisa kabla ya Askofu Jacob Paulo ole Mameo
kumkaribisha Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa kuendesha harambee ya
kuchangisha fedha zitakazowezesha uendelezaji wa Jengo la Kanisa la
Usharika wa Kilakaka uliopo chini ya kanisa hilo mjini Morogoro.
“Kanisa limeshindwa kuvumilia tabia iliyojengeka ya kuona mavazi
yanayovaliwa hasa kwa wanawake ya kuacha matiti yakionekana ...hili sasa
ni agizo kwenye ibada hasa ya ndoa, wanaovaa mavazi hayo , wachungaji
msiruhusu ndoa hiyo ifungwe’’ anasema Mchungaji Pindua. “Wazee wa Kanisa
sasa muwe na vitenge maalumu vya kuwafunika hawa mabibi harusi wenye
kuvaa magauni yanayoacha sehemu ya matiti wazi...hili haturuhusu
kuendelea kufanyika’’ anasema.
“Tunawaheshimu mama zetu, mmetulea , lakini kwa hili la kuacha sehemu
ya maziwa kuonekana wazi hatutalikubali kuanzia sasa , yafuateni haya
maagizo , msiwakwaze wachungaji ‘’ anasema na kutaja nguo nyingine
zisizokubalika kanisani kuwa ni zile za kulalia ambazo ni suruali
zinazobana na kuonesha mapaja.“Ni budi sisi waumini tuheshimu maadili ya
kumcha Mungu na moja ni uvaaji wa mavazi ya heshima mbele ya Mungu
...zile suruali zinazoonesha maumbile yote ya ndani zisitumike kuingia
kwenye ibada ‘’ anaonya Makamu wa Askofu.
Ili kudhibiti tabia mbaya ya uvaaji usiofaa kwa baadhi ya waumini,
miezi kadhaa iliyopita Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam
lilitangaza kuwa limeandaa mpango wa kukomesha uvaaji mbovu unaokwenda
kinyume na maadili ikiwemo kuvaa vimini, nguo za kunyanyua matiti na
milegezo kanisani.
Kanisa hilo linasema, wanawake watakaovaa onyo kanisani watavishwa
kaniki na kulikuwa na taarifa kwamba, matangazo ya kukemea uvaaji mbaya
yalikuwa yakitolewa mara kwa mara katika parokia mbalimbali za Jimbo
hilo linalongozwa na Mwadhama Kadinali Policarp Pengo.
“Ni kama mwezi mmoja sasa umepita, Jumapili moja tukiwa kanisani,
Paroko alitangaza kukemea uvaaji mbaya na kiongozi mmoja naye akatangaza
kuwa Kanisa linaandaa vazi la kaniki ili watakaovaa vimini, milegezo na
kuachia matiti kanisani, watavikwa kaniki na wakirudisha watalipia Sh
500 kama fidia,” anakaririwa mmoja wa waumini katika Parokia ya Msewe.
“Kuna baadhi walikuwa wanakuja wamevaa nguo zinaitwa za kupiga jeki
matiti, sasa akienda kupokea Ekaristi (Mwili wa Yesu), padri anakutana
na matiti kwanza, tukumbuke hao mapadri nao ni binadamu jamani,” anasema
Mwenyekiti Msaidizi wa Baraza la Walei, Parokia ya Msewe, Benedict
Fungo.
“Sasa ukiwapelekea matiti njenje si unawatamanisha na hii ni dhambi,
pia walikuwa wanavaa nguo fupi sana (vimini) na milegezo, mtu akiinama
anaacha nguo yote ya ndani nje, haya si maadili yetu, lazima mtoto wako
ukiona anakwenda vibaya umkanye, usipofanya hivyo wewe si mzazi mwema”.
Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Method Kilaini
anapendekeza kuwa mpango wa kuwavisha kaniki na vitenge watu wanaokwenda
kanisani na milegezo, vimini na nguo za kuacha mabega na matiti wazi
uungwe mkono na Parokia na makanisa yote.
“Kweli hiyo ni hatua ya kuungwa mkono, mimi naomba Parokia zote na
makanisa hasa ya Dar es Salaam yaige, unajua hakuna haja ya kugombana na
watu, mtu akija amevaa ovyo, avikwe kitenge au kaniki na akirejesha
alipe si tu shilingi 500, bali hata zaidi ya hapo,” anasema Askofu
Kilaini na anaomba vyama vya kitume kikiwemo cha Wanawake Wakatoliki
Tanzania (WAWATA), kuandaa vitenge vya kuwavisha watu wa namna hiyo.
“Kuvaa vibaya katika nyumba za ibada ni laana, hasa vijana wanavaa
milegezo utadhani suruali inaanguka, si tabia njema hii lazima ikemewe
kwa mafundisho, lakini pia kwa kuchukua hatua ya kuwasitiri kama hiyo,
turejeshe heshima sehemu hizi takatifu,” anasisitiza Kilaini.
Baadhi ya wachungaji wa makanisa ya kiroho, wanapinga mpango wa
Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaa wa kuwavalisha kaniki wanaovaa
ovyo kanisani kwa maelezo kwamba, hata Yesu alikuja kwa ajili ya
waliopotea. Wanasema, hakuna haja ya kuweka sheria za namna hiyo
kanisani, yatolewe mafundisho ya neno la Mungu yatolewe kwa kina ili mtu
abadilike bila shuruti.
“Yesu alikuja kwa ajili ya waliopotea, kanisani ni mahali pa kimbilio
kwa wakosefu, ukiweka sheria za namna hiyo zitawakimbiza wengi, mwache
mtu aje alivyo na akifika na kuona wengine wanavyovaa na kupata
mafundisho ya neno la Mungu, atabadilika,” anasema Mchungaji Emmaus
Mwamakula.
Mchungaji Mwamakula ambaye ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Kujisomea
Biblia hakubaliani na utaratibu huo kwa kuwa kanisani ni sehemu ya
kimbilio na wengine wanaovaa ovyo wamekataliwa katika jamii zao, hivyo
wanahitaji kusaidiwa na si kuwekewa sheria. Tatizo la ‘kuvaa vibaya ’
halipo Tanzania tu, Baraza la Makanisha nchini Malawi (MCC),
limependekeza kuwa Serikali ya nchi hiyo itangaze aina ya mavazi
wanayotakiwa kuvaa wananchi nchini humo ili kuheshimu utamaduni wa
asili.
Novemba mwaka jana, makanisa hayo yalitoa tamko la pamoja kuhusu
mambo yanayoiathiri nchi hiyo na kusema kuwa, limebaini kuwa, watu
wanavaa kinyume cha utamaduni wa asili wa nchi hiyo, na kinyume cha
maadili ya kiroho wakiwemo wanaotembea karibu uchi kabisa, wanawake
wanaoacha matiti nje na wanaume wanaovaa kata K.
Katika tamko hilo lililotolewa baada ya mkutano wa mwaka wa baraza
hilo, MMC linasema, limeona pia wanaume wanavaa vitu vya wanawake
zikiwemo hereni, wanasuka nywele sambamba na kuvaa nguo za kike. ‘Msingi
wa uhuru na haki za msingi vimetoka kwa Mungu, kwenye bustani ya Eden
pale Adam na Eva walipoambiwa kipi wale na kipi wasile.
Uhuru na haki visikandamize wajibu” linasema tamko la MCC na kuiomba
Serikali ya Malawi itangaze dress code ili Wamalawi wavae inavyostahili.
Baada ya makanisa kutoa tamko hilo, Mamalawi wengi wanatoa maoni yao
kwenye mtandao, wanapinga msimamo huo kwa kusema, Malawi si nchi ya
kikristo kanisa lifahamu nafasi yake kwenye jamii.
Wanasema, kanisa halina haki ya kuamua wananchi wavae au wasivae
nini, na kwamba, sheria za nchi hiyo hazikutolewa kwenye biblia.
Wanaopinga mtazamo wa makanisa kuhusu mavazi wanasema, Serikali ya
Malawi ikikubali mtazamo wa makanisa huo utakuwa udikteta, kila mtu ana
haki ya kufanya anachotaka ili mradi asiingilie haki ya watu wengine.
Wanasema, kama makanisa yanataka kuwa na sheria ya mavazi walieleze
jambo hilo makanisani kwa waumini wao na si katika jamii yote kwa kuwa
Malawi haiongozwi na sheria za kidini. Wanadai kuwa, viongozi wa
makanisa hayo wana imani haba, na watapoteza waumini kwa kuwa,
hawakupaswa kuleta sheria ya mavazi au kuwatisha waumini.
Wanahoji, kutokuwepo kwa vishawishi au uwezo wa kuvishinda
vinakufanya uwe Mkristo bora? Na tangu lini aina ya mavazi ikawa dhambi?
Wanasema, huwezi kumlazimisha mtu avae nini au asivae nini, na kama
zilivyo haki za binadamu, kuvaa ni haki ya msingi ya mtu, na yeye ndiye
anaiyechagua avae nini au asivae nini hivyo Wamalawi hawataki kuelezwa
hilo na wanasiasa na viongozi wa kanisa wenye umri wa zaidi ya miaka 70.
Wanasema wao watavaa kadri wanavyojisikia, kama hao viongozi
wanafanya kazi ya Mungu, wawahubirie mashoga, wasagaji na wanaorekodi
video za ngono waache dhambi hizo, na kwamba hilo ni jukumu lao na si la
Serikali, wasipoyaweza hayo wakiri kwamba wameshindwa.
Wamalawi hao wanasema, Yesu alikuja wakati kukiwa na dhambi sana
duniani, hakulalamika kwa Serikali ya Kirumi kutunga sheria kali na
badala yake alifundisha kuhusu upendo wa Mungu na Baraka anazopata mtu
anapotii neno lake na matokeo yake wengi walimfuata na wakatubu.
Wanasema kanisa halina mamlaka ya kuamua wao wavae vipi, dunia
inabadilika, zamani watu walitembea uchi kwa kwa sababu ya maisha ya
wakati huo, lakini sasa dunia imestaarabika, watu wataendelea kutembea
uchi kwa sababu ya fasheni.
Wakati baadhi ya Wamalawi wakiwa na mtazamo huo, Baraza hilo lenye
makanisa 24 wanachama nchini humo na taasisi washirika 12 za kikanisa
pia linapinga taarifa zinazodai kuwa, takribani makahaba 20,000
wameungana kupinga unyanyasaji, waboreshewe huduma za tiba, na wameunda
umoja wao.
Ukahaba hauruhusiwi Malawi, na inadaiwa kuwa makahaba wao wanaungwa
mkono na mashirika ya kimataifa yasiyo ya kiserikali. Makanisa yanalaani
kuruhusu dhambi hiyo kibiblia, na kwamba, Katiba ya nchi hiyo pia
hairuhusu, na kiutamaduni haikubaliki.
“Kwa Mungu ukahaba ni dhambi na Sheria za Malawi zinakataza kwa hiyo
Baraza la Makanisa Malawi linaisihi Serikali izingatie sheria za nchi
zinazoharamisha ukahaba,” inasema taarifa ya baraza hilo. Baraza
linasema, Biblia inakataza zinaa, nalo linasisitiza kutekelezwa kwa amri
hiyo ya Mungu na linaamini kwamba, si sahihi kuunga mkono ukahaba na
hata demokrasia haiutambui.
MCC inapinga kinachodaiwa kuwa ni mpango wa Serikali ya Malawi kufuta
sheria ushoga, na lisema, licha kuhitaji wafadhili, Malawi ni nchi
yenye hofu ya Mungu, hivyo iendelee kutambua kuwa mapenzi ya jinsi moja
hayawi sehemu ya mambo yanayokubalika katika jamii ya Wamalawi.
Baraza linasisitiza msimamo wake kupinga vitendo vya ushoga kwa kuwa
kibiblia ni dhambi, kimaadili havikubaliki na ni kinyume cha asili ya
uumbaji wa Mungu na kwamba, haki yoyote inayopingana na mamlaka ya Mungu
itasababisha vifo vya Wamalawi. Wanawake kuacha matiti au migongo nje
kanisani, kuvaa vimini, na wanaume kuvaa kata K kanisani si ustaarabu
kwa sababu, kanisani ni nyumba ya ibada, inahitaji staha, na kujiheshimu
kwa kuwa mwili ni hekalu la Mungu.
Hata kama ni suala la fasheni, wanaovaa nusu uchi kanisani wanapaswa
kutumia hekima, wajiheshimu na watambue kwamba, si vazi lolote unaweza
kulivaa wakati wowote na mahali popote, wavae kwa kuzingatia wanakwenda
wapi kwa kuwa kanisani si sehemu ya kuvaa kikahaba, waache ulimbukeni. Chanzo Mwananchi Mtandaoni






No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)