Utafiti wa Tamwa wamrudisha mwanafunzi shuleni - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Utafiti wa Tamwa wamrudisha mwanafunzi shuleni

 Bibi wa mwanafunzi Mwenjuma Magalu, Amina Mohamed (kulia) akizungumza na Mhariri wa mtandao wa Thehabari, Joachim Mushi kijijini Msasa, wilayani Handeni juzi.
 Mwenjuma Magalu (wa kwanza kulia mstari wa pili) ambaye kwa sasa ni mwanafunzi wa kidato cha pili Shule ya Sekondari Komnyang’anyo akiwa darasani na baadhi ya wanafunzi wenzake

Na Thehabari.com, Handeni

UTAFITI wa kihabari uliofanywa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Machi 2012 umefanikisha kumrudisha shuleni mwanafunzi wa sekondari aliyekuwa ametelekezwa yeye pamoja na familia yao.

Mwenjuma Magalu ambaye kwa sasa ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Komnyang’anyo alitelekezwa na babayake yeye pamoja na mamayake mwaka jana, hivyo kushindwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule hiyo licha ya kuchanguliwa kuendelea na masomo.
Hata hivyo baada ya utafiti wa kihabari kufanyika kijijini Msasa Wilaya ya Handeni na taarifa za mtoto huyo kushindwa kujiunga na sekondari baada ya mamayake (kwa sasa marehemu) kukosa uwezo kuripotiwa, alijitokeza mfadhili wa kumsomesha ambaye anagharamia masomo yake hadi sasa.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi juzi akiwa shuleni. Komnyang’anyo, mwanafunzi huyo aliishukuru TAMWA kwa kuibua tatizo la familia yao kwa umma na kupatikana kwa mfadhili ambaye amemrudisha masomoni licha ya familia yao kutelekezwa.

“Binafsi nawashukuru sana hao (TAMWA) waliopaza sauti hadi mjuu wangu kurudi shuleni…hii kwetu ilikuwa ni ndoto kwetu maana mtoto mwenyewe alikuwa amekata tamaa kabisa kurudi shuleni na alikuwa kaanza kufanya vibarua mitaani huku wenzake wakiendelea na shule,” alisema bibi wa mtoto huyo, Amina Mohamed akizungumza.

Bibi huyo akizungumzia maisha ya sasa ya familia hiyo alisema bado wanahitaji msaada wa huduma hasa baada ya mwanaye kufariki dunia mwaka jana na kumuachia watoto wake. 

Aliongeza kwa sasa yeye ni mgonjwa wa TB anayetumia dawa hivyo kwa hali yake ameshauriwa kupumzika jambo ambalo limempa mzigo mkubwa kimajukumu mwanafunzi (Mwenjuma), kufanya kazi za nymbani kama kupika kulima na shughuli nyingine.

Hata hivyo mama wa mtoto huyo (Hadija Magalu) ambaye alitelekezwa na mzazi mwenzake alifariki dunia mwaka jana kwa tatizo la uzazi na kuiacha tena familia hiyo ya watoto watatu katika hali ngumu zaidi chini ya malezi ya bibi mzaa mama.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages