SWAHILI FASHION WEEK KUFANYA
ONYESHO LA MITINDO ZANZIBAR
WABUNIFU ZAIDI YA KUMI
KUONYESHA UBUNIFU WAO KATIKA JUKWAA MOJA
KUFANYIKA IJUMAA YA TAREHE
15/O2/2013, MBWENI RUINS
Onyesho kubwa la mavazi Afrika
Mashariki na kati la Swahili Fashion Week, limepanga kufanya onyesho kubwa
visiwani Zanzibar katika Hoteli ya Mbweni Ruins siku ya Ijumaa ya tarehe
15/02/2013 ambapo wabunifu nguli kutoka Tanzania bara na Visiwani wamethibitisha
kwa shauku na hamu kubwa ya kuacha kumbukumbu nzuri ndani ya usiku huo wa onyesho la
mitindo katika visiwa hivyo vya marashi ya karafuu.
Tukio hili la Swahili Fashion Week
Zanzibar litawaleta kwa pamoja zaidi ya wabunifu kumi kutoka ndani ya nchi
kuonyesha ubunifu na umahiri wao katika tasnia ya sanaa ya ubunifu na kuongeza
kasi ya maendeleo ya tasnia ya mitindo nchini Tanzania huku ikitangaza dhana
nzima ya kujali vitu vinavyotengenezwa Afrika (Promote Made in Africa
Concept)
“Maandalizi yameshika kasi, tuko
tayari kupeleka ladha ya Swahili Fashion Week katika visiwa vya Zanzibar, Kama
inavyofahamika kwamba watu wengi watakuwa visiwani humo kufuatilia Sauti za
Busara, huu ni mwezi wa burudani na vitu vizuri kwa watu wote Zanzibar, timu ya
Swahili Fashion Week inafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kwamba inatibu
kiu ya wapenzi wote wa Swahili Fashion Week na wadau wa maswala ya Ubunifu na
Mitindo Zanzibar” Alisema Mustafa Hassanali muanzilishi na muandaaji wa Swahili
Fashion Week.
“Kupeleka Swahili Fashion Week kwa
mashabiki waliopo visiwani Zanzibar, ni kuendeleza utamaduni wetu wa kuwa tukio
bora la burudani na biashara katika tasnia ya mitindo, tukio hili la Zanzibar
litawashirikisha wabunifu nguli toka bara na visiwani kuonyesha ubunifu na ladha
tofauti za kiutamaduni, na wapenzi wa ubunifu na mitindo kupata ladha kutoka kwa
wabunifu wa ndani ikiwa ni kama sehemu ya kuongeza familia yetu ya mitindo na
ushirikiano baina ya wabunifu wa bara na visiwani” Aliongezea
Hassanali
Baadhi ya wabunifu watakaoshiriki ni
Asia Idarous (Mshindi wa tuzo ya Humanitarian katika tuzo za SFW 2012), Dominick
Godfrey, Subira Wahure, Ailinda Sawe, (Mshindi wa tuzo ya Origin Africa, SFW
2012), Martin Kadinda (Mbunifu Bora wa Nguo za Kiume, SFW 2012), Sarah Masenga
(Mbunifu Bora Chipukizi, SFW 2011), Gabriel Mollel (Mbunifu Bora wa Mwaka na
Mbunifu Mvumbuzi wa mwaka, SFW 2012), Subira Wahure, Jamila Vera Swai, Salim
Ali, Ahmed Abdul pamoja na mshindi wa tuzo ya Mbunifu Anaechipukia wa SFW 2012,
Lucky Creation.
“Swahili Fashion Week Zanzibar ni
onyesho rasmi na la kwanza kufanyika visiwani humo, Swahili Fashion Week
ilishafanya onyesho la mitindo mkoani Arusha mwaka 2011 na mipango ni kufanya
maonyesho mbalimbali katika miji mikubwa hapa Tanzania” Alimalizia Meneja
Uhusiano wa Swahili Fashion Week, Hassan Mrope.
Onyesho limepangwa kuanza mapema
ambapo kuanzia saa moja usiku milango itakuwa wazi. Tiketi za onyesho hili
zinapatikana katika Hoteli ya Mbweni Ruins na Hotspot
Bistro.
Onyesho hili la Swahili Fashion Week
Visiwani Zanzibar limedhaminiwa na Mbweni Ruins, ZG Tours, Daja Salon & Spa,
Vayle Springs Clouds TV, Coconut Fm na 361 Degrees.
Swahili Fashion Week
mpaka sasa ndio ni tukio kubwa la mitindo Afrika ya Mashariki na Kati. Ni mwaka
wa sita sasa, Swahili Fashion Week ni jukwaa la wabunifu wa mitindo na vito vya
urembo kutoka nchini zinazoongea Kiswahili na Bara la Afrika kwa ujumla
kuonyesha vipaji vyao, kutangaza ubunifu wao na kutengeneza mtandao na wadau
duniani. Dhamira kubwa ni kuweka mkazo katika ukanda huu kwamba ubunifu ni
tasnia inayotengeza vyanzo vya mapato huku ikitangaza bidhaa zinazotengenezwa
Afrika “Promoting Made in Africa concept”.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)