Na Beatrice Shayo
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania, Dk Paul Mushi. Kufuatia sakata kuwa Serikali haina mitaala rasmi ya
kufundishia shuleni, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania, Dk
Paul Mushi (pichani), amejiuzulu wadhifa huo. Nafasi yake imechukuliwa na Mkurugenzi wa Idara ya kubuni na kuendeleza Vifaa vya Elimu, Dk. Leonard Akwilapo.
Akihojiwa na NIPASHE kwa njia ya simu jana jijini Dar es Salaam,
Dk. Mushi alithibitisha kujiuzulu na kusema alichukua hatua hiyo kwa
hiari yake bila kushinikizwa na mtu.
"Hakuna aliyenishinikiza nimeamua mwenyewe kuandika barua ya kujiuzulu," alisema Dk. Mushi
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Dk. Akwilapo alipohojiwa juu ya
mtangulizi wake aliyeachia ngazi , Alhamisi wiki hii, alisema
aliondoka kwa maamuzi yake mwenyewe bila shinikizo kama alivyoeleza.
"Sio siri ni kweli amejiuzulu na aliniambia ni maamuzi yake
aliyoyafanya ya kujivua madaraka ya Mkurugenzi Mkuu bila ya kugombana na
mtu na juzi ndio alipewa barua yake na mimi kupatiwa barua ya kuwa
kaimu," alisema Dk Akwilapo
Katika mkutano wa Bunge la mwezi huu, Mbunge wa kuteuliwa na Rais
James Mbatia (NCCR-Mageuzi), aliwasilisha bungeni hoja binafsi kuhusu
udhaifu uliopo katika sekta ya elimu hapa nchini.
Katika hoja hiyo, aliibua sakata la kutokuwapo kwa mitaala
inayoongoza ufundishaji wa masomo shuleni hali inayosababisha kudorora
kwa elimu.
Kadhalika aliibua tuhuma za uchapishwaji wa vitabu ambavyo maudhui
yake hayana viwango pia waliopewa kazi ya kuchapisha ndiyo hao
waliokuwa wahariri na waandishi .
Pia alihoji sababu za uchapishaji wa vitabu hivyo kufanyika nje
ya Tanzania hali ambayo inasababisha kuwapo kwa matumizi mabaya ya
fedha .
Katika kujibu hoja hizo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi
alilithibitishia Bunge kuwa serikali ina mitaala na nakala zake
ziliwasilishwa bungeni na hoja hiyo ikazimwa.
Baada ya kuwasilishwa kwa mitaala hiyo, bunge iliunda kamati ya
kujiridhisha kama ni kweli mitaala hiyo ni sahihi ambapo ilikuja na
majibu ya kujiridhisha kuwa ni ya kweli.
Hata hivyo, kwa upande wa James Mbatia alisema bado kuna utata
katika mitaala hiyo licha ya kamati hiyo kujiridhisha kuwa mitaala ipo
sahihi.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)