Angetile Osiah, Katibu wa Kamati ya Uchaguzi. |
Kamati ya
Uchaguzi ya TFF kwa kuzingatia Kanuni za Uchaguzi za TFF Ibara ya 11
(4) katika kikao chake kilichofanyika tarehe 30 Januari 2013, ilijadili
pingamizi zilizowekwa dhidi waombaji uongozi wa TFF na TPL Board na
kutoa maamuzi kama ifuatavyo:
1. Waombaji uongozi wa TPL Board
(a) Pingamizi dhidi ya Ndg. Said Muhammed Abeid anayeomba kugombea
nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi (TPL Board): Kamati
ilijadili pingamizi iliyowasilishwa na Ndg. Frank M. Mchaki dhidi ya
Ndg. Said Muhammed, aliyeoomba Kamati ya Uchaguzi ya TFF kumwondoa
mwombaji uongozi kugombea nafasi aliyoomba, kwamba Ndg. Said Muhammed:
(i) Si Mwenyekiti wa Klabu ya Azam na hivyo hana sifa za kugombea uongozi wa TPL Board.
(ii) Si mkweli katika maelezo aliyoyatoa kwenye fomu yake ya maombi ya uongozi.
Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilipitia maelezo ya Mweka pingamizi na
ilijiridhisha kuwa pingamizi iliyowasilishwa mbele yake na Ndg. Mchaki
haikukidhi matakwa Kanuni za Uchaguzi za TFF Ibara ya 11(2) kwa kuwa
haikuambatanishwa na vielelezo vyovyote kuthibitisha maelezo ya
pingamizi. Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeitupa pingamizi hiyo.
(b) Pingamizi dhidi ya Ndg. Yusufali Manji anayeomba kugombea nafasi ya
Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi (TPL Board): Kamati ilijadili pingamizi
zilizowasilishwa na Ndg. Daniel T. Kamna na Ndg. Juma Ally Magoma
walioomba Kamati ya Uchaguzi ya TFF kumwondoa mwombaji uongozi kugombea
nafasi aliyoomba, kwamba Ndg. Yusufali Manji:
(i) Hana uzoefu wa uendeshaji wa Mpira wa Miguu uliothibitishwa wa angalau miaka mitano (5) wa uendeshaji wa mpira wa miguu.
(ii) Hana sifa ya kuwa ama mchezaji Mpira wa Miguu, Kocha, Mwamuzi au
kushiriki katika uendeshaji wa Mpira wa Miguu katika ngazi ya Mkoa au
Ligi daraja la kwanza.
(iii) Hana elimu ya kidato cha nne
(iv) Ameshindwa kusimamia katiba ya Young Africans Sports Club Ibara ya 10(6), 18(1)b, 27 (2) na (5).
Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilipitia pingamizi hizo na ilijiridhisha kuwa
pingamizi zilizowasilishwa mbele yake na Ndg. Daniel T. Kamna na Ndg.
Juma Ally Magoma hazikukidhi matakwa Kanuni za Uchaguzi za TFF Ibara ya
11(2) kwa kuwa hazikuambatanishwa na vielelezo vyovyote kuthibitisha
maelezo ya pingamizi.Kamati ya Uchaguzi ya TFF imezitupa pingamizi hizo.
(c) Pingamizi dhidi ya Ndg. Hamad Yahya Juma anayeomba kugombea nafasi
ya Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi (TPL Board): Kamati ilijadili pingamizi
iliyowasilishwa na Ndg. Frank M. Mchaki dhidi ya Ndg. Hamad Yahya Juma,
kwamba Ndg. Hamad Yahya Juma:
(i) Si Mwenyekiti wa Klabu ya Mtibwa na hivyo hana sifa za kugombea uongozi wa TPL Board.
(ii) Si mkweli na mwadilifu na amekuwa akijipachika cheo cha mwenyekiti wa klabu.
Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeitupa pingamizi ya Ndg. Frank M. Mchakikwa
kuwa pingamizi iliyowasilishwa mbele yake haikukidhi matakwa ya Kanuni
za Uchaguzi za TFF Ibara ya 11(2) kwa kutoambatanishwa na vielelezo
vyovyote kuthibitisha maelezo ya pingamizi.
2. Waombaji uongozi wa TFF
(a) Pingamizi dhidi ya Ndg. Athumani K. Kambi anayeomba kugombea nafasi
ya Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF kupitia Kanda ya 9 (Mtwara na
Lindi): Ndg. Kambi aliwekewa pingamizi kwamba amefanya Kampeni kabla ya
muda uliopangwa.
Kamati imeitupa pingamizi ya Ndg. Jeremiah John Wambura kwa kuwa mweka
pingamizi hakutokea wakati alipotakiwa kufika kwenye Kamati ya Uchaguzi
kutoa utetetezi wake kuhusu pingamizi.
(b) Pingamizi dhidi ya Ndg. Eliud P. Mvella anayeomba kugombea nafasi ya
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF kupitia Kanda ya 7 (Iringa na
Mbeya): Ndg. Mvella aliwekewa pingamizi na Ndg. Said Kiponza, Ndg. Abu
Changawa na Ndg. Peter Naminga, kwamba Ndg. Mvella:
(i) Akiwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF kupitia Kanda hiyo ameshindwa kuleta maendeleo ya soka katika ukanda huo.
(j) Ana kesi ya rushwa katika mahakama ya wilaya ya Iringa
Kamati imeitupa pingamizi hiyo kwa kuwa haikukidhi matakwa ya Kanuni za
Uchaguzi za TFF Ibara ya 11(2) kwa kutoambatanishwa na vielelezo
vyovyote kuthibitisha maelezo ya pingamizi.
(c) Pingamizi dhidi ya Ndg. Epaphra Swai anayeomba kugombea nafasi ya
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF kupitia Kanda ya 3 (Shinyanga na
Simiyu): Kamati ilijadili pingamizi zilizowasilishwa na Ndg. Ramadhani
Sesso na Ndg. Tsotsie Chalamila, kwamba Ndg. Epaphra Swai:
(i) Alifanya ubadhilifu wa fedha alipokuwa Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mwanza (MZFA).
(ii) Alitumia madaraka yake vibaya alipokuwa MZFA kujinufaisha kwa kutumia MZFA.
(iii) Alivunja Katiba ya MZFA na FIFA
(iv) Anavuruga shughuli za uendeshaji mpira wa miguu mkoani Simiyu.
Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilipitia pingamizi hizo na ilijiridhisha kuwa
wawekaji pingamizi hawakuwa na sababu za msingi zilizoambatana na
vielelezo vinavyothibitisha maelezo ya pingamizi na kuwa pingamizi
zilizowasilishwa mbele yake zina chembechembe za wazi za mapatano ya
hila na udanganyifu (collusion) dhidi ya Ndg. Epaphra Swai. Kwa
kutokidhi matakwa ya Kanuni za Uchaguzi za TFF Ibara ya 11(2) na
hila/udanganyifu kwa Kamati, Kamati ya Uchaguzi ya TFF imezitupa
pingamizi hizo.
(d) Pingamizi dhidi ya Ndg. Vedastus F.K Lufano na Ndg. Mugisha
Galibonawanaoomba kugombea nafasi ya Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF
kupitia Kanda ya 2 (Mwanza na Mara): Ndg. Lufano na Ndg. Galibona
waliwekewa pingamizi na Ndg. Paul Mhangwa kwamba hawana uzoefu wa
uendeshaji wa Mpira wa Miguu wa miaka mitano (5).
Kamati imeitupa pingamizi hiyo kwa kuwa haikuzingatia Kanuni za Uchaguzi za TFF Ibara ya 11(2).
(e) Pingamizi dhidi ya Ndg. Michael R. Wambura anayeomba kugombea nafasi
ya Makamu wa Rais wa TFF: Pingamizi ziliwasilishwa na Ndg. Said Rubea
Tamim na Ndg. Josea Samuel Msengi kwamba Ndg. Wambura:
(i) Alikiuka Katiba ya TFF kwa kuishitaki Klabu yake ya Simba mahakamani kuhusu masuala ya uchaguzi.
(ii) Alikosa uadilifu kwa kutumia kampuni yake binafsi kufanya biashara na Taasisi aliyokuwa aniongoza akiwa Katibu Mkuu wa FAT.
(iii) Amekuwa akijaribu kupotosha umma kwamba vyombo vya TFF havifanyi
kazi zake kwa kutumia haki na kuviita ‘Mahakama za Kangaroo (Kangaroo
Courts).
(iv) Mwaka 2004 alikiri kwamba alikuwa akiandikwa vizuri na vyombo vya
habari kwa kuwa alikuwa akivipa pesa na kwamba vyombo vya habari
vilimgeuka kwa sababu aliacha kuwapa waandishi pesa.
(v) Mwaka 2004 alikataa kutekeleza maagizo ya FIFA ya kutaka nafasi ya Katibu Mkuu wa FAT iwe ya kuajiliwa.
(vi) Alikosa uwezo wa kutekeleza wajibu na malengo ya TFF.
Ndg. Josea Samuel Msengi aliondoa pingamizi lake dhidi ya Ndg. Wambura.
Kamati imelitupa pingamizi la Ndg. Said Rubea Tamim kwa kuwa halikukidhi
matakwa ya Kanuni za Uchaguzi za TFF Ibara ya 11(2).
(f) Pingamizi dhidi ya Ndg. Jamal E. Malinzi anayeomba kugombea nafasi
ya Rais wa TFF; Aliwekewa Pingamizi na Ndg. Agape Fue kwamba:
(i) Alivunja Katiba ya TFF kwa kufanya jitihada kubwa za kuhakikisha
kuwa wanachama wa TFF kikiwemo Chama chake cha Mkoa wa Kagera
haviheshimu wala kutekeleza maagizo ya TFF, CAF, CECAFA na FIFA baada ya
Kamati ya Utendaji ya TFF kuwasilisha mapendekezo ya mabadiliko ya
Katiba kwa njia ya Waraka, ambayo yalihusisha pia maagizo ya FIFA na
CAF
(ii) Hana sifa ya uzoefu wa miaka mitano katika uongozi wa mpira wa miguu.
(iii) Anakosa uadilifu na haiba ya kuliwakilisha Shirikisho nje na ndani.
Kamati imeitupa pingamizi ya Ndg. Agape Fue kwa kuwa mweka pingamizi
hakutokea wakati alipotakiwa kufika kwenye Kamati ya Uchaguzi kutoa
utetetezi wake kuhusu pingamizi hilo.
(g) Pingamizi dhidi ya Ndg. Athumani J. Nyamlani anayeomba kugombea
nafasi ya Rais wa TFF: Ndg. Nyamlani aliwekewa pingamizi na Ndg.
Mintanga Yusuph Gacha na Ndg. Medard Justiniani kwamba:
(i) Ni Hakimu Mkazi katika Mahakama ya Tanzania na kwa maana hiyo ni
mtumishi wa umma hivyo alikosa kigezo na sifa ya kugombea nafasi ya
urais wa TFF.
(ii) Anakatazwa na Judicial Service Act, Public Service Act 2002 na
Code of Conduct for Judicial Officers of Tanzania kugombea nafasi
aliyoomba ya Rais wa TFF.
(iii) Kutakuwa na Mgoganao wa kimaslahi endapo Ndg, Nyamlani atachaguliwa kuwa Rais wa TFF.
(iv) Amekosa umakini na uadilifu kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake na kusababisha Akaunti za TFF kufungiwa na TRA.
Ndg. Mintanga Yusuph Gacha hakufika kutetea Pingamizi lake ni hivyo
halikujadiliwa na Kamati. Kamati imelitupa pingamizi la Ndg. Medard
Justiniani kwa kuwa alishindwa kuithibitishia Kamati kuwa alikuwa na
ufahamu wa kutosha wa pingamizi lake ikiwa ni pamoja na viambatanisho
vyake, hali iliyotanabaisha kuwa pingamizi hilo lilikuwa na chembechembe
nyingi za hila na udanganyifu.
Imetolewa na:
Angetile Osiah
KATIBU
KAMATI YA UCHAGUZI
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)