Na Joachim Mushi
IMEELEZWA kuwa hali ya elimu nchini kwa sasa si
shwari hivyo ni wakati muafaka kwa wananchi na Serikali kuchukua hatua
madhubuti kukabiliana na hali hiyo. Changamoto hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya HakiElimu, Bi. Elizabeth Missokia alipokuwa
akizungumza na wahariri na waandishi wa habari kutoka vyombo anuai vya
habari kuzungumzia mustakabali wa elimu nchini.
Alisema shule zetu zinapaswa kutoa elimu inayomwezesha mwanafunzi
kujitambua na kumpa maarifa yatakayomsaidia kumudu mazingira yake jambo
ambalo halifanyiki kwa sasa kutoka na sera hafifu. “Wakati tukijaribu
kutafakari changamoto hizi katika sekta ya elimu ni muhimu tukajiuliza
tumefikaje hapa tulipo?,” alisema.
“Matatizo ya mfumo mbovu wa elimu yamechangia kwa kiasi kikubwa na kutokuwa na dira ya elimu, ambayo inatolewa na sera kwa takribani miaka mitano sasa Serikali imekuwa ikiahidi kukamilisha na kupitia sera ya elimu ya mafunzo ya mwaka 1995. Watanzania wamekosa dira ya elimu waitakayo kwa sababu Serikali imeshindwa kukamilisha uandaaji wa sera mpya ya elimu,” alisema.
Alisema Serikali imekuwa ikiandaa sera tangu mwaka 2007, lakini kwa
sababu zisizojulikana imekuwa ikisuasua katika ukamilishaji sera hiyo
mwaka hadi mwaka. “Sera ilianza kuandaliwa tangu mwaka 2007, Serikali kwa sababu zisizo
julikana imebaki ikipiga danadana kila mwaka. Ni dhahiri kwamba
kutokana na mabadiliko makubwa ya kiuchumi, kijamii na kisiasa nchini
inahitajika sera mpya itakayotupa dira sahihi ya sura ya elimu
tunayoitaka, pia kuandaa kutoelekeza mipango sahihi kuboresha mfumo wa
elimu hapa nchini,” alisema Bi. Missokia.
Alisema kikwazo kingine ni migogoro sugu katika sekta ya elimu
inachangia kudorora kwa elimu ya msingi na sekondari, kwani kwa kipindi
kirefu sasa sekta ya elimu imegubikwa na migogoro mingi ikiwemo madeni
ya walimu ambayo mgogoro wake umedumu kwa zaidi ya miaka minane.
Akizungumzia mvutano ulioibuka bungeni juu ya uwepo wa mitaala ya
elimu ama kutokuwepo, Meneja Utafiti na Uchambuzi wa Sera wa HakiElimu,
Godfrey Bonivetura alisema taasisi hiyo haijawahi kuona mtaala wowote
wa elimu licha ya wao kuomba mara kadhaa.
“Kwa mantiki hiyo sisi tunaamini mtaala haupo na kinachofanyika sasa
walimu hutumia muktasari wa masomo kufundishia…mwaka jana tulifanya
utafiti mmoja ambapo tulizungumza hadi na walimu nao walikuwa wakidai
hata wao hawajawahi kuona mtaala,” alisema.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Habari cha HakiElimu, Nyanda Shuli aliitaka
Serikali kuwa wazi juu ya suala hilo na kama kweli inayo mitaala iiweke
katika tovuti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ili wananchi na
wadau mbalimbali wa elimu waweze kuuona. “Ukiwauliza watendaji wa
Serikali juu ya suala la mtaala wanasema upo ukiuomba uuone utapigwa
danadana hadi unakata tamaa…,” alisema Nyanda.
Aidha aliiomba Serikali kuacha kuingiza siasa katika kushughulikia
masuala ya elimu kwani hali hiyo ndiyo iliyoifikisha elimu yetu hivi
sasa. Hivi karibuni ulizuka mjadala bungeni kuhusu kuundwa kwa kamati ya
kuchunguza mitalaa, sera na mihutasari ya elimu, hoja binafsi ambayo
iliibuliwa na Mbunge wa Kuteuliwa NCCR-Mageuzi, James Mbatia akilitaka
bunge kuunda Kamati kuchunguza suala hilo.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)