Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Bi. Lilian Liundi akizungumza
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Loyola ya jijini Dar es Salaam
wakifuatilia mada mbalimbali ndani ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake
Shule ya Sekondari Loyola.
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Loyola wakionesha ubunifu wa
mavazi katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Shuleni hapo.
Na Mwandishi wa Thehabari.com
KAIMU Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania
(TGNP), Bi. Lilian Liundi amesema wanawake wanaweza kuwa viongozi wazuri na
mfano wa kuigwa katika maeneo mbalimbali endapo watajengewa mazingira na
kuandaliwa mapema tangu wawapo shuleni.
Bi. Liundi ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Habari na
Mawasiliano ya TGNP ametoa changamoto hiyo leo katika Shule ya Sekondari ya
Loyola ya jijini Dar es Salaam alipokuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku
ya mwanamke shuleni hapo.
Akizungumza na umati wa wanafunzi wasichana wa shule hiyo na
wageni anuai waalikwa, alisema tafiti nyingi zilizofanywa zinaonesha kuwa
wasichana wanapoandaliwa mazingira mazuri ya elimu wanafanya vizuri
ukilinganisha na wavulana.
Aidha aliongeza kuwa kwa sasa zipo shule zinazochukua wasichana
pekee ambazo zimekuwa zikifanya vizuri zaidi jambo ambalo linaonesha wazi
mazingira mazuri yakijengwa jamii hii inaweza kuinuka na kuwa mfano mzuri.
Alisema kwa sasa vishawishi na changamoto anuai zilizopo
katika shule nyingi ndio kikwazo kwa wanafunzi wa kike kufanya vizuri, hali
ambayo ikifanyiwa kazi kiufasaha mabadiliko kimafanikio kwa kundi hilo yanaweza kutokea.
Hata hivyo alisema tafsiri iliyojengeka ya kwamba wanafunzi
wa kike wanaogopa masomo ya sayansi si sahihi kiuhalisia, kwani mazingira
ambayo wanafunzi hawa wanakumbana nayo ndio kikwanzo katika mafanikio yao kimasomo.
“Mfano shule nyingi za kata ni za kutwa wanafunzi hasa
wasichana wanakaa mbali na shule, wanalazimika kutembea umbali mrefu kwenda na
kurudi shuleni…wanakumbana na changamoto nyingi njiani hivyo wanajikuta
wanashindwa kufanya vizuri au kukatishwa kabisa masomo yao,” alisema Bi. Liundi.
Aliongeza kuwa eneo kama
hili, vyombo husika vikiangalia sheria na sera zinazojenga mazingira mazuri kwa
makundi yote, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha rasilimali zilizopo zinatumika
vizuri wasichana wanaweza kuingia katika ushindani kwa fursa zilizopo.
Kwa upande wake mwanafunzi Grace Ntambi wa kidato cha tano
wa shule hiyo aliiomba serikali kuendelea kutoa elimu kwa mikoa ambayo bado
inaendeleza mila potofu za kumbagua mtoto wa kike ikiwa ni pamoja na kuelemea
kwenye mfumo dume, ili kuangamiza vitendo hivyo.
“Na hii ianzie pia katika ngazi za familia kuna
kila sababu
ya kuondokana na mila potofu za kwamba mtoto wa kike hana haki ya kupata
elimu kama ilivyo kwa mtoto wa kiume…tuwatie moyo wasichana
kwani wanaweza,” alisema mwanafunzi huyo.
Katika hafla hiyo pia TGNP ilipata fursa ya kutoa mada
mbalimbali za masuala ya wanafunzi kujitambua kwa hatua anuai ikiwa ni pamoja
na kutoa ushuhuda ya kwamba wanawake wanaweza wakiamua kufanya hivyo kwa kila
hatua wanayopiga.
Imeandaliwa na Mtandao wa Thehabari.com (www.thehabari.com)
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)