Mkurugenzi
wa Idara ya Maendeleo ya Vijana nchini kutoka Wizara ya Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel akisisitiza kwa wajumbe
wa mkutano wa tathmini ya mbio za Mwenge mwaka 2012 kuhusu
serikali kufuatiliaji maendeleo ya miradi inayozinduliwa wakati wa mbio
za Mwenge mjini Zanzbar.
Mkuu
wa mkoa wa Shinyanga Ali Nassoro Lufunga akizungumza na viongozi na
waratibu wa mbio za Mwenge kutoka maeneo mbalimbali nchini kuhusu
maandalizi ya mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2013.Mkoa wa shinyanga
ulikuwa mwenyeji wa kilele cha mbio za Mwenge kwa mwaka 2012.
…………………………………………….
Na. Aron Msigwa – MAELEZO Zanzibar.
Serikali inaandaa utaratibu wa
kufuatilia maendeleo ya miradi yote inayozinduliwa wakati wa mbio za
Mwenge wa Uhuru ili kuhakikisha kuwa miradi hiyo inakua endelevu na
kuwanufaisha wananchi.
Kauli hiyo imetolewa leo mjini
Zanzibar na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana nchini kutoka
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Prof. Elisante Ole
Gabriel wakati akitoa tathmini ya mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2012 na
maendeleo ya miradi iliyozinduliwa wakati wa mbio hizo kwenye mkutano wa
viongozi na waratibu wa mbio za Mwenge kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Amesema serikali ina wajibu wa
kufuatilia kwa karibu miradi yote iliyozinduliwa na Mwenge wa Uhuru 2012
katika Halmashauri za wilaya, manispaa na Miji ili kuhakikisha kuwa
gharama kubwa iliyotumika wakati wa uanzishaji na ujenzi wa miradi hiyo
inawanufaisha wananchi kutoka kizazi kimoja hadi kingine ili kutunza
hadhi na heshima ya Mwenge wa Uhuru.
Amesema mbio za Mwenge wa uhuru
zimezindua miradi mingi nchini yenye thamani ya mabilioni ya fedha na
kuongeza kuwa si dhamira ya serikali kuona kuwa mwenge wa uhuru
unatumika tu kuzindua miradi ya maendeleo bali kuhakikisha uendelevu wa
miradi hiyo.
“Mbio za Mwenge wa Uhuru kila
mwaka zinazindua miradi mikubwa inayogharimu fedha nyingi, lazima
tufanye tathmini ya miradi yote inayozinduliwa na hatutapenda kuona
mwenge unatumika tu kuzindua miradi kwa maana sherehe, tutapenda kuwa na
taarifa za maandishi juu ya hali ya miradi hiyo ili itolewe kwenye
tathmini ya mbio za mwenge kwa miaka inayofuata” amesisitiza Prof.
Gabriel.
Amesema kuwa utaratibu huo wa
ufuatiliaji utawahusisha wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa
Halmashauri zote ambazo Mwenge wa Uhuru utazindua miradi katika maeneo
yao ili kutoa fursa kwa wananchi kuendelea kunufaika na miradi hiyo na
mbio za Mwenge wa Uhuru. Aidha Prof. Gabriel ametoa wito
kwa wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa miradi yote
inayozinduliwa na Mwenge wa Uhuru inapewa kipaumbele katika usimamizi
na ufuatiliaji.
Kwa upande wake Bw. Wito Mlemelwa
mmoja wa wakimbiza Mwenge wa Uhuru mwaka 2012 akitoa taarifa ya
tathmini ya mbio za Mwenge kwa wajumbe wa mkutano huo kwa niaba ya
kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa ametoa wito kwa watendaji na viongozi
wa maeneo mbalimbali kuhakikisha kuwa miradi yote inayotarajiwa
kuzinduliwa na Mwenge wa Uhuru inakamilishwa kwa ubora na viwango ili
kuepuka kukataliwa.
“Natoa wito kwa watendaji wa
maeneo mbalimbali wawe makini wahakikikishe kuwa miradi yote
inayozinduliwa na Mwenge wa uhuru inakidhi ubora na viwango vilivyowekwa
kulingana na gharama halisi ya fedha iliyotumika kwa sababu Mwenge wa
Uhuru hautahusika kuzindua miradi iliyo chini ya kiwango” amesisitiza
Bw. Mlemelwa. Katika kipindi cha mwaka 2012 mbio
za Mwenge wa Uhuru nchini zilizidua miradi 273 yenye thamani ya zaidi
ya shilingi bilioni 158.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)