Salaam Za Mwaka Mpya Kutoka Mjengwablog! - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Salaam Za Mwaka Mpya Kutoka Mjengwablog!

Ndugu zangu, 

Imekuwa ni utamaduni wangu kutuma salamu za Mwaka Mpya kwa wanakijiji wa Mjengwablog, marafiki zangu kwenye FB na wengine walio ndani na nje ya mitandao ya kijamii.

 Nimefanya hivyo tangu mwaka 2006 ilipoanzishwa Mjengwablog. Na mwaka huu naendeleza utamaduni huo. Nina mambo makubwa mawili kwenye salamu za mwaka huu, lakini, nitaanza salamu hizi kwa kukumbushua ahadi muhimu ya Mwana –TANU; kwamba; 

 ” Nitajielimisha kwa kadri ya uwezo wangu na kuitumia elimu yangu kwa manufaa ya wote”. 

 Ndugu zangu, 

Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita nilikuwa ndani ya garimoshi la Tazara nikielekea Dar kutokea kijijini kwetu Nyeregete. 

Nikiwa Nyeregete kwenye likizo ndefu ya kusubiri matokeo ya Kidato cha Nne, zilinifikia taarifa kuwa nahitajika haraka Dar es salaam kwenda kufanya maandalizi ya kuanza Kidato cha Kwanza shule ya Sekondari Tambaza. Masomo yetu pale Tambaza yalianza Januari 13, 1983. 

 Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita nilivuka kwa kuogelea korongo la Lihamile ili kuifikia Rujewa na hatimaye stesheni ya Tazara kule Ihanga. Korongo hilo lilijaa maji ya mvua ya masika yaliyokuwa yakipita kwa kasi. 

Hakukuwa na daraja. Baadae likajengwa daraja la magogo wakati wa kipindi cha Ubunge wa Kanali Mstaafu, Edmund Mjengwa. Daraja hilo sasa limeoza. Halipitiki. Ahadi nyingi zimetolewa kulijenga upya. Zimebaki kuwa ahadi. Ni daraja muhimu kiuchumi na kijamii kwa watu wa Nyeregete na wengine wengi wenye kulitumia. Ni kero kubwa kwa wananchi wa Nyeregete. 

Nimeongea na baadhi ya viongozi wa Nyeregete. Na nimewaambia, kuwa tushirikiane kuhakikisha, kuwa mwaka 2013 daraja hilo linajengwa hata kama ni kwa nguvu za wananchi. Tayari tumeshafanya utafiti na kuona inawezekana likajengwa kwa kiwango cha zege na chini ya shilingi milioni 20. 

Hivyo basi, mwaka 2013 nitashirikiana na wananchi wa Nyeregete na wengine wote watakaokuwa tayari kusaidia kuhakikisha tunapitisha harambee ya kujenga daraja hilo. Miaka 30 baada ya mimi kuvuka Lihamile kwa kuogelea itakuwa ni aibu kubwa kuwaona tena wananchi wa Nyeregete na wengine wakivuka korongo hilo kwa kuogelea. Ni nini basi maana ya kwenda shule?

 Ndugu zangu, 

Maji ni kero kubwa kwa wananchi wengi wa Bonde la Usangu, Mbarali Mbeya. 

Badala tu ya kuilalamikia na kuisubiri Serikali iwasaidie wananchi kutatua kero ya maji, mwaka 2013 nimeazimia nitashirikiana na wanakijiji wa vijiji vya Magwalisi na Lihamile wilayani Mbarali ili tuweze kuchangisha fedha za kuchimba visima vya pampu kimoja katika kila kijiji husika. 

Nitashiriki kuchangisha sehemu ya fedha zinazohitajika kugharamia visima hivyo kwa kupanda Mlima Kilimanjaro, kitu ambacho nimependa nikifanye katika maisha yangu lakini sijapata bahati ya kufanya. 

Ndugu zangu, 

Hayo ni mawili makubwa niliyotaka kuyasema kupitia salamu za mwaka mpya wa 2013. 

Ni matumaini yangu, Desemba 31, 2013 Mungu atanijalia uhai na kurudi tena hapa kutoa tena salamu za mwaka mpya huku hayo mawili yakiwa tayari yameshafanyiwa kazi kwa nguvu za pamoja, ikiwamo ushirikiano wenu. Nawatakia Heri na Fanaka Za Mwaka Mpya wa 2013. 

Maggid Mjengwa, 

 Morogoro

 0788 111 765

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages