Na Zitto Kabwe
'Dar inachangia asilimia 80 ya mapato. Kitovu cha Uchumi. Dar inachangia 90% ya ufisadi. Uti wa mgongo wa ufisadi nchini'
Malumbano kati
ya wananchi wa Mtwara na Serikali kuhusu matumizi bora ya utajiri wa
nchi yameendelea kwa takribani wiki moja sasa. Baada ya Mkuu wa Mkoa wa
Mtwara na Waziri wa Nishati na Madini kuwaita Watanzania wa Mtwara
Wahaini, wapuuzi na watu hatari, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
naye aliingia kwenye mjadala huo kwa kuonya watu wanaowaunga mkono watu
wa Mtwara na kuwaita watu wanaotafuta umaarufu wa kisiasa na wanaotaka
kugawa nchi. Siku moja baada ya hotuba ya Rais, Waziri wa Nishati na
Madini alifanya mkutano na waandishi wa habari kueleza suala lile lile
ambalo bosi wake alilielezea usiku wa kuamkia mwaka mpya 2013. Hii ni
dalili ya Serikali kuweweseka.
Katika kauli
ya Serikali, ambayo haikuwa na jipya zaidi ya wimbo ule ule wa ‘kugawa
nchi’ ‘umaarufu wa kisiasa’ nk, Serikali ilitaka kuonyesha umma kuwa
watu wa Mtwara hawana shukurani. Kwamba miaka yote toka Uhuru watu wa
Mtwara wamekuwa wakilishwa na Pamba, Kahawa, Chai, Tumbaku, Sukari,
Kidatu nk. Kwamba watu wa Mtwara na Lindi hawakuchangia hata kidogo
kwenye hazina ya Taifa. Hivyo wao kupigia kelele gesi yao ni uchoyo na
roho mbaya na kukosa shukurani. Kauli ya Serikali ni kauli ya chombo
kinachoendelea kukosa ‘legitimacy’ ya kuongoza taifa. Ni kauli ya kukata
tamaa. Ni kauli hatari sana dhidi ya Watanzania waliojitolea damu
kulinda uhuru wa nchi yetu.
Moja, Serikali
katika kauli yake haitaji kabisa kwamba toka Uhuru watu wa Mtwara na
Lindi wamekuwa wachangiaji wakubwa sana katika uchumi wa Taifa kupitia
zao la Korosho. Takwimu za Uzalishaji wa Korosho zinaonyesha kwamba
kuanzia mwaka 1965 mpaka 2011 Korosho imeliingizia Taifa fedha kigeni
jumla ya dola za Kimarekani 4.58 bilioni ( Cashewnuts Sub-sector study
2003, Hali ya Uchumi 2012, Cashewnuts Tanzania Report 2010). Katika
Mwaka wa Uchumi unaoishia Novemba 2012, Korosho imeliingizia Taifa jumla
ya dola za Kimarekani 151 milioni. Katika mwaka 2011 zao hili
liliingiza dola 130 milioni wakati Pamba iliingiza dola 53 milioni tu.
Licha ya Zao la Korosho kuingiza fedha hizi za kigeni (sawa ni shilingi
trilioni 7.2) kwa nchi mikoa ya Lindi na Mtwara ipo miaka 50 nyuma
kimaendeleo kulinganisha na mikoa mingine ya Tanzania. Serikali inataka
kufuta historia ya mchango wa zao la Korosho kwenye uchumi wa nchi yetu
kwa sababu ya uroho wa gesi asilia. Kwa nini kauli rasmi ya Serikali
haijataja Korosho kabisa? Kauli hii ilipitishwa na ngazi zote za
Serikali? Mawaziri wa Serikali wanaotoka mikoa ya Lindi na Mtwara
walikubali kauli kama hii itoke dhidi ya wananchi wao wanaoteseka na zao
la Korosho miaka nenda miaka rudi?
Pili, Serikali
imesahau kabisa mchango wa watu wa Lindi na Mtwara katika ulinzi wa
Taifa letu. Moja ya sababu ya mikoa ya Lindi na Mtwara kuwa nyuma
kimaendeleo ni juhudi za ukombozi wa kusini mwa Afrika. Kambi ya
wapigania uhuru wa Msumbiji ilikuwa Nachingwea. Kambi ya Frelimo
iliwekwa kwenye Shamba la Mkonge kilometa 17 tu kutoka mjini Nachingwea
ambapo ilikuwa makao makuu ya ukombozi wa Msumbiji. Rais Samora Machel,
Rais Joaqim Chissano na Rais Guebuza waliendesha mapambano kutoka kusini
mwa Tanzania. Makaburu wa Afrika Kusini na Wareno walikuwa
wanashambulia nchi yetu na mikoa hii miwili ya Lindi na Mtwara ikawa
‘buffer zone’. Wakati Dar es Salaam inaendelea kwa kila aina ya
maendeleo, mikoa ya Lindi na Mtwara ilikuwa inalinda ili wanaoishi Dar
es Salaam na mikoa mingine waishi wa amani na starehe. Serikali
inapimaje mchango huu wa mikoa hii? Tunaipima kwa fedha? Uroho wa gesi
asilia kuzalisha umeme wa kufurahisha walalaheri asilimia 14 nchini ndio
inaifanya Serikali kusahau kabisa ‘sacrifice’ ya watu wa Mtwara katika
kulinda uhuru wa Taifa letu?
Tatu, Serikali
inasema lazima bomba lije Dar es Salaam kwa sababu Dar ndio inazalisha
asilimia 80 ya Mapato ya Serikali. Kwanza huu ni uwongo. Ni aibu
Serikali kujitetea kwa uwongo. Dar es Salaam ni kituo tu cha kukusanyia
mapato ya Serikali. Uzalishaji mkubwa wa nchi yetu wenye kuzalisha kodi
unafanyika nje ya Dar es Salaam. Walipa kodi wakubwa wengi Ofisi zao Kuu
zipo Dar es Salaam lakini uzalishaji wao unafanyika nje ya Dar es
Salaam. Serikali itoe orodha ya walipa kodi wakubwa 100 tuone uzalishaji
halisi wa mapato hayo unafanyika wapi.Hata hivyo inawezekana kuwa
ikawa kweli Dar es Salaam inakusanya asilimia 80 ya mapato ya nchi. Basi
na tuseme Dar es Salaam inachangia asilimia 90 ya ufisadi wote nchini.
Kashfa zote kubwa za Ufisadi zinafanyika Dar es Salaam na fedha nyingi
za ufisadi zinatumika Dar es Salaam.
Mwisho,
maandamano ya watu wa Mtwara ni kielelezo tosha kwamba watu wa mikoa ya
Lindi na Mtwara wamechoshwa na longolongo za Serikali. Wananchi wa
Mtwara na Lindi wanataka Uwajibikaji wa Serikali kuhusu utajiri wa nchi.
Mtanzania yeyote mwenye tahadhari ya nchi yetu kutokuwa na laana ya
rasilimali ataungana mkono na watu wa Lindi na Mtwara kudai maendeleo.
Nilitoa mfano wa Mgodi wa Golden Pride ambao umemaliza dhahabu yote tani
76 katika eneo la Lusu wilayani Nzega. Kampuni ya Resolute ya
Australia iliwekeza dola 370 milioni kuanzia mwaka 1998 (mkataba wao
ulisainiwa 25th June 1997). Katika kipindi cha uhai wa mgodi, miaka 14,
Kampuni hii imeuza dhahabu ya thamani ya dola za kimarekani 3.3
bilioni. Kabla Serikali haijawaita watu Mtwara wahaini, wapuuzi na watu
hatari, iwaambie watu Watanzania kodi kiasi gani imekusanywa kutoka
mgodi huu katika kipindi cha miaka 14. Mpaka mwaka 2008, kwa mujibu wa
Taarifa ya Kamati ya Bomani, kampuni hii ilikuwa imelipa mrahaba wa dola
11 milioni na kodi nyingine dola 16 milioni. Serikali itwambie ilipofika Disemba 2012 kodi kiasi imekusanywa kutoka kampuni hii?
Pia watu wa
Mtwara na Lindi wameona historia ya bomba la Songosongo. Hata kodi ya
Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa (0.3%) ilikuwa inalipwa Halmashauri ya
Manispaa Ilala na kampuni ya Pan Africa Energy. Ilichukua juhudi za
mbunge wa Kilwa Kaskazini Murtaza Mangungu kuingilia kati ndio kodi
ikaanza kulipwa Kilwa ambapo uzalishaji unafanyika. Watu wa Mtwara ni
werevu, wanajua wafanyalo. Wanataka utajiri wa nchi unufaishe nchi kwa
kuanzia kule utajiri ulipo. Kuna dhambi gani?
Uwajibikaji
katika uvunaji wa Rasilimali ya Gesi ndio chanzo cha maandamano ya watu
wa Mtwara. Serikali isikimbilie kulaumu wanasiasa kwamba ndio
wamechochea maandamano haya. Haya ni maandamno ya wananchi wakitaka
Serikali yao iwajibike kwao. Serikali ithubutu kufanya ubabe wa kujenga
bomba la gesi bila ridhaa ya Wananchi wa Lindi na Mtwara. Wananchi
wanapohitaji uwajibikaji ni wajibu wa Serikali kuwajibika kwao ni sio
kuwaita wahaini, wachochezi, watu hatari, wapuuzi. Watu wa Mtwara
wamechangia maendeleo ya Taifa letu kwa jasho na damu. Serikali ina
wajibu wa kuwasikiliza, kuwaelimisha na kupata mwafaka. Kauli ya
Serikali imewatukana watu wa Mtwara na Lindi. Hawatakubali
kudhalilishwa. Hawatakubali historia yao kufutwa. Hawatakubali waendelee
kubaki nyuma kimaendeleo. Serikali ifikirie tena.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)