Kibao cha Shule ya Sekondari ya Bungu
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Bungu, Dismas Kimweli akizungumza na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni
*Imeandaliwa na Thehabari.com kwa ushirikiano na HakiElimu
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Bungu, Dismas Kimweli akizungumza na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni
Na Mwandishi wa Thehabari.com, Korogwe
SUALA la kuwepo na utata kwa baadhi ya wanafunzi
kukwamishwa na fomu namba 9 ya Takwimu za Shule za Msingi kwa mwanafunzi (TSM9)
kufanya mitihani yao katika shule anuai za sekondari limezua mvutano kati ya wazazi
wa wanafunzi na walimu huku kila upande ukitupa lawama kwa mwenzake.
Baadhi ya
wanafunzi na wazazi waliohojiwa wamedai uzembe upo kwa walimu ambao hutumia
majina ya wanafunzi wengine kuingiza wanafunzi kinyemela, jambo ambalo huzua
utata baadaye kwa mwanafunzi aliyeingia kwa njia hiyo anapokaribia kufanya
mitihani yake.
Uchunguzi
uliofanywa na mwandishi wa habari hizi wilayani Korogwe katika shule kadhaa za
sekondari na msingi umebaini kuwa wapo wanafunzi ambao wamezuiwa kufanya
mtihani wa mwisho wa kidato cha nne na ule wa kidato cha pili wa mchujo
kutokana na hali kama hiyo ya utata katika suala hilo la TSM9.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Bungu,
Dismas Kimweli ambaye shule yake ilikuwa miongoni mwa shule
zilizolalamikiwa, akizungumza na mwandishi wa habari hizi alipinga kuwepo na
wanafunzi waliozuiliwa kufanya mitihani yao kutokana na utata wa fomu namba 9.
Mwalimu
huyo alisema idadi kubwa la wanafunzi ambao hukumbwa na matatizo kama hayo ni
wanafunzi ambao huingia shuleni kwa njia ya uhamisho huku wazazi wao wakiomba
mwanafunzi aendelee kusoma wakati utaratibu wa kufuatilia uhamisho ukiendelea.
“Unakuta
mzazi anamleta mtoto kujiunga na shule yako akitokea shule nyingine na anaomba
aendelee kusoma wakati akiendelea kufuatilia uhamisho...lakini baadaye anakaa
kimya sasa mtoto anakuwa anaendelea na shule bila kuwa na uhamisho ambao
hujumuisha TSM9, ikifika kipindi cha mitihani hapo linakuwa tatizo na mzazi
anajifanya kasahau,” alisema.
“Sasa kama
mtu hajatimiza vitu kama hizi anarushaje lawama kwa walimu au shule...lakini
ikifikia hatua hii wapo ambao huwaeleza nao kuelewa na wapo ambao huwa na
mvutano kidogo,” aliongeza mwalimu huyo.
Akitoa
ufafanuzi wa suala hilo, Kaimu Ofisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, Shaban
Shemzighwa alikiri kuwepo kwa malalamiko ya baadhi ya wanafunzi kutokuwa na
TSM9 hasa wa kidato cha pili lakini alidai waliruhusiwa kufanya mitihani yao na
wao kuwaagiza wakuu wa shule wanazotoka kuhakikisha wanawasilisha namba zao
kwenye vituo inakosahishiwa mitihani.
“Taarifa za
malalamiko zilitufikia na baadhi ya Shule za Sekondari ambazo wanafunzi
walikuwa na matatizo hayo ni Bungu, Patema, Mfundia na nyinginezo, hapa nipo
nje ya kituo cha kazi hivyo ni vigumu kutaja idadi na shule zote,” alisema Shemzighwa
akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu.
Aidha
akifafanua zaidi alisema wanafunzi wengi waliokuwa na matatizo kama hayo wa
kidato cha pili ni wale waliohama kutoka shule moja kwenda nyingine, ambao
hawakuja na TSM9 zao. “…Hata hivyo waliruhusiwa kufanya mitihani na maelekezo
tuliwapa wakuu wa shule kuhakikisha wanapeleka namba za wanafunzi hao katika
kituo cha kusaishia mitihani ili waweze kutambuliwa kihalali vinginevyo
hawawezi kutambulika,” alisema ofisa huyo.
Alisema
inaonekana kuna baadhi ya walimu wakuu walipokea wanafunzi bila TSM9, hata
hivyo haikujulikana kama ni kwa njia ya kinyemela au matatizo ya uhamisho kwa
wanafunzi hao kutoka shule moja hadi nyingine. Hata hivyo licha ya kiongozi
huyu kuitaja Bungu kuwa miongoni mwa shule zilizotolewa tarifa kuwa na tatizo
la fomu namba 9, mkuu wa shule hiyo alipinga shule yake kuwemo.
*Imeandaliwa na Thehabari.com kwa ushirikiano na HakiElimu
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)