JESHI la Polisi limetoa siku saba kwa baadhi ya askari
kuzisalimisha fedha zipatazo sh milioni 150 wanazodaiwa kuiba, ambazo
zilizoporwa na majambazi Mtaa wa Mahiwa na Livingston jijini Dar es
Salaam juzi.
Akizungumza na waandishi wa
habari jijini, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum, Suleiman Kova, alisema
kutokana na tuhuma hizo jeshi hilo limeunda Jopo la wapelelezi ili
kujua ukweli wa madai hayo.
Alisema Jopo hilo litaundwa na
watu watano, likiongozwa na Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum, Ahmed
Msangi, atakayehakikisha kwamba muda mfupi inavyowezekana, ukweli
upatikane ili wananchi wajulishwe matokeo.
Kamanda Kova alisema jeshi hilo
lina mfumo wake wa kuchunguza askari wake inapotokea amejihusisha katika
matukio yanayokwenda kinyume na maadili ya kazi yake.
Alisema tukio hilo halikubaliki
hivyo kila aliyepewa jukumu la kulifuatilia ni lazima ahakikishe kuwa
anafanya kazi kwa ufasaha ili majibu yapatikane haraka kuondoa shaka
shaka kwa wanachi.
Kova alimtahadharisha Msangi
kuwa, endapo atashindwa kutoa majibu ya kuridhisha basi atambue hata
yeye itabidi awajibike ambapo alisema vitu kama hivi vikiachwa viendelee
vinaliletea jeshi hilo sifa mbaya na kupoteza imani kwa wananchi.
“Pamoja na kumkabidhi kazi hiyo
Msangi lakini hata mimi sitakaa kimya bali nitalifuatilia kwa karibu ili
mradi tuwapatie wananchi ukweli”alisema Kova.
Alibainisha kuwa hawezi kupinga
kama askari wanaweza kushiriki katika vitendo hivyo viovu bali suala
hilo bado linahitaji ushahidi zaidi hivyo, ni vema wananchi wenye
ushahidi wakatoa ushirikiano utakaosaidia kupatikana fedha hizo.
Aidha, Kova alilitaka jeshi la
polisi kufanya kazi zake kwa nidhamu, uaminifu na ueledi kwani endapo
ofisa au askari atakiuka maadili ya kazi yake, basi hatua madhubuti
zitachukuliwa dhidi yake bila kuchelewa.
Hata hivyo, katika hali ya
kushangaza jopo hilo linaundwa na polisi wenyewe bila kushirikisha wadau
wengine kwa madai kuwa, eti lifanya kazi kwa kutii sheria zote bila
kwenda kinyume.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)