Staa wa Vichekesho na Filamu Bongo, Said Mohamed Ngamba ‘Mzee Small’ akiwa amelazwa hospitali kutokana na maradhi yanayomsumbua.
KWENU mnaohusika na sanaa ya filamu Bongo. Mnajitambua sina haja ya kuwataja mmojammoja kwa majina, nitamaliza ukurasa bure.
Mimi najua mpo poa, mnaendelea na majukumu yenu ya kila siku. Binafsi niko poa, naendelea na majukumu yangu ya kila siku ikiwamo hili la kuwaandikia barua.
Barua yangu leo moja kwa moja nailekeza kwa nyinyi wote ambao watu sasa hivi wanawatambua kwa jina la mastaa wa filamu katika soko la Bongo, Bongo Movies.
Kikubwa ni kwamba, natambua mchango mlionao katika kusogeza gurudumu la maendeleo ya nchi. Natambua umuhimu wenu wa kuwatibu watu kisaikolojia kupitia filamu zenu mnazozifanya.
Hongereni kwa hilo.Katika taaluma yangu ya uandishi wa habari, mara kadhaa nimeshuhudia uwezo wenu katika kufanikisha mambo yanayowahusu, iwe ni sherehe au misiba.
Eeeh, kwenye sherehe basi mnalipuka na kushangweka kwelikweli. Kwenye misiba, mnahakikisha mnamsindikiza mtu anayewahusu kwa hadhi anayostahili.
Hoja hapa ni kwamba, hadhi ile ambayo mnajitutumua hadi kwenye misiba, kwa nini tusioneshe kwa mkongwe wa sanaa nchini, Said Ngamba ‘Mzee Small’? Tunashindwa nini? Mbona pesa zipo?
Kwa nini tusimsaidie mzee wetu ambaye tunaimani alikuwa chachu ya vijana wengi kuingia kwenye sanaa?
Mzee wetu anasumbulia na ugonjwa wa kupararazi. Anashindwa kufanya shughuli zake za sanaa ambazo ndiyo chanzo cha pato lake la kila siku.
Binafsi nilisikitishwa na kupongeza kitendo cha Rais wa Shirikisho la Filamu nchini TAFF, Saimon Mwakifwamba kuingilia kati na kuanza kutembeza ‘bakuli’ la michango kwa ajili ya kumsaidia mzee huyo.
Nilisikitika kwani sikuona haja ya yeye kuingilia kati suala hilo ambalo naamini lilikuwa chini ya uwezo wenu, mnaweza bwana! Kikubwa ni kipi haswa? Mbona mna ‘mauwezo’, msinifanyie hivyo bwana.
Kwani kuna tatizo gani tukiweka nukta katika starehe hata kwa siku moja, tusipige kilevi siku hiyo halafu tujichangishe fedha za kumpa sapoti mwenzetu kwenye kipindi hiki ambacho anaumwa?
Hakika hili ni dogo, tukiamua tunaweza tena haliwezi kuharibu bajeti zenu hata kidogo.
Ni yule yule,
Mkweli Daima.
Joseph Shaluwa
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)