Waziri wa Uchukuzi Dk Harrison Mwakyembe na wananchi wa kila rangi na jinsia katikati ya maongezi.
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe akisikiliza hoja baada ya kikao
Aseri Katanga akiwa mjadalani kwa chai na Billy Mwangamilo na George Kantande .
David Luhanga na Rajab Juma wamekita ndani ya maongezi.
Dk Hamza na wenzake katika chai.
Mtayarishaji wa mkutano Andrew Coulson akipiga gumzo kwa chai na mmoja wa wahudhuriaji.
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe akihutubia mkutano
Sister Lucia akiuliza swali kuhusu ajali ya meli Zanzibar.
Rashid Dilunga akiwa kazini.Habari na Picha za Freddy Macha
---
Habari na Picha za Freddy Macha
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amewahakikishia
Watanzania na wageni kwamba jitihada zitaendelea kufanywa na serikali
kuboresha usafiri Bongo.
Akiongea mjini London juzi katika “mkutano wa mwaka”
wa jumuiya ya Watanzania na Waingereza (Britain-Tanzania Society) na
Mfuko wa Udhamini wa Maendeleo (Tanzania Development Trust), alisema
bado pana mengi sana ya kufanya toka ateuliwe miezi minne iliyopita.
Waziri Mwakyembe vile vile alifafanua kuhusu majadiliano
ya katiba mpya inayotegemewa kutajwa mwaka 2015.
Akijibu maswali toka kwa Wazungu na Watanzania waliohudhuria
kikao Central Hall, Westminster, hatua chache karibu na Ikulu
ya Uingereza (Whitehall), Mwakyembe ambaye ni mbunge wa Kyela, alifahamisha
kuwa moja ya tatizo lililojaribu kutafutiwa ufumbuzi karibuni ni kuzorota
kwa bandari ya Dar es Salaam. Alisema Wizara ilibidi kubadili uongozi
wa bandari hiyo baada ya ripoti ya kimataifa iliyoichamba Dar kuwa moja
ya bandari mbaya duniani zisizotekeleza kazi zake sawasawa.
“Bandari ya Dar es Salaam ina uwezo wa kulisha
uchumi wa nchi nzima ikiendeshwa vyema,” aliueleza mkutano uliomsikiliza
kwa makini. “Tumezungukwa na nchi nyingi zisizo na bahari ambazo zinatutegemea
kusafirisha mizigo yake. Kwa hiyo basi, wizara ya uchukuzi ikilala na
taifa zima linalala.”
Akitoa mifano kadhaa ya hali mbaya ya usafiri nchini,
Dk Mwakyembe aliongelea kwa hamasa na matumaini kuhusu ujenzi wa barabara
na reli mbalimbali. “Tuna mengi bado ya kufanya. Reli zetu kubwa
ni za kale sana. Ya toka Dar hadi Kigoma na Mwanza mathalan ilijengwa
enzi za Wajerumani kwa hiyo yabidi kutengenezwa upya.”
Alitoa mfano wa ufumbuzi wa tatizo la msongamano
wa magari jijini Dar es Salaam ambapo pesa zilizopangwa kurekebisha
njia nyingine mikoani zimetumika kurahisisha usafiri kati ya Ubungo
hadi mjini na Makanga hadi Kurasini ( kwa nauli nafuu ya shilingi 500)
na muda mfupi wa dakika ishirini.
Akiwaelemisha waliokuwepo kuhusu maendeleo ya kisiasa
Tanzania, Waziri alisema mjadala unaosisimka nchini sasa hivi unahusu
mageuzi ya katiba ambayo “inatakiwa ioane na maisha ya karne ya 21.”
Akifafanua historia ya katiba Tanzania kwa lugha
ya fasaha ya Kiingereza, Waziri huyu ambaye ni mtaalamu wa sheria,
alitaja miaka muhimu kuwa 1961( baada ya Uhuru),1963 (Ujenzi wa taifa
jipya), 1965 (Muungano), 1977 ( kuzaliwa CCM) kisha 1983 na
kupitishwa sera ya vyama vingi mwaka 1992.
Maswali mengi yaliulizwa kuhusu usafiri na ulaji
rushwa uliochangia sana uzorotaji unaoendelea kusababisha ajali kubwa
na za kutisha bara na visiwani.
Na hata baaada ya hotuba rasmi, wakati wa kupata
chai, wananchi na wageni waliendelea kumsonga na kumzunguka Waziri
wakimjuza kwa maswali moto moto. Kiongozi hakuonyesha dalili zozote
za kuchoshwa na shauku hiyo.
Akimshukuru Waziri, mmoja wa maofisa wa Jumuiya ya
Waingereza na Watanzania, Bi. Valerie Leach (anayeendesha shughuli za
kielimu Bongo) alisema inawapa wageni moyo kwamba Tanzania inao viongozi
wanaokinzana na rushwa na ufisadi kama ilivyokuwa enzi zile za Mwalimu
Nyerere.
Mapema Dk Harrison Mwakyembe alikaribishwa kwa maelezo
ya namna alivyoshaokoka kufa mara mbili (ajali ya gari na maradhi ya
ngozi) kutokana na msimamo wake kujaribu kuendeleza jamii.
Mapema mkutano ulielezwa miradi mbalimbali
inayoendelezwa na Mfuko wa Udhamini wa Maendeleo (Tanzania Development
Trust). Kati ya miradi hiyo ni kukarabatiwa nyumba ya wazee Tanga, uendelezaji
wa viwanda vidogo vidogo 37 bara na visiwani, maendeleo ya vijana
wasiokuwa na kazi na vifaa vya wafanyakazi wa hospitali ya Lindi kuepuka
kipindupindu.
Akielezea mapenzi yake kusaidia maendeleo Tanzania,
mwanamakati wa Jumuiya ya BTS, Julian Marcus alisema jitihada za wanachama
zinatokana na michango binafsi na kujitolea bila malipo yeyote.
Shughuli hii ya Jumamosi vile vile ilihudhuhuriwa
na Balozi wetu Uingereza, Mheshimiwa Peter Kallaghe na Mkurugenzi wa
kituo cha biashara London, Yusufu Kashangwa.
Jumuiya ya BTS ilianzishwa mwaka 1975 na Waingereza
na Watanzania kuendeleza mahusiano kati ya nchi hizi mbili. Inaongozwa
na Rais wa zamani, Ali Hassan Mwinyi.
Kikao kijacho cha BTS kitafanyika chuo kikuu cha
lugha za Kiafrika na Asia (School of Oriental and African Studies-SOAS)
London kujadili demokrasia na vyombo vya habari Tanzania, tarehe 6 Desemba.
Kila mwananchi na rafiki wa Tanzania anakaribishwa.
Habari zaidi www.btsociety.org
Au wasiliana na Andrew Coulson
– simu (+44) 121-475-4615
Barua pepe: a.c.coulson@bham.ac.uk
Tovuti: www.freddymacha.com
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)