Tume ya Mabadiliko ya Katiba
imetangaza namba nne (04) za simu za mkononi ambazo wananchi kwa sasa
wanaweza kuzitumia kutuma ujumbe mfupi wa maandishi (‘sms’) kutoa maoni
yao kuhusu Katiba Mpya.
Kwa mujibu wa taarifa ya Tume
hiyo kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo (Jumatano, Oktoba 31, 2012)
namba ambazo wananchi wanaweza kutuma maoni yao kwa njia ya ‘sms’ ni
0715 (Tigo) /0767 (Vodacom) / 0787 (Airtel) / 0774 (Zantel) – 08 15 08.
“Kwa kuzingatia kuwa Watanzania
wengi waliopo mijini na vijijini wanamiliki simu za mkononi, Tume ya
Mabadiliko ya Katiba inaamini kuwa njia hii ni fursa nyingine muhimu kwa
Watanzania kuweza kuwasilisha maoni yao kwa Tume,” imesema sehemu ya
taarifa hiyo iliyotolewa na Katibu wa Tume hiyo Bw. Assaa Rashid.
Ili kutuma maoni, Bw. Assaa
amesema, mwananchi anapaswa kufungua ukurasa wa kutuma ujumbe mfupi wa
maandishi (sms) katika simu yake na kuandika maoni yake pamoja na jina
lake kamili, jinsia, mahali anapoishi, umri, elimu na kazi na kutuma
kwenda kwenye namba yoyote kati ya zilizotolewa.
Kwa mujibu wa Bw. Assaa, baada
ya kutumwa, maoni hayo yatakwenda kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
ambapo yatafanyiwa kazi pamoja na maoni yanayokusanywa kwa njia
nyingine.
Uanzishwaji wa njia hii ya
ujumbe mfupi wa maandishi unalenga kuwapa fursa nyingine wananchi kutoa
maoni yao. Tume ya Mabadiliko ya Katiba pia inapokea maoni ya wananchi
kupitia mikutano ya ana kwa ana; barua pepe (maoni@katiba.go.tz);
njia za posta (S.L.P. 1681, Dar es Salaam au S.L.P. 2775, Zanzibar);
ukurasa wa ‘facebook’ (Tume ya Mabadiliko ya Katiba) na tovuti (http://www.katiba.go.tz/).
Katika taarifa yake hiyo, Tume
imewaomba wananchi kutumia namba hizo kutuma maoni yao binafsi kuhusu
Katiba Mpya bila kushawishiwa na watu, makundi, vyama au taasisi yoyote
na kufafanua kuwa Tume inatarajia kuanza kupokea maoni ya makundi,
vyama na taasisi mara baada ya kumaliza kukusanya maoni binafsi ya
wananchi katika awamu ya nne na ya mwisho itakayomalizika mwezi Desemba,
2012
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)