Tume
ya Mabadiliko ya Katiba inatarajia kuendelea na awamu ya nne na ya
mwisho ya mikutano yake na wananchi wa mikoa sita kuanzia siku ya
Jumatatu, Novemba 19, 2012 hadi Jumatatu, Desema 19, 2012 kwa lengo la
kukusanya maoni yao kuhusu Katiba Mpya.
Mikoa hiyo ni Dar es Salaam,
Arusha, Simiyu, Geita, Mara na Mjini Magharibi na kila siku kutafanyika
mikutano miwili, wa kwanza utaanza saa 3:00 asubuhi – saa 6:00 mchana na
kufuatia na mwingine utakaoanza saa 8:00 alasiri – saa 11:00 jioni.
Taratibu zote za kuanza kazi ya
kukusanya maoni katika mikoa iliyotajwa zimekamilika zikiwemo kuandaa
ratiba na kuisambaza katika ofisi za mikoa, wilaya na Halmashauri za
Manispaa na Wilaya husika. Wajumbe wa Tume na watumishi wa Sekretarieti
wamejigawa katika makundi saba. Kila mkoa utakuwa na kundi moja
isipokuwa Dar es Salaam ambao utakuwa na makundi mawili.
Katika mkoa wa Dar es Salaam Tume
imejigawa katika makundi mawili na siku hiyo ya Jumatatu itaanza na
Wilaya za Temeke na Ilala. Katika wilaya ya Temeke, Tume itaanza na eneo
la Keko wakati katika wilaya ya Ilala itaanza na eneo la Jangwani kwa
mikutano itakayoanza saa 3:00 asubuhi. Kwa mikutano ya alasiri, wilayani
Temeke mkutano huo utafanyika Chang’ombe na ule wa Ilala utafanyika
Tabata.
Kwa upande wa mkoa wa
Arusha, Tume itaanza na Wilaya ya Karatu eneo la Mbulumbulu wakati
mkoani Mara Tume itaanza katika Wilaya ya Tarime eneo la Bumera. Kwa
mkoa wa Simiyu, Tume itaanza na Wilaya ya Busega eneo la Lamadi na
mkoani Geita, Tume itaanza na Wilaya ya Chato eneo la Kachwamba. Kwa
mkoa wa Mjini Magharibi, Tume itaanza katika Wilaya ya Magharibi.
Tume inawaomba wananchi
kuhudhuria mikutano itakayoitishwa na Tume na kushiriki kikamilifu
katika kutoa maoni yao kwa kuzungumza na pale wanapokosa nafasi ya
kuzungumza, watumie fursa ya kuwasilisha maoni yao kwa maandishi kwa
kutumia fomu maalum zitakazokuwa zinatolewa na Tume katika mikutano
hiyo.
Pamoja na kuwasilisha maoni
kupitia mikutano itakayoitishwa na Tume, wananchi pia wanaweza
kuwasilisha maoni yao kupitia tovuti ya Tume (www.katiba.go.tz) au kwa njia ya posta kupitia anuani za zifuatazo
- Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Makao Makuu, Mtaa wa Ohio, S.L.P. 1681, DAR ES SALAAM, Simu: +255 22 2133425, Nukushi: +255 22 2133442; Au
- Jengo la Ofisi ya Mfuko wa Barabara, Mtaa wa Kikwajuni Gofu, S.L.P. 2775, Zanzibar, Simu: +255 224 2230768, Nukushi: +255 224 2230769
Tume inawaomba wananchi
kuhudhuria mikutano itakayoitishwa na Tume na kushiriki kikamilifu
katika kutoa maoni yao kwa uwazi, uhuru na utulivu.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)