Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amerejea Dar es Salaam mchana wa leo, Jumanne, baada ya kumaliza ziara
ya siku tisa katika mikoa minne ambako amekagua, kuanzisha ama kuzindua
miradi 19 ya maendeleo na kutembea kiasi cha kilomita 2,770.
Rais Kikwete amewasili Dar es Salaam
akitokea Dodoma ambako amefanya ziara ya kikazi ya siku mbili baada ya
kumaliza ziara katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Singida.
Katika Mkoa wa
Kilimanjaro ambako Rais Kikwete alianzia ziara yake Oktoba 28, mwaka
huu, miongoni mwa mambo mengine alikagua nyumba za wahanga wa maporomoko
ya mwaka 2006 kwenye kijiji cha Goha na akafungua Kiwanda cha Kusindika
Tangawizi kilichoko Mamba Miamba, Wilaya ya Same, na akafungua Shule ya
Sekondari ya Kata ya Asha Rose Mingiro iliyoko mjini Mwanga.
Miradi mingine aliyoifungua Rais
Kikwete katika Mkoa wa Kilimanjaro ni uzinduzi wa barabara za Rombo
Mkuu-Tarakea na Kwasadallah-Masama na akafungua Ofisi ya Mkaguzi Mkuu na
Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (NAO) mjini Moshi.
Katika Mkoa wa Arusha, Rais
Kikwete alizindua Hospitali ya Wilaya ya Arusha ya Olturumet, akazindua
Mradi Mkubwa wa Uboreshaji wa Miji kwa kufungua barabara za Jiji la
Arusha, akazindua Jiji la Arusha, akafungua rasmi Chuo Kikuu cha Sayansi
na Teknolojia cha Nelson Mandela na akatembelea Kiwanda cha Nguo cha
A-Z.
Kabla ya kuondoka Mkoani Arusha,
Rais Kikwete alifungua Shule ya Msingi ya Sokoine na kuzindua ukarabati
mkubwa wa Barabara ya Minjingu-Arusha.
Mkoani Manyara, Rais Kikwete
alifungua rasmi Barabara ya Singida-Minjingu-Arusha, akazindua mradi
mkubwa wa maji wa Mji wa Babati na akaweka jiwe la msingi kwenye ujenzi
wa Barabara ya Babati-Bonga.
Mkoani Singida, Rais Kikwete
alizindua mradi mkubwa wa maji wa Mwankoko kwa ajili ya Mji wa Singida,
akaweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Barabara ya Manyoni-itigi-Chaya
na akafungua Barabara ya Issuna-Manyoni.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
6 Novemba, 2012





No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)