Ndugu zangu,
Asubuhi hii nikitoka kwenye mchakamchaka ( jogging) nilimsikia mchungaji wa kanisa akiwatamkia waumini wake;
Asubuhi hii nikitoka kwenye mchakamchaka ( jogging) nilimsikia mchungaji wa kanisa akiwatamkia waumini wake;
“ Angalieni upepo, nguvu ya
upepo. Duniani upepo unaweza kutingisha miti, ukavunja matawi na hata
ukaangusha miti….!” Sikusimama nikasikiliza alichotaka kusema Mchungaji
yule juu ya upepo na nguvu zake. Lakini, nami nikaanza kutafakari na
kujiuliza; Matatizo yetu wanadamu na hasa sisi Watanzania ni nini?
Nikafikiri, kuwa mara nyingi
Watanzania hatutaki kuyajua matatizo yetu. Tunataka kuyajua ya wenzetu.
Na tukiyajua yetu, hatutaki kuyaweka wazi. Tu mahodari wa kusiliba
matatizo yetu. Nje hayaonekani, yamesilibiwa, lakini, ndani hali iko
vile vile.
Tuliokaa vijijini tunajua, kuwa
nyumba ya kijijini haijakamilika bila kuwa na mtungi. Afrika hakuna tu
siri ya mtungi, kuna falsafa ya mtungi pia. Ninapoingia kwenye nyumba
kijijini huangalia kwanza ulipo mtungi.
Kwenye mtungi yawezekana ndimo
yalimo maji ya kunywa. Na ukiinamia mtungi wa maji, usiaangalie sana,
chota maji yako, kunywa. Lakini, mtungi pia hutumika kuhifadhia vyakula;
iwe unga au maharage. Mara nyingi mtungi huwekwa kwenye kona ya chumba.
Na mtungi ukikaa sana, basi, siku ukiinuliwa, hutaacha alama.
Na unafanyaje basi mtungi wa
maji unapoonyesha kuwa na nyufa, kuwa maji yameanza kuvuja? Kuna mawili;
la kwanza si la busara sana. Ni jawabu la muda mfupi, la pili ni la
busara zaidi, ni suluhisho la muda mrefu.
Afrika mtungi wenye nyufa unaweza
kuzibwa kwa kusaga vipande vya mtungi wa zamani, kisha ukachanganya na
nta. Baada ya hapo utasiliba kwenye nyufa za mtungi. Hiyo ni njia ya
kwanza, ni suluhisho la muda mfupi.
Maana, tabu inakuja, siku mtungi
utakapohitajika kuchemshia ‘ komba’- togwa la pombe. Basi, kwenye moto
mkali wa kuni nyufa zile, pamoja na kusilibwa na nta, hazitahimili nguvu
ya moto. Mtungi utamegeka vipande vipande. ‘ Komba’, ama togwa la pombe
litamwagika.
Naam, dawa ya mtungi wenye nyufa
si kusiliba kwa nta, ni kufinyanga mtungi mpya, basi. Na jamii yetu
imekuwa ni kama ya ‘ Super- glo’, ile gundi inayoaminiwa inaweza
kusiliba , ama kuunga chochote kile. Kila jambo tunakimbilia kuitafuta ‘
Super-glo’. Kama nta, Super-glo nayo haihimili kwa muda mrefu joto la
moto, au hata la jua.
Wanadamu tuwe na ujasiri wa
kuyatambua matatizo yetu kama yalivyo. Tusiwe wepesi wa kukimbilia ‘
kusiliba’ kwa nta ua super-glo. Mengine ni ya kuyafanyia mabadiliko ya
jumla.
Natamani nikutane na Mchungaji
yule wa Kanisa, aniambie, kuwa kwake alikuwa na maana gani aliposema
kuwa upepo ni tatizo. Tafakari.
Maggid Mjengwa,
Iringa.
0788 111 765
http://mjengwablog.com
0788 111 765
http://mjengwablog.com
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)