Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akisalimiana na
Waziri wa Afya Juma Duni Haji mara baada ya kuwasili katika bohari kuu
ya madawa Maruhubi kuanza ziara yake ya kutembelea taasisi zilizo chini
ya Wizara hiyo
Mfamasia
Mkuu Dr. Habib Ali Sharif akitoa maelezo kuhusiana na hali ya
upatikanaji wa dawa Zanzibar, wakati wa ziara ya Makamu wa Kwanza wa
Rais Maalim Seif Sharif Hamad kwenye bohari hiyo. Katikati ni Mkurugenzi
wa bohari hiyo Mayasa Salum Ali.
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akitembelea
bohari kuu ya madawa Zanzibar huko Maruhubi wakati wa ziara yake katika
taasisi za Wizara ya Afya.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na watendaji wa kitengo cha malaria Mwanakwerekwe wakati
wa ziara yake katika kitengo hicho. Kushoto ni msaidizi meneja wa
kitengo cha Malaria Zanzibar Bw. Mwinyi Msellem.Picha Salmin Said-Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais
---
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema Zanzibar
inahitaji kujipanga ili kulinda mafanikio yaliyopatikana kutokana na
mradi wa kutokomeza malaria Zanzibar.
Amesema mafanikio yalipatikana yameiletea sifa kubwa Zanzibar, hali inayopelekea kuigwa na nchi nyengine duniani.
Maalim
Seif ameeleza hayo katika kitengo cha kudhibiti malaria Zanzibar huko
Mwanakwerekwe, akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kutembelea
taasisi zilizo chini ya Wizara ya Afya kwa upande wa Unguja.
Amesema
mafanikio hayo yanapaswa kulindwa na kuhakikisha kuwa malengo
yaliyotarajiwa ya kuifanya Zanzibar bila ya kuwa na Malaria yanafikiwa
kwa wakati.
“Nataka
hapa tulipofika tusirudi nyuma, serikali kwa upande wake itajitahidi
kuweka mikakati ili kuona kuona kuwa tunasonga mbele hadi kutimiza
malengo yetu”, alisistiza Maalim Seif.
Kwa
upande wake msaidizi meneja wa kitengo cha Malaria Zanzibar Bw. Mwinyi
Msellem amesema Zanzibar imepata mafanikio makubwa ya kupambana na
malaria katika kipindi cha miaka kumi iliyopita ambapo kwa sasa ugonjwa
huo upo chini ya asilimia moja kutoka asilimia 45 mwaka 2001.
Amesema
mafanikio hayo yamepatikana kutokana na mchango mkubwa wa washirika wa
maendeleo, pamoja na mipango imara ya taasisi hiyo ikiwemo ugawaji wa
vyandarua vyenye dawa, utiaji wa dawa za kuulia mbu wa malaria majumbani
pamoja kufuatilia kwa karibu wagonjwa wanaougua malaria ili kuwapatia
matibabu yanayostahiki.
Hata
hivyo ameishauri serikali kuweka mikakati imara ikiwa ni pamoja na
kutenga bajeti kwa ajili ya mradi huo ili kuweza kuundeleza wakati
wafadhili watakapoamua kuondoka.
“Hivi
sasa baadhi ya wahisani wetu tayari wameanza kupunguza misaada yao
kwetu, wengi wao wakidai kuwa tayari tumepiga hatua na misaada hiyo
wanaielekeza kwengine, lakini hapa ni lazima tuwe makini vyenginevyo
hali inaweza kujirejea kama ilivyokuwa mwaka
2001”,alitanabahisha Msellem.
Akiwa
katika Bohari kuu ya madawa Zanzibar huko Maruhubi, Makamu wa Kwanza wa
Rais ameelezea kufarijika kwake kutokana na mfumo wa kisasa unaotumika
wa uhifadhi na utoaji wa dawa, sambamba na usambazaji wake katika vituo
vya afya Unguja na Pemba.
Amesema
mfumo huo wa kutumia teknolojia ya kisasa ya kompyuta utarahisisha
mawasiliano baina Wizara na vituo vya afya, pamoja na kuweza kudhibiti
ubadhirifu wa dawa unaodaiwa kufanywa na baadhi ya watendaji wasio
waaminifu.
Amewataka
watendaji wa ofisi hiyo kuwa makini katika utunzaji wa mitambo
iliyowekwa, na kutoa wito wa kuwepo utaratibu wa mafunzo kwa watendaji
ili waweze kuitunza mitambo hiyo na kuweza kudumu kwa muda mrefu.
Jumla
ya dola za kimarekani milioni moja nukta mbili (1.2million USD)
zimetumika kwa ajili ya matengezo ya jengo hilo la bohari kuu na uwekaji
wa mitambo na vitendea kazi vyengine.
Akizungumza
katika ziara hiyo Mfamasia mkuu wa serikali Dr. Habib Ali Sharif
amesema dawa zinaweza kuhifadhiwa katika bohari hiyo kwa kipindi cha
miezi sita, na wamekuwa wakitumia mfumo wa kupokea maombi kutoka vituo
vya afya kwa ajili ya usambazaji wa dawa.
Amesema
mfumo huo unatumika ili kuweza kutoa dawa kulingana na mahitaji,
sambamba na kudhibiti matumizi mabaya ya dawa kutoka kwa baadhi ya
watendaji kwenye vituo vya afya.
Hata
hivyo amesema bohari hiyo inakabiliwa na tatizo la usafiri ambalo
huzorotesha ufuatiliaji wake katika maeneo waliyopanga kufanya hivyo.
Katika
bodi ya chakula, dawa na vipodozi, Makamu wa Kwanza wa Rais amewataka
wananchi kutoa ushirikiano kwa bodi hiyo ili iweze kufanya kazi zake
vizuri zenye lengo la kutunza afya ya jamii.
“Hii
bodi inafanya kazi kwa ajili ya kulinda afya zetu, ni vizuri basi kuipa
mashirikiano ili kuweza kuwadhibiti wafanyabiashara wanaoweza
kuhatarisha afya zetu kutokana na kuingiza na kusambaza bidhaa zisizofaa
kwa matumizi ya binadamu”,alitahadharisha Maalim Seif.
Kwa
upande wake mrajis wa bodi hiyo Dr. Burhani Othman Simai amesema baadhi
ya wafanyabiashara wasio waaminifu wamekuwa wakiingiza bidhaa
zilizopitwa na wakati pamoja na kubadilisha tarehe za kumaliza muda,
hali ambayo ni hatari kwa afya ya jamii.
Dr.
Simai ametaja baadhi ya changamoto zinazoikabili bodi hiyo kuwa ni
pamoja na kuwpo bandari zisizo rasmi, upungufu wa wataalamu pamoja na
uelewa mdogo wa jamii juu ya kazi zinazofanywa na bodi hiyo.
Ziara
hiyo pia imewashirikisha watendaji wakuu wa Wizara ya Afya wakiwemo
Waziri wa wizara hiyo Mhe. Juma Duni Haji na Katibu Mkuu Dr. Mohammed
Saleh Jidawi.
Na
Hassan Hamad
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)