Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa
Nchini (TPBC) inapenda kuueleza umma kuwa taarifa zinazotolewa na
kikundi kinachoongozwa na Chaurembo Palasa za kuitisha mkutano wa
kuhakiki wanachama ni potofu kwani wanachama wa TPBC ni Kamisheni za
mikoa na haina wanachama mmoja mmoja katika ngazi ya taifa. Katiba ya
TPBC iliyotoka mwaka 2001 imetamka wazi kuwa wanachama wa TPBC ni
Kamisheni za Mikoa.
Hakuna mwanachama wa TPBC
anayeitwa Chaurembo Palasa. Kadi ya uanachana anayoitembeza kwenye
mitandao ni ya zamani kabla ya katiba ya TPBC kubadilika na kufuta
uanachama wake.
Yeye mwenyewe alishiriki kama
mwanachama wa kutoa maamuzi ya kikao kilichofuta uanachama wake kwani
ilionekana kuwa mabondia wanatumika kuleta fujo kama anavyotumika yeye
hivi sasa. Bwana Chaurembo Palasa anakaribishwa kuleta maoni yake
kuhusu namna ya kuboresha shughuli za TPBC kama alivyojitokeza na kwenda
kulipa ada (japokuwa waliingilia jambo lisilowahusu). Yeye na kikundi
chake wanaendelea kuchukua marejesho (refund) ya pesa hizo kila mwezi
kutoka kwa Mweka Hazina wa TPBC bwana Boniface Wambura.
Chaurembo na kikundi chake
kinachoongozwa na kiongozi mmoja wa chama cha ngumi za kulipwa na ambaye
ameamua kuleta fujo ili kufifisha juhudi za TPBC za kuleta maendeleo ya
ngumi nchini wanataka kuturudisha kwenye migogoro isiyoisha ya miaka ya
80 na 90 ambayo ilitawala tasnia ya ngumi Tanzania.
Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa
Nchini (TPBC) imepanga kuanza kufanya uchaguzi tarehe 31 March 2013
kuchagua viongozi wapya watakaoiongoza Kamisheni hiyo.
Uchaguzi huo utaanzia ngazi za
mikoa kwa kuchagua Makamishna wa mikoa pamoja na Kamati za Utendaji.
Kilele cha uchaguzi huo kitakuwa ngazi ya taifa ambako viongozi wakuu
kuanzia Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Mweka Hazina na wajumbe wa Kamati
ya Utendaji watachaguliwa. Nafasi ya Urais ni ya heshima ambapo
atateuliwa na Kamati ya Utendaji pamoja ya ile ya Katibu Mtendaji ambayo
ni ya kuajiriwa!
Rais wa sasa Onesmo Alfred McBride Ngowi hatatetea tena kiti chake baada ya kuiongoza TPBC kwa takribani miaka kumi (10)!
Ngowi amewataka watanzania walio
na uwezo pamoja na nia ya kuiongoza Kamisheni hiyo wajitokeze ili waweze
kugombea nafasi za uongozi. Ngumi za Kulipwa zimekuwa ni ajira na ni
vyema tukapata viongozi wazuri wa kuiongoza TPBC ili waweze kutoa nafasi
za ajira kwa vijana!
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)