Mbunge wa Jimbo la Ubungo-CHADEMA,John Mnyika
--
Baada ya habari kutolewa juu ya uamuzi wa Spika kuhusu
tuhuma kwamba baadhi wa wabunge na wajumbe wa kamati ya Nishati na
Madini walijihusisha na vitendo vya rushwa katika kutekeleza kazi zao za
kibunge, nimeulizwa na baadhi ya wanahabari na wananchi kwa simu na
kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii sababu za kusimama bungeni tarehe 9
Novemba 2012 mara baada ya Spika kutoa uamuzi huo na kutaka kuomba
muongozo.
Nalazimika kutoa ufafanuzi huu nje ya bunge baada ya mkutano wa bunge
kuahirishwa bila Spika kunipa fursa ya kusema jambo hili bungeni kwamba
nilitaka muongozo wake kwa mujibu wa Kanuni ya 5(1) na 5 (2) kuwa
nakusudia kukata rufaa dhidi ya uamuzi wake kutokana na kuwa na maudhui
kadhaa yasiyozingatia katiba ya nchi, sheria mbalimbali za nchi, kanuni
za kudumu za bunge, maamuzi ya awali ya maspika wa Bunge pamoja na mila
na desturi za mabunge mengine yenye utaratibu wa kibunge unaofanana na
utaratibu wa bunge letu.
Hata hivyo kwa kuzingatia kuwa rufaa huchukua muda kusikilizwa
nilitaka niombe muongozo wake kabla ya Mkutano wa Bunge kuahirishwa kwa
kuwa katika uamuzi wake hakueleza hatma ya Kamati ya Nishati na Madini
ilivyovunjwa, hivyo Spika anapaswa bado kueleza kwa umma iwapo kamati
hiyo inarejeshwa au inaundwa kamati nyingine au kuelekeza kamati
nyingine ya kudumu ya Bunge inayopaswa kuisimamia Serikali wakati huu
ambapo nchi inakabiliwa na matatizo mengi kwenye sekta za nishati na
madini yenye athari kwa maisha ya wananchi wakiwemo wa Jimbo la Ubungo.
Kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini nasisitiza
kwamba Spika anapaswa kurejea barua yangu ya toka mapema Oktoba ambayo
mpaka sasa haijapatiwa majibu, hoja niliyoiwasilisha bungeni na kuungwa
mkono ya jambo lililohusu haki za bunge na miongozo niliyoomba bungeni
kuhusu masuala ya nishati kwa nyakati mbalimbali katika mkutano wa Bunge
uliomalizika na kutoa kauli kwa umma.
Kwa kuwa katika uamuzi wake Spika wa Bunge ameeleza kwamba Waziri wa
Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wake Eliackim
Maswi wametoa maelezo yasiyokuwa kweli kwa nyakati mbalimbali uwepo wa
kamati ya bunge kwa ajili ya kuisimamia Wizara hiyo kwa niaba ya bunge
ni suala linalohitaji uamuzi wa haraka.
Aidha, katika uamuzi wake Spika zaidi ya kutoa onyo kali kwa Katibu
Mkuu na Wabunge hakutoa onyo kwa Waziri wa Nishati na Madini wala
hakueleza chochote iwapo alipokea ushauri kutoka kwa Kamati Ndogo ya
Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuhusu ukiukwaji wa kanuni uliofanywa
na Spika mwenyewe bungeni wakati wa kadhia nzima.
Kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Spika anaweza kutoa taarifa bungeni
wakati wowote na taarifa yake haijadiliwi hivyo sehemu kubwa ya taarifa
ya tarehe 9 Novemba 2012 ilikuwa ni maelezo kuanzia sehemu ya kwanza
mpaka sehemu ya pili.
Uamuzi wa Spika unapatikana sehemu ya tatu ya maelekezo hususan
kifungu cha 6.12 ya kwamba “tuhuma husika hazikuweza kuthibitishwa” na
baadaye kufuatiwa na uamuzi wa Spika kuhusu watoa tuhuma katika
vipengele (a), (b), (c) na (d).
Nakusudia kukata rufaa ili taarifa kamili ya Kamati Ndogo ya Haki,
Maadili na Madaraka ya Bunge iweze kuwasilishwa kwa ukamilifu wake
kwenye kamati husika ya kudumu ya Bunge na hatimaye taarifa kamili
kuwasilishwa na kujadiliwa bungeni ili ‘mbivu na mbovu’ zijulikane na
masuala yanayohitaji kufanyiwa uchunguzi wa ziada na vyombo vingine vya
nje ya Bunge yaendelee kwa hatua zaidi badala ya uamuzi huu wa ‘funika
kombe’.
Yapo masuala ya ziada ambayo binafsi niliyaeleza mbele ya kamati
ndogo chini ya kiapo ambayo sitakiwi kuyaeleza nje ya bunge kwa mujibu
wa kanuni na sheria husika , hata hivyo taarifa kamili ikiingia bungeni
kutakuwa na uhuru wa majadiliano kwa mujibu Kwa Ibara ya 100 ya Katiba
ya Nchi.
Aidha, nitaka rufaa kwa kuwa kiwango cha ‘adhabu’ kilichotolewa
kwenye uamuzi wa Spika hakilingani na ‘makosa’ ambayo yameelezwa kuwa na
uzito wenye kuathiri “kwa kiasi kikubwa hadhi ya Bunge kama taasisi na
heshima ya wabunge waliohusishwa”.
Spika amefanya uamuzi wake chini ya Kanuni ya 5(1) na 72 (1) lakini
hakuzingatia kuwa kanuni ya 72 (3) inaeleza kuwa iwapo mbunge ameshindwa
kuthibitisha ukweli Spika amepewa fursa ya kumsimamisha mbunge huyo
kuhudhuria vikao vya Bunge visivyozidi vitano.
Aidha nitakata rufaa kwa kuwa waliodaiwa kutoa kutoa tuhuma bila
ushahidi walipaswa kujieleza kwa tuhuma hizo kabla ya kuhukumiwa kwa
misingi ya kanuni za haki ya asili zilizopo pia katika katiba ya Nchi na
kwa kuzingatia matakwa ya kanuni za kudumu za Bunge; hata hivyo Spika
amefikia uamuzi wa moja kwa moja wa kutoa adhabu ya ‘onyo kali’ kinyume
na masharti ya kanuni ya 5 (1).
Ikumbukwe kwamba Spika katika maelezo yake amesisitiza kuwa Kamati
Ndogo ilipewa hadidu rejea moja tu, “Kuchunguza na kumshauri Spika iwapo
tuhuma kwa baadhi ya wabunge na wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini
kujihusisha na vitendo vya rushwa ni za kweli au hapana”, baada ya
kuchunguza kwa mujibu wa hadidu rejea hiyo na kuwasilisha ripoti yake
Spika alipaswa kama kuna ukiukwaji mpya wa kanuni uliobainika kutokana
na uchunguzi huo kuanzisha mchakato wa adhabu.
Binafsi niliitwa kwa maandishi kuisaidia kamati ndogo katika
uchunguzi wake kutokana na maoni niliyowasilisha bungeni ya kwamba
“….Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inafahamu kwamba kuna kampeni kubwa
inafanywa ndani na nje ya Bunge ili uamuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya
Nishati ubatilishwe kwa maslahi ya Makampuni yaliyokosa zabuni kuiuzia
TANESCO mafuta ya kuendesha mitambo ya kufua umeme…”.
Sijawahi kuandikiwa au kuitwa popote kutakiwa kujieleza kwa ‘kuisemea
tuhuma bungeni bila ya kufanya utafiti kupata ukweli’ na maelezo hayo
niliyoyatoa bungeni hayakukiuka kanuni yoyote ya bunge kama ambavyo
nitathibitisha wakati nitakapokata rufaa.
Kwa upande mwingine nitakata rufaa kwa kuwa adhabu aliyopewa Katibu
Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Eliakim Maswi hailingani na ukubwa
wa makosa anayodaiwa kuyafanya, ikiwa ni kweli amevunja haki za bunge
kwa kuzusha tuhuma za uongo dhidi ya wabunge kwa ajili ya kujihami dhidi
ya baadhi ya wajumbe wa kamati ya Bunge ya Nishati na Madini waliokuwa
wanahoji kuhusu utendaji wa Wizara yake.
Kwa kosa hilo ikiwa maelezo ya Spika kuhusu matokeo ya uchunguzi wa Kamati ni sahihi anapaswa kufunguliwa mashtaka kwa mujibu wa Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge na kupewa adhabu ya zaidi ya onyo ikiwemo hata faini au kifungo au walau kutakiwa kuwajibika.
Kwa kosa hilo ikiwa maelezo ya Spika kuhusu matokeo ya uchunguzi wa Kamati ni sahihi anapaswa kufunguliwa mashtaka kwa mujibu wa Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge na kupewa adhabu ya zaidi ya onyo ikiwemo hata faini au kifungo au walau kutakiwa kuwajibika.
Kadhalika kwa Spika ameeleza kuwa mbinu aliyotumia ni pamoja na
kutaka kuwalipa fedha wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini
shilingi milioni mbili kwa kila mjumbe madai haya ni ya jaribio la
kufanya ufisadi wa fedha na matumizi mabaya ya madaraka kama ilivyokuwa
kwenye kashfa ya Katibu Mkuu aliyemtangulia David Jairo hivyo Spika
alipaswa kupendekeza kwa mamlaka ya uteuzi wake kuchukua hatua za
kinidhamu na kisheria.
Uamuzi wa Spika ‘kufunika kombe’ hauna tofauti na maamuzi
yaliyotangulia ambayo yamesababisha mpaka sasa Serikali haijawasilisha
bungeni ripoti ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge kufuatia uchunguzi
uliofanywa na kamati teule ya Bunge.
Ni vizuri ikakumbukwa kwamba katika hotuba yangu bungeni kwa niaba ya
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni tarehe 27 Julai 2012 nilisisitiza
kwamba “ili ukweli wa kina uweze kujulikana Kambi Rasmi ya Upinzani
inapendekeza kuwa bunge liazimie kuunda Kamati Teule ya Bunge kuchunguza
masuala yote ya ukiukwaji wa sheria, matumizi mabaya ya madaraka na
tuhuma za ufisadi katika utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme na
ununuzi wa mafuta wa ajili ya mitambo ya umeme.
Uchunguzi huo uhusishe pia mkaguzi mkuu kufanya ukaguzi wa
kiuchunguzi (Forensic Audit) kwa malipo yaliyofanywa na makampuni ya BP
(Sasa PUMA Energy), Oryx na Camel Oil ili kubaini iwapo kuna vigogo
zaidi wa serikali waliojinufaisha kwa kisingizio cha dharura ya umeme.
Izingatiwe kwamba masharti ya ibara ya 27(2) ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania inamtaka kila mtu “… kutunza vizuri mali ya Mamlaka ya Nchi na ya pamoja (na) kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhirifu….”.
Mchakato huu ungewezesha kupata ukweli wa ziada kibunge kuliko utaratibu uliotumiwa na Kamati Ndogo na Spika.
Nitaeleza masuala ya ziada nitakayoyakatia rufaa na kauli yangu
kuhusu maelezo na uamuzi wa Spika juu ya Waziri na Waziri Kivuli wa
Nishati na Madini.
John Mnyika (Mb)
10/11/2012
10/11/2012
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)