Mhe.
Bernard K. Membe (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa akisaini kitabu cha wageni leo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Mbeya, wakati akiwa katika ziara ya siku mbili Mkoani humo.
Mhe.
Waziri Membe akifafanua kuhusu mgogoro wa Mpaka wa Ziwa Nyasa kati ya
Tanzania na Malawi mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama chini ya
Uenyekiti wa Mhe. Abbas Kandoro, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.
Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Mhe. M. Malenga akimkaribisha Mhe. Waziri Membe (wa pili kulia), wakati
alipotembelea Ofisini yake Wilayani Kyela. Mhe. Membe yupo Mkoani
Mbeya kwa ziara ya siku mbili ambapo atatembelea na kuzungumza na
wananchi waishio katika maeneo yaliyopo kando ya Ziwa Nyasa.
Balozi Irene Kasyanju (wa pili kushoto), Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria kwenye Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Balozi Dkt. Mohamed Maundi (kushoto), Mkurugenzi wa Chuo cha Diplomasia - Kurasini wakisikiliza maelezo ya Mhe. Malenga kuhusu Wilaya ya Kyela.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoani Mbeya wakimsikiliza kwa makini Mhe. Waziri Membe (hayupo pichani).
Mkuu wa
Wilaya ya Kyela akiuongoza msafara wa Waziri Membe kuelekea kwenye
mpaka wa Mto Songwe uliopo kati ya Tanzania na Malawi.
Waziri
Membe akiangalia Mto Songwe, huku akitafakari mpaka kwa vile hapo
aliposimama kwa ufupi ni nchini Malawi ambapo wananchi wa nchi zote
mbili upishana wakiwa katika shughuli zao za kawaida (angalia alama ya tundu lililoko chini ya fensi - kulia).
Mhe. Waziri Membe akiongea na Wajumbe wa msafara wake akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Abbas Kandoro (mwenye shati jeupe mbele ya Waziri), Balozi Irene Kasyanju (wa pili kushoto), Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria kwenye Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Balozi Dkt. Mohamed Maundi (kushoto), Mkurugenzi wa Chuo cha Diplomasia - Kurasini.Picha hii na Mbaraka Islam
Mhe. Waziri Membe na msafara wake wakiwa wamesimama kwenye mpaka wa Mto Songwe.
Mhe. Waziri Membe akisalimiana na mmoja wa Machifu kutoka Malawi, Bw. Clement Kyungu Mwakasungura ambaye alikutana naye Kasumulu, Wilayani Kyela - Mkoani Mbeya.
Mhe.
Bernard K. Membe (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa akiongea na wazee waishio Katumbasongwe, kando ya Ziwa Nyasa
ndani ya Wilayani Kyela, Mkoani Mbeya.
Waziri
Membe akiongea na wakazi wa Matema, Wilayani Kyela ambapo aliwasihi
waendelee na shughuli zao za kujiletea maendeleo. Aidha, Mhe. Membe
alisema Serikali inajitahidi kadri iwezavyo kutafuta suluhisho la
mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa kati ya Tanzania na Malawi.
Wazee
wa Katumbasongwe wakinyoosha mikono kujitambulisha umri wao wakati wa
Mkutano wao na Waziri Membe uliofanyika jana Wilayani Kyela, Mkoani
Mbeya. Wazee walio weka mikono juu wana umri kati ya miaka 60 hadi 85.
Waziri Membe alikuwa Mkoani humo kwa ziara ya siku mbili ambapo
alitembelea maeneo na makazi ya wananchi waishio ufukweni mwa Ziwa
Nyasa.
Wakazi wa Katumbasongwe walimiminika kwa wingi kumsikiliza Mhe. Membe.
Waziri Membe (hayupo pichani) pia
alipata fursa ya kuongea na wazee wa Matema ikiwa ni sehemu ya mwisho
wa ziara yake ya siku mbili Mkoani Mbeya. Katika mazungumzo yake na
wazee hao, Waziri Membe aliwaeleza kuwa ziara hii ni sehemu ya kukusanya
ushahidi muhimu kutokana na maelezo ya historia watakazochangia hususan
tangu enzi ya ukoloni kuhusu Ziwa Nyasa.
Wakazi wa Matema, waishio katika ufukwe wa Ziwa Nyasa, Wilayani Kyela wakimsikiliza Waziri Membe alipowatembelea jana.
Makazi ya wananchi wa Malawi kando ya Mto Songwe ambapo mmoja wa wananchi anaonekana akifua nguo (pichani - upande wa kushoto ambao ni ng'ando ya mpaka kwa upande wa Malawi) wakati wengine (kulia) wanaonekana
wakiendelea na shughuli zao za kawaida huku wakiwa tayari ng'ando ya
mpaka kwa upande wa Tanzania.Picha Zote na Daisy Mwakawago-Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
---
“Hakuna
mtu kusema Ziwa lote ni lake,” alisema Waziri Bernard K. Membe (Mb),
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na kuongeza kuwa
lazima kuwe na dhamana inayoonesha mipaka, kanuni na sheria ili kuondoa
wingu la shaka yoyote hususan kwa Taifa lolote na wananchi wake.
Aidha,
Waziri Membe aliongeza kuwa Serikali ina jukumu la kumaliza mgogoro wa
mpaka wa Ziwa Nyasa kati yake na Malawi, na jitihada muhimu zinafanyika
ili kuumaliza kwa amani na utulivu.
Waziri
Membe aliyasema hayo jana mjini Mbeya alipokuwa akizungumza na Kamati
ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mbeya, ambayo hiko chini ya Uenyekiti wa
Mhe. Abbas Kandoro, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.
Akiainisha
jitihada hizo, Mhe. Membe alisema kuwa Kamati ya Taifa inayojumuisha
timu ya wanasheria na wataalamu wa mipaka imeundwa kwa madhumuni ya
kutatua mgogoro huo na timu ya Malawi. Pia
kuna timu ya Kikosi Kazi chini ya Waziri Membe, ambayo jukumu lake ni
kukusanya nyaraka na kumbukumbu muhimu za mgogoro huo tangu miaka ya
1890 hadi leo.
Kwa
mujibu wa maelezo ya Waziri, baada ya Kikosi Kazi kumaliza kazi yake,
kitawasilisha rasmi nyaraka kwa Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete na kwa
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili hatua muhimu za Serikali zifanyiwe
kazi.
Aidha,
Mhe. Waziri alisema kuwa kuna umuhimu wa kutumia vyombo vingine ili
kusaidia kutatua tatizo hili kama vile Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za
Kusini mwa Afrika (SADC), Baraza la Uongozi wa Wakuu wa Afrika la SADC
(Leadership Forum - SADC), Umoja wa Afrika (AU) na ikiwezekana kuipeleka
kesi kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ).
Kwa upande wake, Mhe. Kandoro alisema kuwa hali Mkoani Mbeya ni tulivu na kwamba maisha yanaendelea vizuri. Alikanusha
kuhusu taarifa zisizo za kweli zilizotangazwa kwenye mitandao kwamba
mabomu yamerushwa Mkoani Mbeya hususan kwenye maeneo ya mpaka wa Ziwa
Nyasa.
Aidha,
Mkuu wa Mkoa aligusia ukamatwaji wa wavuvi na mitumbwi kutoka Malawi
ambayo ilikuja ufukweni mwa Tanzania, na kusisitiza kuwa hatua muhimu
zilichukuliwa kwa kuzingatia na kuheshimu ujirani mwema.
Katika
ziara yake, Waziri Membe pia alitembelea Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya
Kyela, Bibi Margareth Malenga, ambapo alipata taarifa kuhusu hali ya
ulinzi na usalama katika mipaka ya Ziwa Nyasa, pamoja na mahusiano kati
ya Wilaya ya Kyela na Wilaya ya Karonga nchini Malawi. Wilaya ya Kyela
iko mpakani mwa Wilaya ya Karonga nchini Malawi.
Akisoma
taarifa ya Wilaya yake, Bibi Malenga alisema “hali ya mipaka ni tulivu
na kueleza kuwa hivi karibuni, mnamo tarehe 11 Oktoba, 2012 walipata
ugeni wa Mhe. Mganda Chiume, Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi na ujumbe
wake akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Karonga nchini humo.”
Kwa
mujibu wa Bibi Malenga, lengo la ziara ya Waziri Chiume lilikuwa ni
kukagua mpaka wa Ziwa Nyasa kwa upande wao lakini waliona ni vizuri waje
Wilayani Kyela kuona hali ya mahusiano ilivyo baina ya wananchi wa
upande wa Kyela na wale wa Karonga.
Akiendelea
na ziara yake, Waziri Membe pia alipata fursa ya kuongea na wazee
alipotembelea maeneo ya Katumbasongwe na Matema yaliyopo katika ufukwe
wa Ziwa Nyasa.
“Tumekuja
hapa kupata ushahidi wenu wa kihistoria tangu enzi ya ukoloni ambao
utazisaidia Kamati zilizoteuliwa kutatua mgogoro huu ili ziweze
kukusanya kumbukumbu na kufanya kazi ipasavyo,” alisema Waziri Membe.
Aidha,
Waziri Membe aliwahakikishia amani na utulivu wananchi wa Kyela, na
kusema kuwa “Serikali inajitahidi kadri iwezavyo kutatua mgogoro huu kwa
njia ya kidiplomasia na hata kama ikiwezekana kwenda ICJ.”
Kabla
ya kumaliza ziara yake ya siku mbili jana Mkoani Mbeya,
Mhe. Membe alitembelea Kasumulu ambapo mpaka wa Mto Songwe hupo, ikiwa
ni pamoja na Katumbasongwe na Matema kwenye ufukwe wa Ziwa Nyasa ambapo
alizungumza kwa kina na wakazi waishio ufukweni mwa Ziwa hilo.
Na
TAGIE DAISY MWAKAWAGO,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
30 Oktoba, 2012
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)