Shirika la HakiElimu limezindua kampeni ambayo imepewa jina la “Boresha Elimu ya Chekechea”.
Lengo la kampeni hii ni kuitaka Serikali itimize ahadi na wajibu wake
wa kutoa elimu bora kwa wanafunzi wote wa elimu ya awali ambayo ni
muhimu sana katika kujenga msingi imara kielimu. Ni ukweli usiopingika
kuwa elimu ya awali itolewapo kikamilifu, huwa ni msingi imara kwa
mtoto katika elimu yake ya baadae.
Elimu ya Awali ni muhimu kwa maendeleo ya mtoto kimwili, kiakili na
kimaadili. Katika Sera ya Elimu na mafunzo ya mwaka 1995 Serikali
inaonesha umuhimu wa elimu ya awali,inapotamka ; “Tafiti kadhaa
zilizofanyika nchini katika miaka ya 1980 zilibaini kuwa watoto
waliopitia elimu ya awali huwa na mafanikio makubwa zaidi wanapoanza
darasa la kwanza. Kutokana na kutambua umuhimu huu, Serikali iliamua
kuingiza Elimu ya Awali kwa watoto wenye umri wa miaka 5 na 6 kwenye
mfumo rasmi wa elimu na kila shule ya msingi inapaswa kuwa na madarasa
ya Elimu ya Awali.” Sera ya Elimu na Mafunzo 2010. Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi . Toleo jipya Rasimu ya 2 March 2011.(uk 5-6).
Uwekezaji katika huduma bora kwa mtoto na elimu ya awali huwa na
faida maradufu kwa watoto wetu- ambao ni raia wetu wa baadaye. Walipa
kodi nao pia hufaidika na huimarisha uchumi. Faida ya uwekezaji wa fedha
za umma katika elimu bora ya awali ni kubwa sana. Lakini je, Tanzania
imeligundua hili na kulitekeleza kikamilifu? Na je, maneno haya ambayo
sera inasisitiza yako yanatekelezwa kwa vitendo?
Baada ya kufanya tafiti katika sehemu mbalimbali nchini HakiElimu
inasikitishwa na jinsi ambavyo elimu ya awali inavyotolewa katika
mazingira yasiyofaa hali inayochangia kushuka kwa kiwango cha elimu
nchini. Kama ilivyo katika elimu ya msingi na ile ya sekondari , elimu
ya awali imegubikwa na changamoto nyingi. Baadhi ya changamoto hizi ni
upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa, unaosababisha mrundikano mkubwa
katika madarasa, ukosefu mkubwa wa walimu wenye taaluma ya elimu ya
awali pamoja na vifaa vya kufundishia. Aidha, kutokuwepo na tofauti ya
kimadarasa katika elimu ya awali ( yaani watoto wa umri wa miaka 5 na
miaka 6 kusoma katika darasa moja, na wingi wa masomo pia ni changamoto.
Akiwasilisha Bungeni makadirio na matumizi ya wizara yake kwa mwaka
2012/2013, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi , Dkt Shukuru Kawambwa,
alisema Serikali ilitoa mwongozo unaoelekeza kila shule ya Msingi
kufanya Serikali imeelekeza yafuatayo katika sekta ya elimu nchini
kuhusiana na Elimu ya Awali:
(i) Kuhakisha kuwa kila shule ya msingi ina darasa la Elimu ya
Awali, lenye madawati yanayolingana na hali ya watoto wa elimu hiyo,
(ii) Kujenga vyoo kwa ajili ya watoto wa Elimu ya Awali wasiingiliane na wale wa shule za msingi.
(iii) Kuandaa waalimu wengi wa Elimu ya Awali na kuwapanga katika shule zinazohusika
Katika kutekeleza maagizo hayo Serikali ilitoa mwongozo unaoelekeza
kila shule ya msingi kuwa na darasa la Elimu ya Awali. Pia wizara
iliahidi kushirikiana na Halmashauri ili kuhakikisha kuwa Elimu ya Awali
inapata rasilimali stahiki kama inavyoelekezwa katika MMEM II, ikiwa ni
pamoja na upatikanaji wa walimu na vifaa vya kufundishia na kujifunzia.
Lakini licha ya agizo hilo pamoja na makubaliano mengine yaliyofikiwa
na serikali katika mwaka wa fedha 2012/2013, Serikali haijatenga kiasi
chochote cha fedha kwa ajili ya elimu ya Awali. Hili linatupa wasiwasi
wadau wa elimu kama kweli Serikali ina nia ya dhati kuboresha elimu ya
awali nchini au bado inaendelea kuja na mikakati ambayo haina
utekelezaji.
Baada ya kuona madhara ya kukosa elimu bora ya awali kwa watoto wetu,
HakiElimu inatoa wito kwa watanzania wote nchini wenye mapenzi mema na
maendeleo ya taifa letu kuungana nasi katika kampeni hii kwa njia
zifuatazo;
- Kuhimiza wananchi wote wenye watoto wenye umri wa kuandikishwa shule za awali wafanye hivyo kwa wingi. Kuna baadhi ya sehemu inaripotiwa wazazi bado hawajaelewa umuhimu wa kuwapeleka watoto katika madarasa haya ya awali.
- Kuwabana viongozi wetu tuliowachagua kuanzia mwenyekiti wa mtaa, diwani na Wabunge wetuwanachukua hatua kukabiliana na changamoto zilizopo ili kufanikisha Elimu bora ya Awali kwa watoto wetu.
- Wananchi kuandika barua kwenye magazeti mbalimbali hapa nchini zikielezea hali ya elimu ya awali inavyotolewa katika maeneo mliyopo. Barua hizo mnaweza kuzituma moja kwa moja kwenda kwa Wahariri wa magazeti mnayoyasoma kupitia anuani zilizopo katika gazeti ulipendalo. Vilevile mnaweza kututumia barua hizo kupitia sanduku letu la barua 79401 DSM; zikiwa na kichwa cha habari ‘BORESHA CHEKECHEA’. Sisi tutazipeleka katika magazeti mbalimbali nchini na zitachapishwa na kufikisha ujumbe kwa viongozi wetu.
- Aidha, ili kuchagiza mafanikio katika sekta hii ya elimu, HakiElimu imeandaa vipindi vya radio katika mikoa ya Morogoro, Mbeya, Tabora, Tanga, Kagera, Dodoma na Mara ambavyo vitatoa nafasi ya Marafiki wa Elimu kujadili jinsi gani elimu ya awali inaweza kuboreshwa hapa nchini na nini kifanyike. Katika vipindi hivyo vinavyoendeshwa na Marafiki wa Elimu wananchi wote mnaombwa kupiga simu na kutoa mchango wa nini kifanyike ili kuboresha elimu ya awali nchini.
- Hali kadhalika, kwa watanzania wanaotumia mtandao wa Internet tunawaomba mshiriki kampeni hii kwa kutembelea mtandao wetu wa facebook katika www.facebook.com/hakielimu,mtandao wa twitter unaopatikana kupitia www.twitter.com/hakielimu na blog yetu inayopatikana kupitia www.hakielimu.blogspot.com ambako mtapata fursa ya kuona na kushiriki kutengeneza album kubwa ya kihistoria nchini Tanzania ambayo itabeba ujumbe wa umuhimu wa elimu ya awali na nini kifanyike kuboresha elimu hiyo nchini.
Sambamba na hilo, HakiElimu imezindua matangazo mawili ya radio
na televisheni yatakayokuwa yakiruka katika vituo vya radio na
televisheni takribani 12 nchini Tanzania. Moja ya matangazo hayo
litaonesha changamoto zilizoko katika elimu ya awali nchini na tangazo
la pili litaonesha mfano wa shule bora au elimu ya awali nchini
Tanzania. Tunaomba mtumie dakika zisizozidi 3 kuangalia matangazo
yanayopatikana katika mtandao wetu wa YouTube kupitia
www.youtube.com/hakielimutz
Aksanteni
Imetolewa na
Bi. Elizabeth Missokia
Mkurugenzi Mtendaji – HakiElimu
1 Oktoba, 2012
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)