- YATAFANYIKA TAREHE 24-28 OKTOBA, 2012 JIJINI JOHANNESBURG, AFRIKA KUSINI
-
KUSHIRIKISHA WABUNIFU ZAIDI YA 35 AFRIKA, NI MSHIRIKI PEKEE KUTOKA TANZANIA.
Mbunifu maarufu wa mavazi kutoka
Tanzania, Mustafa Hassanali ndiye Mtanzania pekee katika fani ya mitindo
aliyepewa mualiko wa kushiriki katika maonyesho ya Wiki ya Mitindo Afrika chini
ya African Fashion International (AFI) yatakayofanyika kwa siku nne kuanzia
tarehe 24-28 Oktoba, 2012 katika ukumbi wa Melrose Arch, jijini
Johannesburg, Afrika ya Kusini.
Mashindano hayo yanayodhaminiwa na
kampuni ya kutengeneza Magari ya Mercedes-Benz yanatarajiwa kuwashirikisha
wabunifu wa mavazi zaidi ya 35 kutoka sehemu mbalimbali barani Afrika, baadhi ya
nchi hizo ni wenyeji Afrika ya Kusini, Ivory Coast, Morocco, Msumbiji, Cameroon,
Rwanda, Angola, DRC, Nigeria, Ghana na Tanzania.
“Ni maonyesho ya pekee na yenye
heshima yake barani Afrika na hata duniani kwa ujumla kwani wabunifu walioalikwa
ni wazoefu na bora katika fani ya Mitindo barani Afrika. Hivyo mwaliko wangu si
tu utaweza kutangaza kazi ni nazofanya bali pia utasaidia kutangaza nchi yetu ya
Tanzania kupitia maonyesho haya” Alisema, Mustafa
Hassanali.
“Watakapotaja jina langu pale katika
maonyesho, hawatasema tu huyu ni Mustafa Hassanali, bali watasema huyu ni
Mustafa Hassanali kutoka Tanzania, hivyo itakuwa ni mchango mkubwa kwa nchi yetu
kuweza kuonyesha fursa zilizopo kupitia Ubunifu wa Mitindo. Nimejiandaa vizuri
katika haya maonyesho, nataka kuonyesha nini Tanzania tunacho katika tasnia ya
ubunifu kwa ulimwengu mzima ni imani yangu kufanya vizuri” Aliongeza
Hassanali.
AFI inaandaa mashindano haya ili
kuweza kutangaza kazi za wabunifu wa mavazi kutoka barani Afrika katika soko la
dunia kwani Afrika ina wabunifu wazuri na imara hivyo kujitokeza kwao katika
maonyesho haya kutafungua milango zaidi katika soko la kimataifa na kuongeza
fursa nyingi zitakazoinua uchumi wa bara hili kupitia sanaa ya ubunifu wa
mitindo.
Licha ya kushiriki katika maonyesha
haya, Mustafa Hassanali pia anawaomba Watanzania wote kwa ujumla kuweza kumpigia
kura ya kuwa mwanamitindo bora barani Afrika kupitia tovuti ya
www.awardnomination.afi.za.com na kuweza kuiletea sifa tasnia ya
mitindo nchini Tanzania.
Huu ni mwaka wa tisa kwa Mustafa
Hassanali kupata mwaliko wa kuonyesha ubunifu wake katika maonyesho haya.
Ameshashiriki katika maonyesho zaidi ya nchi 16 katika miji 25 tofauti duniani,
amekuwepo katika kilinge cha sanaa ya mitindo kwa muda mrefu hapa nchini,
amechangia kwa kiasi kikubwa mabadiliko na maendeleo ya kazi za ubunifu wa
mavazi hapa Tanzania.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)