MTOTO ANETHUMIWA KUKOJOLEA QURAN NA WAKAZI 35 WA MBAGALA WAFIKISHWA MAHAKAMANI - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

MTOTO ANETHUMIWA KUKOJOLEA QURAN NA WAKAZI 35 WA MBAGALA WAFIKISHWA MAHAKAMANI

Watuhumiwa wa vurugu za Mbagala wiki iliyopita, wakiwa chini ya ulinzi wa polisi, walipofikishwa mahakama ya hakimu mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kwa mara ya kwanza jana. Watuhumiwa 29, wawili kati yao wanawake, walisomewa mashtaka mbalimbali kuhusiana na vurugu zilizopelekea makanisa kadhaa kuchomwa moto wiki iliyopita, chanzo ikiwa ni baadhi ya watu wanaodaiwa kuwa waislamu, kuandamana wakipinga mtoto mmoja kukojolea Quraan tukufu. Dhamana ya watu hao itaamuliwa Oktoba 30.
.........................................
Mtoto anayetuhumiwa kukojolea Quran Tukufu pamoja na wakaazi 35 wa Mbagala, Dar es Salaam, wanaodaiwa kuchoma makanisa na kuharibu magari za Serikali wamefikishwa kizimbani  leo  katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu chini ya ulinzi mkali wa Polisi.
Mtoto huyo mwenye umri wa miaka 14 (jina limehifadhiwa), na ni mwanafunzi, alifikishwa mahakamani hapo kwa shtaka la kudhalilisha dini ya Kiislamu kwa kukojolea Quran Tukufu Oktoba 10 mwaka huu, akiwa eneo la Mbagala Chamazi. Kesi hiyo inasikilizwa katika mahakama ya watoto kwa sababu mtoto huyo ana umri chini ya miaka 18.

Washtakiwa wengine  waliosomewa mashtaka yao ni Maenga Yusuph (28), Hamad Euli (26),Shego Musa (26), Abdallah Said (22),Ramadhan Salum (28), Mashaka Iman (21), Kassimu Juma (33), Ibrahim Jumanne (20), Sospeter  John (33), Hamza Mohamed (22), Mwanahamisi Mohamed (30) , Dodo Mohamed (20) na wengine 23.

Wakazi hao wa Mbagala wanashtakiwa na makosa manne ya kula njama, kuharibu mali, wizi, kuvunja majengo na kuchoma moto makanisa  kati ya Oktoba 10 na 12 mwaka huu kwa nia ovu ya kutenda kosa.

Wakili wa Serikali, Tumaini Kweka, alimwambia  Hakimu Sundi Fimbo wa mahakama hiyo kuwa washtakiwa walivunja na kuingia ndani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Mbagala, na kutenda makosa hayo.

Washtakiwa hao pia wanatuhumiwa kuharibu mali mbali mbali zenye thamani ya sh. milioni 500 za  kanisa la KKKT.

Pia wanatuhumiwa kuiba vitu mbalimbali  vyenye thamani ya sh. milioni 20, lakini kabla ya kuiba mali hizo walimtishia Michael Samwel kwa kutumia nondo na matofali kwa nia yakufanikiwa kuiba mali hizo.

Washtakiwa hao wanatuhumiwa kuchoma moto kanisa la ELCT, kanisa la Agape Usharika wa Mbagala na kusababisha uharibifu wa mali zenye thamani ya sh. milioni 80.

Vile vile washtakiwa wanatuhumiwa kuharibu magari tisa, ambapo thamani ya uharibifu huo ni sh. milioni 20. Katika ya gari ambazo zimeharibiwa  lipo gari la  Serikali PT 2068 mali ya Jeshi la Polisi,  gari lingine ni la  Mchungaji Kinyota.

Pia wakili wa Serikali, Ladslaus Komanya, alidai kuwa washtakiwa wanatuhumiwa kuvunja kanisa la  Tanzania Assemblies of God (TAG), KKKT na kuiba vitu mbali mbali vyenye thamani ya sh. milioni 8 mali ya Kanisa la Waadventisti Wasabato (SDA).

Mawakili hao wa Serikali walidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika, na waliomba mahakama itoe masharti ya dhamana kwa kuzingatia kifungu namba 148 kifungu kidogo cha 5 (e).

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 30 mwaka huu kwa kuangalia dhamana za washtakiwa, ambapo kuna washtakiwa wengine hawatapata dhamana kwa sababu wamepatikana na shtaka la unyang'anyi wa kutumia silaha. Kisheria shtaka hilo halina dhamana kwa hiyo washtakiwa hao wataendelea kusota rumande.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages