Kuwasha moto ni jambo jepesi sana, lakini, kuuzima moto, yaweza kuwa ni kazi ngumu sana.
Ona, moto ulioanza kwenye nyumba
moja ya nyasi kijijini, waweza kusambaa haraka na hata kuteketeza kijiji
kizima. Na tangu utotoni tumetahadharishwa hatari ya kucheza na moto.
Naam, binadamu usicheze na moto, labda iwe kwenye mazingaombwe.
Sisi sote ni ndugu, na hii ni
Nchi Yetu. Hatuna haja ya kubaguana kwa misingi ya ukabila, dini na
rangi. Tuna historia ya kujivunia. Ni historia yetu wenyewe. Kinyume na
baadhi yetu wanavyofikiri au wanavyotutaka tufikiri, historia yetu
haikuanzia enzi za Mwarabu , Mjerumani au Mwingereza. Historia yetu
haikuanzia enzi za TANU wala Afro Shiraz.
Na dini hizi za kimapokeo
zinazotufanya sasa tufarakane zimekuja na kuzikuta dini zetu za asili,
na bado tunazo. Na hakika, Afrika hatugombanii matambiko. Afrika kila
ukoo una tambiko lake, hivyo basi, dini yake. Kamwe hutasikia Waafrika
wanagombania matambiko. Hutasikia Waafrika wakigombana kwa tofauti za
matambiko yao.
Na sisi ni Waafrika. Hii leo
mahala ambapo unaweza kuwagawa Watanzania na hata kufanikiwa kuwafanya
wachinjane ni kwenye kwenye tofauti zao za imani hizi za kimapokeo;
Uislamu na Ukristo.
Naam, tusifike mahali
tukagombana kutokana na tofauti za imani ama dini ambazo wala si za
asili yetu. Imani au dini ambazo, kama ilivyo dini zetu za asili, nazo
zinatutaka wanadamu tuishi kwa amani, upendo na maelewano.
Na hilo ndilo Neno la leo.
Maggid Mjengwa,
Iringa.
Iringa.
0788 111 765, 0754 678 252
http://mjengwablog.com
http://mjengwablog.com
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)