ismail Jussa
--
“Leo asubuhi nimewasilisha kwa Mwenyekiti wa Chama Taifa, Mheshimiwa
Profesa Ibrahim Lipumba barua ya kuomba kujiuzulu nafasi ya Naibu Katibu
Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) kwa upande wa Zanzibar , uamuzi ambao
nimeomba uanze kutekelezwa rasmi tarehe 10 Oktoba, 2012. “Nimechukua
uamuzi huu baada ya kuzungumza na kushauriana na viongozi wangu wa juu
wa Chama ambao ni Mwenyekiti, Profesa Lipumba, Makamu Mwenyekiti
Mheshimiwa Machano Khamis Ali na Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad
takriban miezi miwili iliyopita.
Nawashukuru baada ya kunitaka niwape muda wa kulitafakari
walinikubalia lakini wakaniomba nibakie hadi tutakapokamilisha baadhi ya
shughuli muhimu za Chama katika kipindi hichi. “Sababu kubwa
zilizonisukuma kukiomba Chama kiniruhusu niachie nafasi hii ni kutokana
na muda mrefu sasa kuhisi kwamba majukumu niliyo nayo ya kuwa msimamizi
mkuu wa utendaji wa Chama kwa upande wa Zanzibar na wakati huo huo kuwa
Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wa jimbo la Mji Mkongwe hakunipi fursa
ya kujifaragua na kutumikia nafasi zote mbili kwa ufanisi unaotakiwa.
Nataka kuona kazi ya kuibana Serikali ndani na nje ya Baraza ili
iwajibike zaidi kwa wananchi inaimarika zaidi. “Sambamba na sababu hiyo
ni kwamba nimekusudia kutumia muda mwingi zaidi kutoa mchango mkubwa
zaidi katika harakati za wananchi wa Zanzibar zinazoendelea za
kuhakikisha kuwa Zanzibar inarejesha mamlaka yake kamili kitaifa na
kimataifa itakayofuatiwa na kuwepo kwa Muungano wa Mkataba kati yake na
Tanganyika yenye mamlaka kamili kitaifa na kimataifa. “Harakati
zinazoendelea Zanzibar kwa njia za amani na za kidemokrasia kwa kutumia
mchakato wa Katiba Mpya zinahitaji kuungwa mkono na kupewa msukumo wa
dhati na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliochaguliwa na wananchi wa
Zanzibar kwenda kusimamia maslahi yao na ya nchi yao.
Nimetafakari na kuona kwamba nikiwa sina majukumu mengine ya
kiutendaji nitakuwa na muda kutosha wa kulifanya hili mimi na
Wawakilishi wenzangu tunaotoka CUF na CCM, vyama viwili vya siasa
vilivyomo Barazani. “Nafurahi kwamba leo nimetimiza azma yangu hiyo.
Pamoja na uamuzi huu, naendelea kubaki kuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la
Uongozi la Taifa na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa. “Nawahakikishia
viongozi na wanachama wenzangu wa CUF kwamba tutaendelea kushirikiana
pamoja katika shughuli nyengine zote za kisiasa za Chama na kwa pamoja
tutafanya kazi kuyatimiza malengo tuliyojiwekea. Naahidi kumpa
ushirikiano kikamilifu mwanachama yeyote atakayeteuliwa kujaza nafasi
ninayoiwacha.
” HAKI SAWA KWA WOTE ”
ISMAIL JUSSA
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)