Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Profesa Idris Kikula
Bodi ya
Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesema imeshapeleka fedha
za chakula na malazi katika vyuo vyote vyenye sifa ya kupata huduma hiyo
tangu wiki iliyopita.
Kauli hiyo ya HESLB, ilitolewa na Afisa Habari wake, Veneranda Malima, jijini Dar es Salaam jana.
Alisema kuhusu utaratibu wa wanafunzi kupata fedha hizo siyo jukumu la
HESLB bali ni viongozi wa vyuo hivyo kwa utaratibu waliojipangia
wenyewe.
Hata hivyo, Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) cha jijini Dar es Salaam,
kimesema fedha hizo hazijafika, lakini kimeahidiwa na HESLB kuwa
zitapelekwa katikati ya wiki hii.
Waziri wa Mikopo wa Chuo hicho, Alek George, alisema: “Sio kweli
kwamba, fedha zimeshatumwa hapa chuoni, walituambia kuwa wiki hii
watatupatia, lakini mpaka sasa bado.”
Wakati CBE wakisema hivyo, Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) kilisema
kupitia kwa Kaimu Afisa wake wa Mikopo, Rajabu Kufiri, kuwa wameshasaini
fedha hizo tangu wiki iliyopita na kwa sasa wako katika utaratibu wa
kuwapatia wanafunzi fedha hizo.
Chuo cha Tumaini Kampasi ya Dar es Salaam kilisema bado hawajapewa fedha
hizo kutokana na kuchelewa kufungua chuo, na kwa sasa utaratibu wa
kuwasajili wanafunzi unaendelea ili kupata idadi kamili ya wanafunzi
wanaoendelea na masomo.
Afisa Mikopo wa Chuo hicho, Ukende Mwakitwange, alisema juzi HESLB
waliwapatia orodha ya wanafunzi waliosajiliwa katika chuo hicho, lakini
fedha hawajapatiwa.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Profesa Idris Kikula,
alisema: “Bado hatujapata mikopo na leo hii (jana) nimetoka kuzungumza
na wenzangu kuhusiana na suala hilo la mikopo kwa wanafunzi.”
Alisema kutokana na hali hiyo utawala umeamua kumtuma mtu kwa ajili ya kufuatilia suala hilo HESLB.
Afisa Habari wa Chuo Kikuu cha St. John, Karim Meshack, alisema HESLB
imewapelekea majina ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza, ambao wanastahili
kupata mikopo.
Alisema mikopo hiyo inaweza kufika chuoni hapo mara baada ya wanafunzi hao kufanyiwa usajili.
Naye Afisa Mikopo wa Chuo cha Mipango, Daud Nyagalu, alisema: “Bado hatujapata mikopo na tunaendelea kufuatilia.”
Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ushirika na Biashara (MUCCoBS), Profesa
Faustine Bee, alisema: “Tunatarajia kufungua chuo Oktoba 15, mwaka huu,
wanafunzi watakapofika chuoni ndio tutakuwa kwenye nafasi nzuri ya
kuzungumzia kama wametuingizia fedha au la, matarajio yetu ni kupata
fedha hizo kwa wakati.”
Uongozi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Stephano Moshi (Smmuco), ulisema chuo
bado hakijafunguliwa na baada ya kufunguliwa ndio watakuwa kwenye nafasi
nzuri ya kueleza juu ya fedha za wanafunzi hao kama zimeingizwa kwenye
akaunti au la.
Chuo cha Ustawi wa Jamii hakipapata fedha hizo na habari kutoka ndani ya
uongozi zinaeleza kuwa chuo kilichelewa kufanya mitihani na kupeleka
majina katika Bodi.
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kilisema fedha hizo zingepelekwa
chuoni hapo Alhamisi iliyopita, jana kilishindwa kuthibitisha kuzipokea
baada ya Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandara, kueleza
kuwa alikuwa mbali na chuo.
Hata hivyo, Naibu Makamu Mkuu wa UDSM (Utawala), Profesa Yunus Mgaya na
Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Frolence Luoga, hawakupatikana.
Habari na Gwamaka Alipipi, Amos Mbungu na Issaya Kisimbilu, Dar; Jacqueline Massano, Dodoma; na Salome Kitomari, Moshi.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)