Ndugu zangu,
KUNA tunaokumbuka kisa cha mfalme simba na wanyama wenzake. Mfalme simba alipatwa na ugonjwa. Akabaki kibandani asiweze kutembea. Na njaa nayo ikamshika. Wanyama wengi walimtembelea mfalme kumjulia hali. Walikwenda akina pundamilia, twiga, swala na wengineo. Kila aliyeingia kibandani kwa mfalme hakutoka nje.
KUNA tunaokumbuka kisa cha mfalme simba na wanyama wenzake. Mfalme simba alipatwa na ugonjwa. Akabaki kibandani asiweze kutembea. Na njaa nayo ikamshika. Wanyama wengi walimtembelea mfalme kumjulia hali. Walikwenda akina pundamilia, twiga, swala na wengineo. Kila aliyeingia kibandani kwa mfalme hakutoka nje.
Mfalme simba katika kiu yake ya nyama akamtamani sana kobe.
Ni kobe katika wanyama wote ambaye hakuonekana katika nyumba ya mfalme
simba kumjulia hali. Simba akatuma ujumbe akilalamika; “Enenda
ukamwambie kobe, nashangaa katika kuugua kwangu sijamwona kuja
kunijulia hali”!
Ujumbe ukamfikia kobe. Siku moja kobe naye akaenda kumjulia hali
mfalme simba. Hakufika mpaka iliko nyumba ya mfalme simba. Alisimama
mbali na kutamka: “Ewe mfalme wangu simba, nimekuja kukujulia hali,
waendeleaje na afya yako?”.
Mfalme simba akajibu: “Mbona salamu hizo unazitoa ukiwa mbali hivyo?”.
Kobe akamjibu mfalme wake: “ Kuna jambo linanishangaza mfalme wangu,
naona nyayo zote za wanyama zimeelekea kwako, lakini hakuna nyayo
zinazorudi”
Katika jamii yetu sasa kuna akina mfalme simba wagonjwa na wenye
njaa ya nyama. Wamewatafuna twiga, swala, pundamilia na wengineo. Sasa
wanawatamani akina kobe pia!
Ndio, katika nchi yetu sasa kuna
harakati za kimakundi. Tunaziona ndani ya chama tawala, tunaziona nje
ya chama hicho. Kuna wenye kuongoza harakati hizo.
Na Watanzania tulio wengi tumekuwa ni watu wa kupenda sana kutafuna
maneno. Kuna mawili makubwa ambayo ni mapungufu yetu; mosi, hatuna
misimamo, pili, tukiwa nayo hatuisimamii.
Tunapenda sana
kuzungumza tusichomaanisha na mara nyingi hatumaanishi tunachozungumza.
Na Mtanzania haumizi kichwa kujiuliza; “ kwanini nizungumze”. Maana
suala si unachozungumza, bali ni kwanini unazungumza.
Na kwanini wananchi wanaonekana kukata tamaa na kukosa imani kwa
kinachozungumzwa na viongozi wao. Ndio, kikubwa kinachokosekana hapa
ni namna nzuri ya kuwasiliana na wananchi ili kuwafahamisha na labda
kuwaelimisha juu ya kilichotokea.
Watanzania wengi hawana taarifa muhimu kuweza kutafsiri matukio na
kinachozungumzwa na viongozi wao. Ni ukweli kuwa Watanzania walio
wengi wanaishi vijijini. Ni takribani asilimia 21 tu ya Watanzania
wenye fursa ya kupata taarifa muhimu juu ya kinachoendelea katika nchi
yao; ni kupitia magazeti, runinga na redio. Waliobaki asilimia sabini
na tisa ya Watanzania ndio hao wa Manzese Dar es Salaam, Mwanjelwa
Mbeya, Kihesa na Kilolo Iringa na kwingineko.
Ni hawa wasio na taarifa za kutosha kutafsiri mambo na hata kufanya maamuzi yanayotokana na kuwa na taarifa (informed decisions). Ni asilimia 79 hii ya Wanzania wa Mwanjelwa , Kilolo na kwingineko wenye kuiweka Serikali madarakani kwa wingi wa kura zao.
Media, kwa maana ya ya wanahabari ndio walipaswa wajitoe
kwenye vita vya kimakundi na kuwasaidia Watanzania hawa kupata taarifa
zitakazowawezesha kufanya maamuzi sahihi.
Lakini miongoni mwa
wanahabari hawa, kuna walioingia katika foleni ya kwenda kuwajulia
hali wafalme wagonjwa. Wamejiingiza kwenye vita ya kimakundi.
Wamelisahau jukumu lao, wamelisahau kundi kuu. Ni kundi lile la asilimia
79 ya Watanzania.
Tunaziona nyayo za baadhi ya wanahabari zikienda kwa wafalme wagonjwa, hatuzioni nyayo zao za kurudia!
Wanahabari
walipaswa kuwa daraja la kupitisha taarifa kutoka chini kwa wananchi
kwenda juu kwa viongozi, na kinyume chake. Lakini, miongoni mwa
wanahabari hao, wameamua kwa makusudi kulivunja daraja hilo. Ni kweli
kuwa kila mwanadamu kwa namna moja au nyingine ananunulika, lakini kwa
wengine, bei zao ni utu na heshima, basi. Wanasukumwa kufanya yale
yenye maslahi mapana kwa taifa.
Na hilo ni Neno La Leo. ( Limechapwa pia kwenye Mwananchi, leo Jumapili)
Maggid,
Iringa
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)