Makamu
wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar balozi Seif Ali Iddi akiwa pamoja
na Mwenyekiti wa Ushirika wa Mageuzi ya Kijani ya Afrika{ AGRF }Dr. Kofi Anna Kulia na Bibi
Melinda Gates Mwenyekiti Mwenza ambae pia
ni kuanzilishi wa Mfuko wa Misaada wa Kimataifa. Kushoto ya Balozi Seif
ni Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Burundi Bwana Invazi.
Rais
wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika
picha ya pamoja na Viongozi mbali mbali wa kimataifa waliohudhuria Mkutano wa
Pili wa Ushirika wa Mageuzi ya Kijani ya Afrika unaofanyika Hoteli ya Ngurdoto
Mkoani Arusha Tanzania
Baadhi
ya Mawaziri wa SMZ na SMT waliohudhuria
Mkutano wa Pili wa Ushirika wa Mageuzi ya Kijani ya Afrika{AGRF }KATIKA Ukumbi wa Hoteli ya Kimataifa ya Ngurdoto
---
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. jakaya
Mrisho Kiwete alisema Bara la Afrika linaweza kufanikiwa kuondokana na Janga la
Umaskini na Njaa endapo Jamii za Mataifa hayo zitajikita zaidi katika kuwa wazi
na kushirikiana pamoja.
Rais Kikwete
alieleza hayo wakati akiufungua Mkutano wa Pili wa Ushirika wa Mageuzi ya
Kijani ya Afrika {African Green Revolution Forum -AGRF} wa siku tatu unaofanyika katika Ukumbi wa
Hoteli ya Kimataifa ya Ngurdoto Mkoani
Arusha ambao pia umehudhuriwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
Ali Iddi kwa niaba ya Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Sheni.
Alisema hakuta kuwa na njia ya mkato kwa Bara hili
kuelekea kwenye Kilimo imara bila ya kuwa na
mipango makini itakayosimamiwa na Washirika wa sekta hiyo zikiwemo Taasisi za
Umma,Sekta Binafsi na Jumuiya za kiraia
ikitiliwa maanani zaidi Vituo vya Utafiti katika maeneo ya Kilimo hasa
Vijijini.Rais Kikwete
alisisitiza kwamba Wakulima wengi ndani ya Bara la Afrika katika maeneo ya
Vijijini wanakabiliwa na Taaluma duni inayochangia kudumaza uzalishaji katiika
sekta ya Kilimo.
Alifahamisha
kwamba jembe la mkono linaloendelea kutumiwa na Wakulima walio wengi Barani Afrika linapunguza nguvu za Wakulima
hao katika uzalishaji na hatimae kuzindisha matatizo na mapungufu katika Sekta
hiyo muhimu.
“ Nguvu
nyingi za Wakulima wadogo wadogo Barani Afrika zinaishia katika jembe la Mkono
ambalo hutumiwa na wakulima waliowengi hasa Vijijini”. Alisisitiza Rais
Kikwete.
Alieleza
kuwa Kilimo kinaendelea kuwa chanzo kikubwa cha utajiri wa Afrika licha ya kuwa
sera ambazo hazikuhitaji na kutiliwa maanani
katika miongo kadhaa iliyopita.
Hata hivyo
alifafanua kwamba Kilimo kitaendelea kuwa msingi wa usalama wa chakula na
maendeleo ya Kiuchumi.
Aidha
alieleza kuwa dhamira iliyopo ya pamoja iliyojumuisha makundi mbali mbali ya
sekta ya Umma na zile Binafsi katika
Mkutano huo wa Pili wa Ushirika wa Mageuzi ya Kijani Barani Afrika inaweza kushawishi muelekeo wa mageuzi na
uwekezaji kwenye Kilimo cha Bara la Afrika.
Alisema
Kilimo kinaajiri zaidi ya asilimia 65% ya nguvu kazi Barani Afrika na
kinaendelea kuongoza uchumi wa Mataifa mengi ya Bara hili ikiwa ni kati ya
asilimia 60% na 80% ya mapato ya ndani.
Rais wa
Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania aliupongeza Uongozi wa Ushirika wa Mageuzi ya
Kijani ya Afrika { AGRF } kwa uamuzi wake wa kuufanya Mkutano huo wa Pili
Nchini Tanzania uamuzi ambao umeipa heshima kubwa Tanzania katika Nyanja za
Kimataifa.
Kupitia
Mkutano huo Rais Kikwete pia alimpongeza Mwenyekiti mwenza ambaye pia ni
muanzilishi wa Mfuko wa Kimataifa wa Misaada Bibi Melinda Gates kwa juhudi zake
za kuendelea kuunga mkono harakati za Kiuchumi na Kijamii za Mataifa maskini
Duniani ikiwemo Tanzania.
Naye Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitoa salamu katika Mkutano
huo kwa niaba ya Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Sheni alisema mkazo
unaendelea kuchukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwajengea
uwezo Wakulima Wadogo wadogo.
Balozi Seif
alisema Mkazo huo umewekwa kupitia
msaada wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Kilimo { IFAD } sambamba na
uimarishwaji wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo kiliopo Kizimbani.
Makamu
wa
Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kuwa Zanzibar bado imekipa Kilimo
kipaumbele katika kumkomboa Mwananchi ambapo zaidi ya
asilimia 80% ya watu wote wanategemea Kilimo ambacho ni sekta muhimili
kwa Uchumi na Maendeleo ya Taifa.Mapema Mwenyekiti wa Ushirika wa
Mageuzi ya Kijani
ya Afrika ambaye pia ni Katibu Mkuu Mstaafu wa Umojwa Mataifa Dr.Koffi
Annan
alisema Afrika inahitaji kuongeza nguvu katika kuwajengea uwezo wa
uzalishaji
Wakulima wadogo wadogo hasa kutokana na asilimia 60% ya Ardhi ya Bara
hili kuwa
ni jangwa.
Dr. Annan
alisema ni vyema Wataalamu wakaangalia zaidi
mbinu bora za kuimarisha miundo mbinu katika maeneo ya Vijijini ili kupambana
na changamoto zilizopo kwa kutumia mbinu za kisasa za Kilimo.
“Mafanikio
ya Bara la Afrika katika kutanuka Kiuchumi kutategemea miundo mbinu ya
uwekezaji katika maeneo ya wakulima wadogo wadogo hasa Vijijini”.Alisisitiza
Mwenyekiti huyo wa Ushirika wa Mageuzi ya Kijani ya Afrika{AGRF}Dr. Annan.
Aliongeza
kwamba mbinu hizo ni vyema zikaenda sambamba
na ushirikishwaji wa Sekta Binafsi pamoja na uendelezwaji wa Sekta ya utunzaji
wa Mazingira.
Kwa upande
wake Mwenyekiti Mwenza ambae pia ni muanzilishi wa wa Mfuko wa Kimataifa wa
Misaada Bibi Melinda Gates ameipongeza Tanzania kwa hatua yake ya kuimarisha
Sekta ya Kilimo kupitia Mpango wake wa Kilimo kwanza.
Aliahidi
kwamba Taasisi yake itaendelea kuunga mkono jitihada za Mataifa kadhaa
ulimwenguni katika harakati zao za kujikwamua na umaskini na kuondokana na
maradhi.
Mkutano huo
wa Pili wa Ushirika wa Mageuzi ya Kijani ya Afrika{ AGRF }umehudhuriwa na
Washiriki zaidi ya elfu moja kutoka Taasisi, Jumuiya na Mashirika mbali mbali ya
ndani na nje ya Bara la Afrika.
Na
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)