Mabadiliko ya Uongozi TAMWA: Valerie Msoka achuku nafasi ya Ananilea Nkya - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Mabadiliko ya Uongozi TAMWA: Valerie Msoka achuku nafasi ya Ananilea Nkya

 Ananilea Nkya
--
Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kimepata Mkurugenzi Mtendaji mpya ambaye anachukua nafasi ya Ananilea Nkya anayemaliza muda wake baada ya kulitumikia shirika hilo kwa miaka kumi na moja.

Mkurugenzi huyo mpya wa TAMWA, Valerie Msoka ambaye ni miongoni mwa wanahabari wanawake 12 walioanzisha TAMWA,  amefanya kazi  za kutukuka  katika ngazi  ya kitaifa, kikanda na kimataifa.

Valerie Msoka atakabidhiwa rasmi ofisi Alhamisi tarehe 27 Septemba katika sherehe fupi itakayofanyika  kuanzia saa 3.30 hadi ya 5.00 asubuhi.

Sherehe hiyo itakayofanyika katika ofisi za TAMWA zilizoko  eneo la Sinza-Mori, Dar es Salaam inatarajiwa kuhudhuriwa na wahariri  na  wanahabari kutoka vyombo vya habari mbalimbali,  wawakilishi wa mashirika ya wanahabari,  Wakurugenzi Watendaji kutoka mashirika ya kiraia na viongozi  wa TAMWA  wa zamani na  sasa.

Valerie Msoka alifanya  kazi  Radio Tanzania Dar es Salaam, shirika la utangazaji la Uingereza BBC idhaa ya Kiswahili na Kiingereza kabla ya kujiunga  na Umoja wa Mataifa.

Kadhalika Valerie Msoka mwenye shahada ya Uzamiri  katika fani ya  Uandishi wa habari wa Kimataifa (M.A in International Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha City nchini Uingereza,  amefanya  kazi   kwenye maeneo ya vita ikiwemo  Iraq, Sudan, Rwanda, Congo na Burundi.

Valerie Msoka  anachukua uongozi wa TAMWA wakati shirika hili likiwa linajiandaa kuanza kutekeleza  mradi  mkubwa wenye lengo la kuimarisha vuguvugu katika harakati za kujenga usawa wa kijinsia na kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

TAMWA  itatekeleza mradi huo kwa kushirikiana na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Chama Cha Wanasheria Wanawake nchini (TAWLA),  Chama Cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) na Kituo cha Usuluhishi (CRC).

Wilaya kumi zitanufaika na mradi huo ambazo ni Wete (Pemba Kaskazini), Unguja Magharibi (Unguja Urban West), Wilaya ya Unguja kusini (Unguja South district), Kisarawe (Pwani), Newala (Mtwara), Mvomero (Morogoro), Lindi vijijini na Ruhangwa (Mtwara),  Kinondoni na Ilala, (Dar es Salaam).

Ananilea Nkya
Mkurugenzi Mtendaji

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages