Waliobainika kutojua kusoma, kuandika sekondari waendelea na shule - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Waliobainika kutojua kusoma, kuandika sekondari waendelea na shule

Na Joachim Mushi, Korogwe

WANAFUNZI waliojiunga na masomo ya kidato cha kwanza mwaka huu katika shule za Serikali na baadaye kubainika kuwa hawajui kusoma na kuandika kwa ufasaha wanaendelea na masomo yao.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi, katika baadhi ya shule za sekondari kwa wilaya za Korogwe na Moshi Mjini umebaini wanafunzi hao kuendelea na shule licha ya walimu kuwachuja na kutoa taarifa sehemu husika kama walivyo elekezwa.

Akizungumza hivi karibuni katika mahojiano mjini Moshi, Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Sekondari Mawenzi, Domin Kweka alisema kwa mujibu wa vigezo vilivyotolewa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kubaini wanafunzi wanaofaulu kujiunga na sekondari, wasio na sifa jumla ya wanafunzi sita walibainika.

Alisema wanafunzi hao walishindwa kabisa kufanya vizuri katika mtihani waliopewa jambo ambalo lilionesha ulakini katika kujiunga kwao na masomo ya sekondari, japokuwa wanaendelea na shule hadi sasa.

"Sisi tuliwapata sita, hawa walikuwa hawajui kusoma na kuandika na kutoa taarifa sehemu husika tunasubiri utaratibu mwingine...lakini hadi muda huu wanaendelea na masomo ya kidato cha kwanza," alisema Kweka.

Aidha aliongeza kuwa tatizo hilo hujitokeza kila mwaka kwa wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza na hadi sasa katika madarasa mbalimbali wapo wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika.

Alisema kwa shule hiyo ya Mawenzi kidato cha kwanza kina wanafunzi sita wasiojua kusoma na kuandi, kidato cha pili wanafunzi sita, kidato cha tatu wanafunzi watatu huku kidato cha nne kikiwa na wanafunzi wawili wasiojua kusoma na kuandika.

Uchunguzi uliofanywa wilayani Korogwe pia ulibaini wanafunzi walioshindwa kufaulu katika mchujo uliotolewa na Serikali kuendelea na masomo ya kidato cha kwanza, licha ya shule kadhaa za sekondari kupeleka majina hayo kwa viongozi wa idara husika.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Nyerere Memorial ya Wilayani Korogwe, Steven Killo alikiri shule yake kuwa na baadhi ya wanafunzi kadhaa wasiojua kusoma na kuandika hata katika madarasa mengine japokuwa hakutaja idadi.

Aidha aliongeza kuwa katika shule hiyo mchujo kwa wanafunzi wapya waliojiunga kidato cha kwanza walibaini kuwepo kwa mwanafunzi mmoja asiyejua kusoma na kuandika na kuwasilisha taarifa kwa viongozi wa idara ya elimu wilaya na hakukuwa na maelekezo yoyote baada ya taarifa.

Akizungumzia suala hilo Ofisa Elimu Taaluma, Halmashauri ya Mji wa Korogwe, Elius Mkwizu alisema hata hivyo nia ya Serikali kuwapima wanafunzi hao haikuwa kuwarejesha nyumbani bali kujua tatizo hilo na kuangalia namna ya kulidhibiti.

Habari hii imeandaliwa na mtandao wa Thehabari.com (www.thehabari.com) kwa ushirikiano na HakiElimu

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages