Mchungaji wa Kanisa la Christian Chapel la Dar es Salaam, George Makala (kulia)akifafanua jambo kwa waandishi leo
Mwanasheria wa Wakazi hao, Living Kimaro (katikati) kutoka Kampuni ya L & K. Law Chambers akizungumza na wanahabari leo
Mwenyekiti, Antony Mseke akizungumza
Waandishi wakioneshwa mipaka ya eneo hilo
Bango la NEMC eneo nje kidogo ya eneo hilo linasema hivi
Baadhi ya wakazi wa Mbezi Beach Kata ya Kilongawima waliokubwa na bomoa bomoa wakiwatembeza wanahabari leo kuona eneo hilo
Na Joachim Mushi wa Thehabari.com
WAKAZI 32 wa eneo la Mbezi Beach Kata ya Kilongawima
wanakwenda mahakamani kupinga kitendo cha Serikali kuwabomolea nyumba zao hivi
karibuni, kitendo ambacho wanadai wameonewa kwani wao wanamiliki maeneo hayo
kihalali, huku baadhi yao
wakiwa na nyaraka muhimu za umiliki na baraka kutoka Serikali za Mtaa husika.
Wakizungumza na vyombo vya habari leo wakazi hao wamesema
wanasikitishwa na kitendo hicho cha mabavu kufanywa na Serikali tena kwa kuvizia
ilhali kulikuwa na taratibu za kisheria za kufuatwa kabla ya zoezi hilo kama
kulikuwa na haki ya kufanyiwa hivyo.
Akitoa tamko la wakazi wa eneo hilo
leo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa wakazi
hao, Antony Mseke alisema madai ambayo Serikali kupitia Baraza la Usimamizi wa
Mazingira (NEMC) imeyatoa kuwa wao wamevamia eneo la mikoko na kujenga maeneo
yasioruhusiwa hayana msingi wowote kwani eneo hilo lipo mbali na mikoko hiyo.
Alisema wanakwenda mahakamani kutafuta haki yao
kwa kuwa kilichofanyika ni uvunjaji wa sheria na huenda kuna sababu nyingine
wanazo na si kama ilivyotamkwa na waliobomoa.
Mseke alisema eneo hilo
kuna mabango ya NEMC ambayo yanaainisha ni eneo gai lisiloruhusiwa kujengwa
ambamo imo mikoko ya bahari, lakini katika nyumba zote zilizobomolewa zipo nje
na mbali na mipaka ya taasisi hiyo ya mazingira.
“Tumeonewa kupita kawaida tunaiomba Serikali isiwe ikifanya
kazi kwa hali kama hii ya mabavu…tunakwenda
mahakamani kutafuta haki yetu maana tunaamini tupo hapa kihalali,” alisema
kiongozi huyo na mwakilishi wa waathirika wa bomoa bomoa hiyo.
Akifafanua zaidi Mchungaji wa Kanisa la Christian Chapel la
Dar es Salaam, George Makala ambaye naye ni mmoja wa wakazi waliokubwa na adha
hiyo alisema baadhi yao wamekuwepo eneo hilo tangu mwaka 1992 bila matatizo
yoyote huku wakitambuliwa na Serikali za mitaa kihalali.
Alisema anashangaa kuona NEMC kujitokeza na kuwabomolea
majengo yao
tena bila taarifa kitaratibu. Ameongeza zoezi hilo
linaulakini kwani yapo majengo mengine ambayo ni ramani moja eneo hilo lakini
hayakubomolewa jambo ambalo linazidi kujenga mazingira ya uonevu.
Alisema pamoja na mambo mengine alama za ‘X’ ziliwekwa Julai
8, 2012 na watu wasiojulikana na baada ya wao kuanza kufuatilia Julai 10, 2012 wavamizi
walikuja na silaha kali na kufanya ubomoaji jambo ambalo limewatisha.
“Sisi hatukuwa na mgogoro na Serikali wala kugoma chochote, eneo
ambalo mara zote lilikuwa na mvutano lilikuwa mbele yetu tena ni mbali
nasi…siku zote tulitambua hilo hata baadhi ya viongozi wa Serikali wanalijua
hilo, tunashangaa kuona leo tunabomolewa hivi,” alisema mchungaji huyo ambaye
licha ya jingo lake kubomolewa na Kanisa analochunga pia limebomolewa.
Naye Mwanasheria wa Wakazi hao, Living Kimaro kutoka Kampuni
ya L & K. Law Chambers ya jijini Dar es Salaam
amesema zoezi hilo halikufanyika kitaratibu wala
na mamlaka husika hivyo wanakwenda mahakani kudai haki yao.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)