Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Ananilea Nkya akiwasilisha ripoti ya utafiti kwa wanahabari hivi karibuini.
--
SERA
ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ya Mwaka 2000, imenukuu sehemu ya Katiba ya
Tanzania ya mwaka 1977 na marekebisho yake ya mwaka 1984. Sehemu hiyo inaeleza
kwamba Tanzania ni nchi inayothamini usawa na haki za binadamu. Katiba pia inasisitiza
usawa na heshima kwa binadamu wote, heshima ya kutambua na kuthamini utu wa mtu
pamoja na kuhakikisha haki mbele ya sheria.
Hata
hivyo wakati Katiba ya nchi na Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia
inasisitiza hayo bado hali ya unyanyasaji wanawake kwa vipigo nchini Tanzania
inajitokeza kwa kiasi kikubwa hasa maeneo ya vijijini. Kwa
mujibu wa utafiti wa kihabari (journalistic survey) uliofanywa mwezi Aprili
2012 na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) kwa kushirikiana na
vyombo mbalimbali vya habari katika mikoa 20, ikiwepo 15 ya Tanzania Bara na mitano
ya Zanzibar kuhusu hali ya vitendo vya ukatili nchini. Bado suala la vipigo kwa
wanawake limejitokeza kiasi kikubwa.
Ripoti
ya utafiti huo inaonesha kuwepo kwa vipigo kwa wanawake karibu kila wilaya iliofanyiwa
utafiti. Kimsingi hili laweza kuwa tatizo kubwa la kitaifa. Katika familia
nyingi, wanawake bado wanaendelea kupigwa na wanaume, hasa waume zao au wapenzi
wao.
Na
kama hiyo haitoshi taarifa za utafiti zinabainisha kuwa yapo maeneo ambayo hata
viongozi wa kiserikali ngazi za jamii vijijini wamekuwa wakitoa adhabu za
vipigo ambazo huwaathiri zaidi wanawake. Kipigo chochote kwa mwanamke ni kibaya
kwa kuwa kinamuathiri hata katika utendaji wake wa majukumu ya uzalishaji mali.
Takwimu
zilizotolewa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto mwaka 2000,
kupitia mwongozo wa sera ya wizara hiyo zinaeleza kuwa wanawake ni wazalishaji
wakubwa hasa maeneo ya vijijini. Inakadiriwa kuwa asilimia 60 ya chakula huzalishwa
na akinamama. Licha
ya kundi hilo muhimu kwa uzalishaji kuwa hodari wa kuzalisha lakini halina
uamuzi juu ya mali ambayo linaizalisha kutokana na mazingira ya mfumo na
vitendo vya unyanyasaji vikiwemo vitendo vya vipigo dhidi yao.
Lakini
utafiti wa kihabari katika taarifa yake unafafanua kwamba miongoni mwa sababu
za wanawake kupigwa ni ulevi, “mdomo” wa akina mama, ubabe wa akinababa,
fumanizi, mfumo dume, ukiukwaji wa mafunzo ya ndoa, wivu, umaskini, “mapenzi,”
ndoa za mitala, ndoa za kulazimishwa na mambo mengine.
Pamoja
na hayo sheria imeweka wazi dhidi ya adhabu kwa kipigo, Sheria ya Makosa ya
Jinai Sura ya 16 ya mwaka 2002 kifungu
240 cha kinasema kwamba mtu yeyote aliyempiga mwenzake atakuwa ametenda kosa la
jinai na atahukumiwa kwenda jela kwa muda wa mwaka mmoja.
Adhabu hii itatumika katika
mzingira ambayo muathirika wa kipigo hakupata madhara makubwa sana. Aidha kifungu 241 cha Sheria ya Makosa ya
Jinai kinatoa adhabu ya kifungo cha miaka mitano jela kwa mtu yeyote
aliyemdhuru mwenzake kwa kipigo na mtu huyo kupata madhara makubwa sana.
Mfano
utafiti unabainisha kuwa Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam, kwa mwaka 2011
pekee kesi 14 ziliripotiwa. Hakimu Mkuu
wa Mahakama ya Mwanzo Mbagala (PPCM) Fatuma Katunzi, anasema kesi za vipigo
zipo na kwamba mwaka 2011 zilifikishwa kesi 6, kati ya kesi hizo 2 zilitolewa
hukumu ya kifungo na faini.
Mwenyekiti
wa Mtaa wa Msufini Kata ya Chamazi, Muharami Mlawa, anasema kesi 5 ziliripotiwa
katika mtaa huo. Naye Mwenyekiti wa mtaa wa Majimatitu ‘B’ Kata ya Charambe
Fadhil Mpinga anasema kesi 3 za vipigo zilifikishwa kwake. Ofisa Mtendaji Mtaa
wa Mianzini Jimmy Berege, anasema uongozi wa mtaa huo ulipokea kesi 6 kati ya
kesi hizo tatu ziko polisi.
Neema
Lalashe (46) ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Uhuru Kata ya Orukasment, wilayani Simanajiro,
anasema kwa sasa vitendo vya kipigo dhidi yao vinafanyika kistaarabu tofauti na
miaka ya nyuma.
“Zamani
mwanaume alikuwa anafunga mikono na miguu kwenye mti ndiyo unachapwa, unapigwa
mpaka unapoteza fahamu lakini siku hizi kidogo hayo mambo yamepungua, kama
umekosea atakuchapa lakini hufungwi tena na kamba,” anasema Lalashe.
Mwanamama
huyu anaamua kuhalalisha kipigo kutokana na mazoea, na anafikia hata kuona
kipigo cha nyuma kilikuwa cha kudhalilisha zaidi kuliko kinachotolewa kwa sasa.
Hali hii inaonesha ni namna gani maeneo mengine vipigo vinazoeleka na hata
kuhalalishwa kijamii kutokana na kukata tamaa kimsaada.
Bi.
Wandoa Edward (37) mkazi wa Kijiji cha Kisiriri, Kata ya Kisiriri, Iramba
mkoani Singida, anatamani kujitoa kwenye ndoa kutokana kero za kinyanyasaji
anazozipata kwa mwenza wake. “Nataka
kurudu nyumbani, kwani nimechoka kuishi katika ndoa yenye manyanyaso. Nyumba
yangu si salama tena,” anasema Bi. Edward.
Mtendaji
wa Kata ya Karatu, Paulo Lagwen anakiri kuwepo kwa vipigo kwa wanawake kutoka
kwa waume zao. Anaendelea kubainisha kuwa idadi ya vipigo kwa sasa imepungua
ikilinganishwa na ilivyokuwa hapo nyuma.
Anasema
kwa Wilayani Karatu, vipigo dhidi ya wanawake vipo, ingawa ni nadra kwa matukio
haya kukuta yanaripotiwa katika vyombo vya dola. Wanaume wa Kiiraq
wamestaarabika kidogo kwa utoaji vipigo kwa sasa. Idadi ya vipigo imepungua
ikilinganishwa na hapo awali.
Mkoani
Mbeya maeneo ya vijijini, zipo ndoa nyingi zizovunjika kutokana na kipigo kwa
wanawake. Mfano kati ya watu wote 22 waliohojiwa walikiri wanaume kuwepo wanaotoa
vipigo kwa wanawake. Lucia Gwamaka mkazi wa Kijiji cha Mpandapanda, anasema
kupigwa kwa mwanamke ni jambo la kawaida.
Kama
hiyo haitoshi tatizo la vipigo linajitokeza tena wilayani Kilolo mkoani Iringa.
Taarifa ya utafiti inabainisha kuwa viongozi wanapofikishwa kwenye ofisi za
kijiji kwa shitaka lolote viongozi hujichukulia sheria mkononi na kuwapiga
watuhumiwa.
Kwa mfano utafiti ulishuhudia
wanawake wawili ambao walikuwa na ujauzito katika Kijiji cha Kidabaga kwa
nyakati tofauti wakipigwa na viongozi wa kijiji hicho na hatimaye mimba
walizokuwa wamebeba zikaharibika kutokana na madhara ya vipigo.
Kwa mujibu wa taarifa ya utafiti inadaiwa kuwa viongozi waliohusika na
vipigo hivyo ni Mwenyekiti wa kijiji cha
Kidabaga, Nicolous Katandasi na
Mtendaji wa kijiji hicho, Vincent Gaifalo. Taarifa inafafanua kuwa Mwenyekiti
wa Kijiji, Nicolous Katandasi mnamo mwezi Mei 2011 alimchalaza viboko 16 mama
Silivia Kimata, kitendo kilichosababisha mimba ya miezi mine kuharibika.
Aidha
Mtendaji wa kijiji hicho, Vincent Gaifalo alimchalaza viboko 30 Seidina
Kidwangise aliyefika kijijini hapo kumzika ndugu yake na kusababisha mimba
yake kutoka na mama huyo kupata ulemavu
wa kushindwa kusimama na kutembea.Mganga
Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Iringa, dakta Deogratias Manyama anathibitisha
kwamba hospitali hiyo Aprili 19, 2012 ilimpokea na kumlaza Bi. Kidwangise akiwa
hawezi kusimama wala kutembea na uchunguzi ulibaini alikuwa amepoteza ujauzito huku
mwili wake ukiwa na majeraha.
Jambo
la kushangaza wanakijiji hao walisema kuwa ingawa mtendaji wa kijiji aliyempiga
mama huyo na kumsababishia madhara hayo makubwa
alikuwa amefikishwa polisi, hawaamini kuwa haki itatendeka dhidi yake
kutokana na kushamiri kwa rushwa hapo kijijini na kwenye vyombo vya sheria wilayani.
“Ingawa
wanakijiji wa Kidabaga wamechukua hatua na kuhakikisha kuwa viongozi hao
wameondoka madarakani lakini hawajafikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya
kuumiza wanawake na kuharibu ujauzito wao,” anasema mwanakijiji mmoja ambaye
hakutaka jina lake kiusalama.
Akina
mama wa Kimasai nao wanapigwa lakini mila zao haziruhusu kushitaki. “Hata kama
ameumizwa hawezi kusema badala yake huchinjiwa kondoo na kupewa mafuta kama
tiba,” anasema Lea Saitobiki, Mjumbe wa Halmashauri ya Kijiji akihojiwa katika
utafiti huo.
Anasema
hata kama utasikia amepigwa ukienda kumuuliza anakataa kata kata kuwa amepigwa.
Kufuatia masuala hayo kufanywa siri, hakuna takwimu zinazoonyesha tatizo la
vipigo kwa wanawake lina ukubwa gani katika kata hiyo.
“Sisi
kama serikali tunashindwa kuingilia mambo ya kifamilia, huwezi kwenda kwenye
nyumba ya mtu ukaanza kuuliza wewe kwa nini unampiga mke wako wakati mke
mwenyewe hajawahi kuja kuripoti,” anasema Ofisa Mtendaji Kata ya Mwembe,
Athumani Mkumbwa.
Kuna
haja sasa ya Serikali kwa kushirikiana na wadau anuai kuhakikisha
inapiga vita vitendo hivi vya vipigo kwa kundi hili ikiwa ni pamoja na
kutoa elimu kwa jamii nzima, ili kuona kwamba vipigo kwa wazalishaji
mali hawa haviendelei. Hali hii itaongeza kwa kiasi kikubwa uwajibikaji
kwa kundi hili katika ngazi ya familia hivyo kujikuta inachochea
maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)