Afisa Mtendaji Mkuu wa Twiga Bancorp Limited, Hussein Mbululo (kulia) akifafanua jambo juu ya Tuzo ya Dhahabu waliyo ipata kutoka Geneva Uswis kwa Ubora wa huduma zao, kwa waandishi wa Habari waliotembelea banda la Benki hiyo katika maonesho ya kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam yanayoendelea katika viwanja vya JK Nyerere maarufu Saba Saba barabara ya Kilwa. Pamoja ni wafanyakazi wa Benki hiyo waliopo viwanjanani hapo.
SIKU chache baada ya kupokea Tuzo ya dhahabu ya Kimataifa ya utoaji bora wa huduma, Benki inayomilikiwa na Serikali ya Twiga Bancorp, imeweka hadharani siri ya kupewa tuzo hiyo inayojulikana kama Century International Gold Quality ERA.
Benki ya Twiga Bancorp ilikabidhiwa tuzo hiyo karibuni na Kampuni ya Kimataifa ya Business Initiative Directions jijini Geneva Uswis.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo, Hussein Mbululo, alisema huduma ya moneygram inayowezesha Watanzania na watu wa mataifa mengine kutuma fedha nje kwa dakika chache imechangia kuiwezesha benki hiyo kushinda tuzo hiyo.
Tuzo hiyo kwa Benki ya Twiga Bancorp imekuja siku chache baada ya Serikali kupitia kwa Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk. William Mgimwa kuliambia Bunge kwamba Serikali ipo mbioni kuziongezea mtaji benki zake ikiwemo Benki ya Twiga ili kuziwezesha kuboresha huduma zake. Benki nyingine ni Benki ya Wanawake (TWB), Benki ya Posta (TPB) na Benki ya Rasilimali (TIB).
Mbululo alisema huduma nyingine iliyoiwezesha benki hiyo kushinda tuzo hiyo ni utoaji wa mikopo kwa wafanyakazi bila kuwalazimu wafanyakazi hao kuwa na akaunti katika Benki ya Twiga hatua ambayo imewezesha wafanyakazi nchi nzima hata mahali kusiko na benki hiyo kunufaika na mikopo hiyo.
“Walieleza kuridhishwa na huduma zetu kufikia kiwango cha ubora wa juu lakini pia walieleza kuridhishwa na ubunifu tunaoendelea kuufanya katika kuboresha huduma za kibenki nchini ukilinganisha na benki nyingine.
Kupitia huduma za Money gram mtu anaweza kumtumia fedha za ada au dawa kwa mwenzake aliyepo Uingereza au Marekani na akaweza kuzipata ndani ya dakika tano tu jambo ambalo limewavuta watu wengi kutumia benki yetu,” alisema Mbululo.
Alisema benki hiyo pia imetoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Benki Kata za Jamii (VICOBA) katika maeneo mbalimbali hapa nchini hatua ambayo imewezesha kupewa nishani ya kuwa mlezi bora wa VICOBA nchini na kupewa tuzo.Hadi sasa Benki hiyo inahudumia vikundi zaidi ya 150 vya VICOBA.
Alisema benki hiyo inayoendelea kujitanua kwa kufungua tawi moja mkoani kila mwaka, hivi karibuni itafungua tawi jipya mkoani Dodoma na hivyo kuifanya kuwa na matawi Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Dodoma, huku tawi la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam, likiendelea kuvunja rekodi ya kufunguliwa kwa saa 24 kwa siku zote saba za wiki.
Alisema mtandao wa huduma kwa benki hiyo umeimarika kutokana na kadi zake za ATM kuweza kuunganishwa na Mtandao wa Umoja wenye kuzihusisha benki zaidi ya 24, zikiwa na mtandao wa zaidi ya ATM 160 nchi nzima.
Kuhusu mtaji utakaongezwa na serikali kwa benki hiyo, Mbululo alisema fedha hizo zitasaidia kuboresha huduma za benki hiyo kwa kuwezesha kujenga matawi mapya, kununua mashine na kununua kompyuta na vifaa vyake ili kutanua zaidi huduma zake na kuwezesha kuwafikia wananchi wengi.
Afisa Mwandamizi, Mwendeshaji, Lydia Matembele akitoa maelezo kwa vijana waliotembelea banda lao katika maonesho ya Kimaifa ya Biashara maarufu saba saba .
Banda la Twiga Bank lipo kando ya lango kuu la Kuingilia Karume Hall.
Benki ya Twiga Bancorp inatoa huduma ya kuweka na kuchukua fedha dirishanai au katika ATM yake iliyopo viwanja vya Sabasaba kama mmoja wa wateja wa Umoja Switch anavyofanya.
Mkuu wa Uendeshaji Richard Kombole (kulia)akizungumza na mteja nje ya Banda lao
Afisa Mwandamizi, Mwendeshaji, Lydia Matembele akimsikiliza Mfanya Biashara, Yahia Idriss wa Kampuni ya Giad Sewedy Cables ya Nchini Sudan alipofika kupata huduma ya kubadilishiwa fedha katika Banda hilo la Maonesho linalofanya huduma kamili za Kibenki.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)