Na Joachim Mushi, wa Thehabari.com
MAMA wa mwanafunzi Mwenjuma Magalu aliyechaguliwa kujiunga
na Shule ya Sekondari Komnyang’anyo wilayani Handeni na kushindwa kujiunga na
shule hiyo kutokana na familia hiyo kutelekezwa na baba amefariki dunia.
Mama huyo Hadija Magalu amefariki dunia juzi ikiwa ni muda
mfupi baada ya kujifungulia nyumbani kwake hali iliyomfanya apoteze damu nyingi
hatimaye kuzidiwa na kufariki dunia.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo mtoto wa mama huyu (Mwenjuma
Magalu) amezitoa kwa mwandishi wa habari hizi, alisema mama yake alifariki
dunia muda mfupi baada ya kujifungua pamoja na kichanga chake wakati ndugu na
jamaa walipokuwa wakifanya taratibu za kumpeleka hospitalini kutokana na hali
yake kuwa mbaya.
Marehemu Hadija Magalu mkazi wa Kijiji cha Msasa ndiye
aliyekuwa akiwalea wanae watatu akiwemo Mwenjuma Magalu, baada ya baba wa
watoto hao kuwatelekeza, kitendo ambacho kilimfanya mama huyo kushindwa kumudu
baadhi ya mahitaji ya familia ikiwemo gharama za masomo ya sekondari.
Mapema Desemba 12, 2011 marehemu alishindwa kumlipia mwanae,
Mwenjuma Magalu gharama za masomo (sh. 72,000) hali iliyomfanya mtoto huyo
kukata tamaa ya kuendelea na shule kabla ya kuanza kufanya vibarua kwa moja ya
kampuni za Kichina zinazojenga barabara inayopita Kijiji cha Msasa.
Hata hivyo licha ya familia hiyo kukumbwa na msiba huu
mzito, faraja iliyopo kwa sasa ni kitendo cha kujitokeza kwa wasamaria ambao
wameahidi kumsomesha mwanafunzi Mwenjuma Magalu hadi hapo atakapo maliza elimu
ya kidato cha nne.
Tayari mwanafunzi
huyo amerudi shuleni na kuanza masomo baada ya wafadhili kuanza kumgharamia
masomo yake ya sekondari katika shule ya Sekondari Komnyanganyo.
*Habari hii
imeandaliwa na mtandao wa Thehabari.com (www.thehabari.com)
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)