Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Naura, Ndugu
Sunday G. Mshobozi ambaye pia ndiye mwalimu pekee wa somo la Fizikia
kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha nne.
Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Sekondari
ya Naura, Ndugu Mary Shirima akifanya mahojiano na mwandishi kufahamu
changamoto zinazoikabili shule hiyo
Baadhi ya wanafunzi wanaosoma shuleni hapo wakiwa katika
muda wa mapumziko
Wanafunzi wakiwa katika muda wa mapumziko wakati wenzao
wa kidato cha tano wakiendelea na mitihani ya mock
Nyumba pekee ya Walimu iliyoko shuleni hapo ingawa
haitumiki kwa kuwa haijakamilika
-----
Uchunguzi uliofanywa na Shirika la HakiElimu umegundua
kuwa Shule ya Sekondari ya Naura iliyoko katika kata ya Lemara , eneo
la Njiro ni miongoni mwa shule zenye maendeleo hafifu ya kielimu ukilinganisha
na shule nyingine za serikali na kata zilizoko katika Manispaa ya Wilaya
ya Arusha.
Shule hii iliyoanzishwa mwaka 2008 , inakabiliwa na
upungufu mkubwa wa walimu kwani kuna masomo hayajawahi kuwa na walimu
toka shule hiyo ianzishwe mfano masomo ya Chemistry, Mathematics
na Book- Keeping . Pia kuna masomo ambayo yana mwalimu mmoja mmoja
mfano English, Commerce, Literature, na Civics toka kidato cha
kwanza mpaka cha nne.
Tofauti na shule nyingine ambazo hukimbiwa na walimu
kutokana na kuwa mazingira magumu shule hii iko eneo zuri na maarufu
waishio watu wenye kipato cha juu mkoani Arusha lijulikanalo kama Njiro
na kuacha maswali kuwa kama kuna tatizo la uongozi wa shule au kuna
tatizo la upangaji wa walimu unaofanywa na serikali , hili hali shule
nyingine zikiwa na walimu lukuki.
Akielezea sababu nyingine za kudorora kitaaluma shuleni
hapa Mwalimu Mshobozi alisema kuna mrundikano mkubwa wa wanafunzi kushinda
uwezo wa shule akitolea mfano wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato
cha kwanza kwa mwaka huu kufikia 307. Tofauti na malengo ya shule
ya kata kusomesha wanafunzi wa maeneo ya karibu , wanafunzi wa
shule hii wanatoka katika kata zote zilizoko manispaa hii kukiwa na
umbali mrefu na kukabiliwa na shida kubwa ya usafiri jambo ambalo pia
alilielezea kuwa ni moja ya sababu za kudorora kitaaluma kwa wanafunzi
wa shuleni hapo.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu msaidizi Bi Mary Shirima
alisema sababu za kudodora kitaaluma kwa shule yake ni mwako mdogo wa
kielimu kwa wazazi pamoja na watoto wenyewe akisema wengi wa wanafunzi
ni kama wamelazimishwa kuja kusoma shuleni hapo na wazazi wao hawajishughulishi
na maendeleo ya watoto wao. “ Historia ya wanafunzi waliomaliza
kidato cha nne ni tata kwani kuna waliokuwa wameolewa na wafanyabiashara
mara baada ya kumaliza darasa la saba ,ghafla wakasikia wamechaguliwa
kujiunga na kidato cha kwanza na kulazimika kuja shuleni, sasa katika
hali hiyo unatarajia nini” aliuliza Mwalimu Shirima.
Katika mtihani wa kidato cha nne wa taifa wa mwaka
jana 2011 jumla ya wanafunzi 164 walifanya mtihani huo ambapo
hakuna aliyepata daraja la kwanza wala la pili, wanafunzi 2 walipata
daraja la tatu , 24 wakapata daraja la nne na 138 walifeli kwa kupata
zero. Shule hii ilishika nafasi ya mwisho kati ya shule 137 zilizofanya
mtihani huo katika mkoa wa Arusha. Kitaifa ilishika nafasi ya 2994 kati
ya 3108 zilizofanya mtihani huo.
HakiElimu inatoa wito kwa Serikali kupitia mamlaka
husika kuangalia upangaji wa walimu na uchaguzi wa wanafunzi shuleni
hapo. Wazazi na wakazi wa Njiro nao wanatikiwa kuchukua jitihada za
ziada kuhakikisha wanafunzi walioko shuleni hapa wanapata elimu bora
na kuelimika .Uongozi wa shule nao ni siri ya mafanikio au kushindwa
kufanya vema , hivyo uongozi wa Shule ya Sekondari Naura uongeze jitihada
kuhakikisha shule hii inafanya vema kama shule za Kaloleni, Ngarenaro
na Arusha Day .
Habari hii imeandaliwa na
Idara ya Habari na Utetezi
HakiElimu
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)