Wakati Bunge liko kwenye mchakato wa Bajeti
ya 2012/13, yameanza kujitokeza maneno na taarifa mbalimbali juu ya kupanda kwa
mishahara ya watumishi wa Umma wakiwemo Wabunge. Mathalani, siku ya Jumatano
tarehe 20 Juni 2012, gazeti moja linatokalo kila siku lilikuwa na habari yenye
kichwa kisemacho “Mishahara ya Wabunge
juu”.
Ofisi ya Bunge imeona ni vyema kutoa ufafanuzi
juu ya suala zima la mishahara ya Wabunge ili umma uweze kuelimika ipasavyo juu
ya taratibu zinazotawala jambo hili kama ifuatavyo:
·
Bajeti
ya Ofisi ya Waziri Mkuu, ambayo inajumuisha Fungu Na. 42 lenye Bajeti ya Bunge
bado haijasomwa Bungeni, na hivyo haiwezekani leo hii kueleza kuwa kuna
nyongeza ya bajeti inayohusu mishahara kwa Wabunge.
·
Si
kweli kwamba mishahara ya Wabunge imeongezwa toka kiwango wanacholipwa sasa,
kwa kuwa mishahara yao kama ilivyo ya watumishi wote wa umma, hurekebishwa kwa
waraka maalum toka Ofisi ya Rais, na si Kamisheni au Kamati yoyote ya Bunge.
·
Waraka
wa mwisho wa toka Ofisi ya Rais unaotoa Masharti ya Kazi ya Mbunge ulitolewa
tarehe 25 Oktoba 2010, na kueleza kuwa Mbunge atalipwa mshahara katika ngazi ya
LSS (P) 2, na ni waraka huo unaotumika mpaka sasa.
·
Mapendekezo
ya ongezeko la 32% ya Bajeti ya Ofisi ya Bunge yaliyooneshwa kwenye kitabu cha
Bajeti namba 2, cha matumizi ya kawaida yaliyowasilishwa mezani ni ya matumizi
mengine ambayo hayana uhusiano na ongezeko la mishahara.
Mwisho, Ofisi ya Bunge wakati wote inathamini
sana mchango wa vyombo vya habari katika juhudi za kuelimisha umma juu ya kazi
za chombo chao cha uwakilishi. Hata hivyo, Ofisi inasikitishwa sana na habari
za upotoshaji zinazotolewa kwa lengo la kujenga chuki kati ya Wabunge na watu
wanao wawakilisha.
Kwa mantiki hiyo, tunazidi kuwasihi Waandishi
waandike habari au makala baada ya kufanya utafiti wa kina kuhusu jambo husika
na pale inapobidi waweze kupata ufafanuzi toka Idara husika katika Ofisi ya Bunge,
ili kuepuka kuupotosha umma.
Imetolewa
na:
Idara
ya Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa
Ofisi ya Bunge,
S.L.P 941, DODOMA.
21 Juni 2012
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)