Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishana
Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi Bw, Zelothe Stephen, Kulia akitoa
maelezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dk. Rehema Nchimbi kuhusu Vifo vya
wahamiaji Haramu Raia wa Ethiopia, Kushoto akisikiliza ni Mkuu wa polisi
Wilaya ya Kongwa Bw. Davis Nyanda.
Na.Luppy Kung’alo wa Jeshi la Polisi Dodoma
DODOMA, JUNE 27, 2012. Jeshi la Polisi mkoani Dodoma limewakamata wahamiaji haramu Themanini na
Mbili (82) wote wanaume wenye asili ya Ethiopia
jana majira ya 08:OOHRS asubuhi baada ya
kuonekana wakitanga tanga katika vijijji vya
Chitego na Mkoka Tarafa ya ZOISA Wilayani Kongwa mjini hapa.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma. Bw. Zelothe Stephen kuhusu vifo vya Wahamiaji Haramu arobaini na tatu (43)
vilivyotokea jana mjini humo alisema Raia hao wote wanatoka Kanda
ya Kusini nchini Ethiopia kwenye vijiji vya Kambata, Hadia na Sirite.
Alisema Kukamatwa watu hao walioingia nchini bila kibali kupitia mpaka wa
Tanznia na Kenya wakielekea nchini Malawi kulifanikwa baada ya wananchi wema
kuwaona na kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ambapo walifika na kufanya
Operesheni Maalum ya Kuwasaka na kuwakamata.
”Wananchi kutoka vijiji hivyo ambavyo vipo umbali
wa kilometa 141 toka Dodoma mjini waliweza kuona maiti nyingi zimetupwa kando ya barabara ya Kiteto – Dodoma na
baadaye kuwaona watu wengine walio hai katika harakati za kupita Porini
kuelekea kijiji cha Izava Wilayani Chamwino hivyo kuingiwa na hofu na kutoa
taarifa hizo.”aliongeza Kamanda Zelothe.
Alisema baada ya kupata Taarifa hizo, Jeshi
la Polisi lilifika katika eneo hilo
ambako walishirikiana na wananchi wa eneo hilo, hadi kufikia jioni hiyo walifanikiwa
kuwakamata raia hao wa Ethiopia wapatao
82 ambao walikuwa wakizungumza lugha ya kiingereza cha kubabaisha.
Kamanda Zelothe Stephen alisema kwa mujibu ya maelezo ya raia hao walisema kwamba
walianza safari yao takribani miezi mitano iliyopita wakitokea Ethiopia
kuelekea nchini Malawi, kupitia nchini Kenya ambako walidai kuwa ndiko kituo
kikubwa cha wao kukusanywa na kuanza safari ya pamoja.
”Walipofika Arusha walitawanywa
katika vikundi vidogo na kuhifadhiwa kwenye nyumba mbalimbali huku wakipewa
chakula kidogo na maji na kwamba siku ambayo hawakumbuki walikusanywa usiku na
kupakiwa kwenye lori moja lililofunikwa kote na kuanza safari kuelekea Malawi.”
alisistiza Bw. Zelothe
Aidha Mkuu huyo wa Polisi Mkoani Dodoma alisema kuwa
raia hao wakiwa njiani baadhi yao
walianza kuzirai na kufariki, hivyo walifanya jitihada za kupiga kelele na
kumgongea dereva lakini hakuwa tayari kusimama hadi walipokuja kutelekezwa
usiku wa manane kwenye eneo la tukio hilo na lori hilo kutoweka.
Akizungumzia Hali za maiti katika eneo zilipotupwa, alisema maiti nyingi zilionekana zikiwa tayari zimeanza kuharibika
ambapo jumla ya maiti (22 ) zilisafirishwa
kwenda kuhifadhiwa katika Hospitali ya Serikali ya Mkoa wa Morogoro na nyingine
(21) zimehifadhiwa kwenye Hospitali ya Serikali Mkoa wa Dodoma kusubiri uchughuzi wa Daktari na
taratibu.
Wakati huo huo Kamanda Zelothe amesema huduma za kibinadamu zimekuwa zikitolewa
kwa raia hao wa kigeni, na mahali waipohifadhiwa ni jirani na kituo cha
Polisi Kati Mkoani Dodoma kwa ushirikiano na taasisi nyingine ikiwa ni pamoja na
Idara ya Afya, Red Cross, Uhamiaji na Uongozi wa Mkoa.
Kamanda Zelothe Stephen aliwashukuru wananchi wa Vijiji vya Chitego na
Mkoka kwa kutekeleza zana ya Polisi
Jamii na Ulinzi Shirikishi kwa kutoa taarifa za tukio hilo, aidha wito kwa
wananchi wote kuendelea kutoa taarifa za matukio mbalimbali wasiyoyaelewa
katika kamati za Ulinzi na Usalama katika ngazi za Kijiji, Kata, Tarafa. Wilaya
na Serikali Kuu ili kuweza kudhibiti uhalifu katika maeneo yetu.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)