BABA wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, mzee Steven Mwaitenda
Baba wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, mzee Steven Mwaitenda akilia na kufarijiwa
Usu Mallya akilia baada ya kushuhudia mzee Steven Mwaitenda akibubujikwa na machozi mbele yao
Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Usu Mallya (kushoto) akiwa na Mkuu wa
Kitengo cha Habari na Mawasiliano, Lilian Liundi walipomtembelea Dk.
Ulimboka kumfariji jana
Mzazi akimlilia mwanaye Dk. Ulimboka kwa uchungu MOI
Baadhi ya wanaharakati anuai wakiwa na maua walipomtembelea Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Ulimboka kumfariji jana
Baadhi ya wanaharakati wakiwa na nyoso za hudhuni baada ya kilio cha baba wa Dk. Ulimboka jana MO
Baba wa Dk.
Ulimboka aangua kilio MOI
Na Joachim Mushi, Thehabari.com
BABA wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, mzee Steven
Mwaitenda amejikuta akiangua kilio kwa uchungu mbele ya wanaharakati ambao
walimtembelea mwanae, Dk. Steven Ulimboka kumpa pole kufuatia tukio la kutekwa
na kujeruhiwa vibaya na watu wasiojulikana.
Hali hiyo ilitokea jana jioni katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa
Muhimbili (MOI), ambapo wanaharakati kutoka taasisi na asasi mbalimbali za
utetezi wa haki za binadamu walifika kwa lengo la kumpa pole Dk. Ulimboka
kufuatia kitendo kilichomfika.
Mzee Mwaitenda alijikuta akibubujikwa na machozi na
kushindwa kuendelea kuzungumza alipokuwa akitoa shukrani kwa wanaharakati hao,
kwa niaba ya mwanaye ambaye wanaharakati hao walishindwa kumuona wote kutokana
na hali yake ilivyo sasa.
“Niseme wazi nimefarijika sana kwa ujio wenu kumwona mwanangu dhidi ya
mambo ya kikatili aliyofanyiwa akitetea haki za wengine…,” alisema mzee
Mwaitenda kabla ya kushindwa kuendelea na kuangua kilio mbele ya wanaharakati.
Baada ya tukio hilo
baadhi ya wanaharakati walimshika wakishirikiana na wanafamilia ya mzee Mwaitenda
na kumbebeleza kisha kumtoa mbele ya mkusanyiko huo wa wanaharakati na
kumrudisha wodini huku wakimfariji.
Wakizungumza mara baada ya tukio hilo wanaharakati wameelezea kusikitishwa na
vitendo vinavyoendelea MOI eneo ambalo amelazwa kiongozi huyo wa madaktari
ambavyo vimeendelea kutishia usalama wa Dk. Ulimboka.
Akifafanua zaidi mwakilishi wa wanaharakati hao, Markos Albania alisema
taarifa walizozipata usiku wa juzi kuna wagonjwa ‘feki’ ambao walijitokeza MOI
huku wakitaka kulazwa wodi ya Wagonjwa Mahututi (ICU) alipolazwa Dk. Ulimboka
lakini baadaye waligoma kuingizwa wodini.
“Wapo wagonjwa ambao waliletwa na kutaka kupelekwa ICU moja
kwa moja…kuna watu wanakuja usiku wa manane wakitaka kumtembelea Dk. Ulimboka…matendo
yanayoendelea kutokea ukilinganisha na kauli za Serikali zilizotolewa bungeni
yanatishia usalama na uhai wa mgonjwa,” alisema Albania.
Aidha amesema kitendo cha vyombo vya usalama kuendelea
kumuhoji Dk. Ulimboka akiwa hoi hospitalini si vya kiungwana kwani tayari
muhusika amewataja hadi kwa majina watu ambao anawashuku lakini hadi sasa
hakuna aliyechukuliwa hatua yoyote.
Pamoja na hayo wanaharakati hao wameitaka Serikali kuunda
tume huru mchanganyiko na raia ambayo itachunguza kiundani suala hilo, kwani hawana imani na Jeshi la Polisi ambalo limedai
kuunda timu ambayo inachunguza kwa kina suala hilo.
Dk. Ulimboka ambaye ni kiongozi wa madaktari ambao
wanaendelea na mgomo wan chi nzima kuishinikiza Serikali kutekeleza madai yao alitekwa juzi na watu
wasiojulikana na kupigwa na kuteswa kikatili kabla ya kutelekezwa katika msitu
wa Mabwepande.
*Habari hii imeandaliwa na Mtandao wa Thehabari.com (www.thehabari.com)
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)