SAFARI LAGER KUDHAMINI MASHINDANO YA MCHEZO WA POOL TABLE KWA WANAFUNZI WA VYUO VYA ELIMU YA JUU. - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

SAFARI LAGER KUDHAMINI MASHINDANO YA MCHEZO WA POOL TABLE KWA WANAFUNZI WA VYUO VYA ELIMU YA JUU.

Meneja wa Bia ya Safari Lager, Oscar Shelukindo (kulia) akimkabidhi kombe Mwenyekiti wa Chama cha Pool Taifa(TAPA) Isach Togocho ikiwa ni zawadi ya mshindi wa kwanza atakayopewa katika mashindano ya Poool  vyuo vikuu  yaliyozinduliwa rasmi Dar es Salaam jana.Kushoto ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Amos Kafyinga. Bingwa wa Singles,mwaka jana kutoka Chuo cha IFM, Charles Evance akizindua rasmi mashindano hayo 
Mchezaji wa Pool, Rahma Kosei akicheza kuashilia uzinduzi huo upande wa wakinadada ambao mwaka huu watashiriki kutoka chuo cha CBE.
Amos Kafyinga akizungumza na waandishi wa habari
Mwenyekiti akizungumza
 
KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Safari Lager leo imetangaza rasmi kudhamini kwa mara nyingine tena mashindano ya mchezo wa Pool Table kwa vyuo vya elimu ya juu hapa Tanzania. Mashindano haya yajulikanayo kama “Safari Lager Higher Learning Pool Championships” yanafanyika kwa mwaka wa tatu sasa, Safari Lager imekuwa wadhamini wakuu wa mashindano haya kwa miaka yote hii mitatu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar Es Salaam leo meneja wa Safari Lager Bwana Oscar Shelukindo alisema nia hasa ya kudhamini mashindano haya ni kuwapa wanafunzi burudani baada ya ratiba ngumu za masomo ili waweze kupumzisha akili warudi wakiwa na ari mpya. Mapumziko husaidia akili kufanya kazi kwa haraka na kuwa na ubunifu zaidi. Bw. Shelukindo aliendelea kusema “Mbali na kupumzisha akili, michezo husaidia kuwakutanisha watu mbalimbali, kujenga afya bora na katika mazingira yetu ya sasa mchezo wa Pool umekua zaidi na unaweza kuwa kama fani nyingine zinazomuingizia mchezaji pesa”. Safari Lager imekuwa wadhamini wa mchezo wa Pool toka mwaka 2008, imedhamini mashindano ya ndani na ya nje ya nchi pia. Imedhamini timu ya Taifa ya mchezo wa Pool kushiriki mashindano ya dunia ya mchezo wa Pool nchini Ufaransa mwezi wa kumi mwaka 2010 ambapo timu yetu ilifanya vizuri.

Naye Bw. Amos Kafwinga, katibu wa chama cha mchezo wa Pool Tanzania (TAPA) alisema mashindano haya yanaanzia kwa vyuo kushindana katika ngazi ya mkoa na baadae mikoa yote itashindana katika ngazi ya taifa ili kupata mshindi wa jumla kwa vyuo vyote. Mashindano ya mwaka huu yanatarajiwa kuanza rasmi kutimua vumbi katika mkoa wa Morogoro Jumamosi ijayo tarehe 12 May 2012. Mashindano ya mwaka huu yatahusisha wanafunzi wa vyuo vilivyo katika mikoa ya Morogoro, Dodoma, Iringa, Mbeya, Kilimanjaro, Arusha, Mwanza na Dar Es Salaam. Mashindano ya taifa mwaka huu yatafanyika katika mkoa wa Iringa mwanzoni mwa mwezi wa sita.
Mwaka jana chuo cha Usimamizi Wa Fedha (IFM) kiliibuka na ushindi katika mashindano ya kitaifa yaliyofanyika mkoani Dodoma, walijipatia kikombe na jumla ya shilingi milioni mbili na laki tano. Akizungumzia ushindi huo Bwana Charles Venance ambaye ni mwanafunzi wa chuo hicho na kiongozi wa timu ya pool ya chuo alisema fedha hizo ziliwasaidia katika mahitaji mbalimbali ya masomo. Alisema “Tumejiandaa vizuri sana mwaka huu na kwa hakika ushindi utabaki IFM, vyuo vyote vitakubali kwamba IFM ni moto wa kuotea mbali kwenye Pool!”.

Akitoa shukrani kwa Safari Lager kwa niaba ya Chama cha Mchezo wa Pool Tanzania (TAPA), Mwenyekiti wa chama hicho Bw. Isaac Togocho alisema “Taswira ya mchezo wa pool hapa nchini imebadilika kwa kiasi kikubwa na sasa inawavutia vijana wa kaliba mbalimbali kwani si mchezo wa kupotezea muda tena kama wengi walivyodhania, Pool ni miongoni mwa michezo inayokua kwa kasi kubwa na kuwapatia kipato wachezaji na vijana kwa ujumla. Hii yote imetokana na Bia ya Safari Lager kukubali kuudhamini mchezo wa Pool table. Kwa niaba ya chama tunatoa shukrani nyingi sana na kuomba Safari Lager iwe nasi ili tuendelee mbele zaidi”.
  
Bwana Oscar alizitaja zawadi za washindi katika ngazi ya mikoa kuwa timu itakayoshinda itajipatia kitita cha shilingi laki tano, washindi wengine watajipatia shilingi laki tatu kwa mshindi wa pili, laki mbili na laki moja kwa mshindi wa nne. Washindi kwa upande wa mchezaji mmoja mmoja wa kiume watajipatia shilingi laki moja na nusu kwa bingwa na laki moja kwa mshindi wa pili. Wachezaji wa kike watajipatia laki moja kwa bingwa na shilingi elfu hamsini kwa mshindi wa pili. Mshindi katika ngazi ya taifa ataibuka na kikombe pamoja na jumla ya shilingi milioni mbili taslim, jumla ya shilingi milioni tisa na laki tano zitatolewa kama zawadi katika michuano ya ngazi ya taifa.

Bwana Oscar alimalizia kwa kutoa shukrani kwa wanywaji wa bia ya Safari Lager na wachezaji wote wa mchezo wa Pool kwa ujumla, aliwaomba wajinoe kwani Safari Lager inadhamini tena mashindano ya kitaifa ya mchezo wa pool ambayo yataanza hivi karibuni.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages