Ndugu Mfutakamba akiwa mitaa ya Iringa na picha ya chini
alipotembelea Chuo Cha Maendeleo ya Wananchi Ilula kuzindua mradi wa
kuifadhi maji ya mvua
---
Ndugu zangu,
Ujamaa ni imani. Na Wajamaa tuko wengi nchi hii.
Kuna
tuliojifunza tangu utotoni, kwamba Ujamaa ni imani. Tunajitahidi kuishi
kama tulivyojifunza. Kuishi kama tunavyohubiri sasa. Lakini, kama
ilivyo kwa imani nyingine, ni jambo gumu, ni mitihani kila kukicha,
naam, Uislamu ni mgumu, Ukristo ni mgumu. Hivyo basi, na Ujamaa pia.
Ndugu
yangu Athumani Mfutakamba ( Pichani juu) ameondolewa kwenye Baraza
jipya la JK. Nimesikitika, ni kwa vile, Mfutakamba niliyemfahamu tangu
tukiwa nae hapa Iringa si yule niliyekuwa nikimsoma kwenye media siku za
karibuni. Kwamba imeandikwa kuwa ana ugomvi na Waziri mwenzake Omar
Nundu. Na ugomvi wenyewe ulikuwa na harufu ya kugombania ’ maslahi
binafsi’- mambo ya rushwa na milungula.
Mfutakamba
niliyemfahamu mie niliamini kuwa alikuwa ni Mjamaa mwenzangu wa
Kidemokrasia( Social Democrat). Aliishi kama alivyohubiri. Hakuwa na
makuu. Mjini Iringa ilikuwa nadra kumwona akiwa kwenye gari kwenye mitaa
ya mji. Tulitembea nae kwa miguu. Tulisimama wote kwenye meza za
magazeti, kusoma na kupiga gumzo. Ilikuwa vigumu kwa wengi kutambua kuwa Mfutakamba alikuwa na cheo cha U-DC. Mfutakamba alishuka chini kwa wananchi.
Nakumbuka
miaka kadhaa iliyopita niliratibu maombi ya fedha kiasi kutoka Shirika
la misaada la Sweden ili zikisaidie Chuo Cha Maendeleo ya Wananchi Ilula
kijenge matanki ya kuhifadhi maji ya mvua. Tulichoomba kama msaada ni
kiasi kidogo, lakini, nguvu kazi ya kujitola ya watu wa Ilula ilitumika
zaidi katika kufanikisha mradi huo.
Mradi
ulipokamilika, nilifanikisha mawasiliano na Ndugu Mfutakamba, kama DC
wa Kilolo, aje kutufungulia rasmi mradi huo na kusema mawili matatu.
Mfutakamba aliitikia wito wetu, alifika na kuifanya kazi hiyo kwa
gharama za Serikali. Hatukuombwa mchango wowote wa mafuta ya gari ya
Mfutakamba kufika Ilula kutoka umbali wa kilomita zaidi ya mia moja.
Ndio,
huyo ndio Ndugu Mfutakamba niliyemfahamu; hakutanguliza maslahi
binafsi, bali ya wananchi. Ndiye Mfutakamba tuliyekunywa nae chai, na
tulikula nae chakula cha pale kwa ’ Baba Nusa’- moja ya migahawa ya watu
wa kawaida kabisa hapa Iringa. Ukweli, si mara moja,
nilikaa na ndugu Mfutakamba pale kwa ’ Baba Nusa’ na kujadili mambo ya
wananchi na changamoto za maendeleo yao.
Niliposikia JK amemteua Mfutakamba kuwa Naibu Waziri, nikasema, Naam, hapo JK amepata kiongozi mtumishi wa watu.
Hakika, habari
kuwa Mfutakamba amekubali kupandishwa ndege na Wachina kwenda ’
kutalii’ nchi kadhaa na hatimaye kukaa chini na waliompandisha ndege
kujadili masuala ya tenda za ujenzi wa gati hii na ile pale Bandarini
zilianza kunitia mashaka. Si Mfutakamba yule niliyemfahamu.
Yumkini
mjini kuna mengi na mambo mengi ya kuwatamanisha viongozi kutaka
kujipatia fedha nyingi zaidi, na kwa haraka. Na ukawa mtihani kwa ndugu
yangu Mfutakamba.
Na katika maisha kuna kuanguka. Sote tumepata kuanguka, nani ambaye hajaanguka. Kilicho muhimu kwa mwanadamu ni kujifunza kutokana na anguko. Si kusimama na kujiendea zako kana kwamba hakuna kilichotokea.
Naamini,
Ndugu yangu Athumani Mfutakamba moyoni bado ni Mjamaa wa Kidemokrasi- A
Social Democrat. Anaweza kujisafisha kutoka kwenye kashfa iliyomkuta,
na hatimaye kurudi tena.
Naam, Ujamaa ni Imani, sidhani kama mwenzangu Athuman Mfutakamba imemshinda kabisa.
Na hilo Ni Neno La Leo.






No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)