Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohammed Gharib
Bilal akihutubia kwenye mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu
Maendeleo Endelevu katika Bara la Afrika leo mjini Gaborone.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohammed Gharib
Bilal akizungumza na Rais wa Liberia Bibi Ellen Johnson Sirleaf kwenye
mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Maendeleo Endelevu Barani
Afrika leo mjini Gaborone
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohammed Gharib
Bilal akiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa Nchi pamoja na
wawakilishi kutoka nchi za Afrika waliohudhuria mkutano wa Maendeleo
Endelevu katika Bara la Afrika.PICHA NA VPO
TAARIFA KWA VYOMBO VYA
HABARI
MAKAMU WA RAIS DKT. MOHAMMED GHARIB
BILAL AMWAKILISHA RAIS KATIKA MKUTANO WA MAENDELEO ENDELEVU AFRIKA JIJINI
GABOFRONE, BOTSWANA TAREHE 24 MEI, 2012
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Dkt. Mohammed Gharib Bilal amemwakilisha Rais
Jakaya Kikwete katika mkutano wa Maendeleo Endelevu Afrika unaolenga katika
kujumuisha thamani ya Rasilimali Asilia katika kupima maendeleo ya kiuchumi katika
nchi za Afrika.
Katika
mkutano huo, Tanzania imeunga mkono kuanzishwa kwa mfumo wa kujumuisha thamani ya
raslimali asilia ambao utahusishwa kwenye tathmini ya pato la taifa kwa manufaa
ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Makamu
wa Rais alisema wakati akihutubia mkutano huo leo Alhamis Mei 24, 2012 kuwa,
mchango wa rasilimali asilia zina nafasi kubwa katika kuchangia katika pato la
taifa lakini ili mchango wake utambulike, nchi zinahitajika kuwa na utaratibu
wa kuzifanyia tathmini hasa kuhusu matumizi yake na faida zake katika uchumi
huku pia athari zake zikitazamwa hasa zile zinazotokana na kupoteza uhalisia wa
mazingira ama kuharibu mazingira ya nchi.
“Ni
imani ya serikali ya Tanzania kuwa mpango huu utasaidia kutoa nafasi ya nchi
kujikagua hasa kwa kuzingatia rasilimali zinazotumika na faida inayopatikana.
Tena mpango huu utatoa nafasi kwa nchi kujiuliza kama matumizi ya rasilimali
zake yanalenga kutambua faida ya sasa na siku zijazo ili kuhakikisha kuwa
mazingira yanabakia kuwa salama kwa ajili ya vizazi vijavyo,” anasema
Mheshimiwa Makamu wa Rais Katika hotuba yake.
Kwa
mujibu wa Makamu wa Rais, dhana ya kutathmini mazingira na kujumisha raslimali
asilia kwenye hesabu za pato la taifa, kunaweza kusaidia nchi kufikia maamuzi
ambayo yataliwezesha taifa kupata maendeleo endelevu hali ambayo itachangia
jitihada za kupunguza umaskini na kukuza uchumi.
“Tathmini
ya hesabu kuhusu maendeleo, ukijumuisha na hesabu za raslimali asilia, zinaweza
zikatupa takwimu za kina kwa ajili ya kusimamia vizuri uchumi,” anaeleza Makamu
wa Rais na kuongeza:
“Tena
kwa upande mwingine, hesabu za mapato katika sekta za maji, nishati na
nyinginezo, udhibiti wa uchafu wa mazingira na hali kadhalika matumizi makubwa
ya raslimali zinahitajika ili kukuza uchumi na wakati huo huo zikitakiwa
kufanyiwa tathmini ya faida zake na hasara kwa mazingira na hali ya nchi katika
miaka ijayo.”
Katika
mkutano huo, pia kumejadiliwa suala la umuhimu wa serikali za nchi za Afrika
kutazama upya sera na mikakati ya nchi
hizo na kuweka mikakati inayolenga
katika kutunza mazingira ambayo itawezesha kupata maamuzi ya busara yatakayohakikisha upatikanaji wa maendeleo
endelevu.
Dkt.
Bilal anaueleza mkutano huo kuwa, Tanzania iliona umuhimu wa raslimali asilia
tangu nchi ilipopata uhuru mwaka 1961 ambapo iliweza kutenga asilimia 30 ya
eneo la nchi kwa ajili ya wanyama na viumbe hai. Tena ziliwekwa sera nzuri
zilizolinda uvunaji wa raslimali hizo kwa manufaa ya taifa.
“Dunia
hivi leo inakabiliwa na matumizi yasiyo endelevu ya raslimali asilia.
Tumemaliza benki ya raslimali asilia kwa kuwa matumizi yamekuwa makubwa zaidi
kwenye uvuaji wa samaki, uvunaji wa misitu, hewa iliyopo na vingine vingi
vilivyobaki. Mbaya zaidi, tumekuwa tukitumia vibaya raslimali hizo wakati zaidi
ya watu bilioni moja wanaishi katika umaskini uliokithiri, “ anasema
Makamu
wa Rais ameueleza mkutano huo pia kuwa, nchi nyingi za Afrika zinategemea
kilimo kama njia kuu ya uchumi na sekta hii bado inategemea mvua huku
ikihusisha wakulima wadogo wadogo hali ambayo inaonesha ma mazingira
yataharibiwa ni wazi maisha ya wengi yataathirika. Anasisitiza kuhusu kuwepo
kwa mfumo mpya wa kilimo unazingatia kutoharibu rasilimali asilia na wakati huo
huo kuhakikisha kuwa mazingira yanabaki kama yalivyo ili yasaidie jamii zijazo.
Akifungua
mkutano huo, Rais Seretse Khama Ian Khama wa Botswana alisema nchi yake
imeandaa mkutano huo kwa lengo la kutaka kuzungumzia masuala ya Afrika kwa
pamoja juu ya maendeleo endelevu na kuangalia namna nchi hizo zinavyoweza
kutumia utajiri wa raslimali za asili katika kukuza maendeleo ya nchi zao.
Katika
mkutano huo, Tanzania na Botswana zimepongezwa kwa uhifadhi wa maliasili na
mazingira kwa ajili ya kizazi cha sasa na cha baadaye.
Mkutano
huo wa pia unahudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka nchi zipatazo 11 wakiwemo
Marais Hifikupenye Pohamba wa Namibia, Bibi Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia,
Waziri Mkuu wa Msumbiji na nchi .
Mkutano
huu ni maandalizi ya mkutano wa Mazingira wa Rio +20 unaotarajiwa kufanyika
nchini Brazil mwezi ujao katika jiji la Rio de Janeiro. Maazimio ya mkutano huu
yanalenga nchi za Afrika kushiriki mkutano huo zikiwa na sauti moja kuhusu
utunzaji wa mazingira na pia kukabiliana na tabia ya uharibifu mkubwa wa
mazingira hasa unaofanywa na nchi tajiri duniani.
Imetolewa
na: Kitengo cha Habari
Ofisi ya Makamu wa Rais
Alhamisi – 24/5/2012
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)